Theresia Gasper -Dar es salaam
BEKI wa Yanga, Andrew Vincent, ‘Dante’, amesema bado hajamalizana na uongozi wa klabu yake hiyo kuhusu fedha anazoidai.
Dante hajaitumikia Yanga tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, akiweka shinikizo la kutaka kulipwa stahiki zake ambazo ni pamoja na fedha za usajili.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Dante alisema kwa sasa anasubiri hadi dirisha Dogo la usajili lifunguliwe na baada ya hapo ndio atafahamu hatma yake.
“Nilianza kufanya mazungumzo vizuri na uongozi lakini badae tukashindwa kuelewana.
“Ila bado naendelea kuwasikilizia hadi hapo dirisha dogo litakapofunguliwa ndio nitafahamu hatma yangu,” alisema Dante.
Alisema kwa sasa ataendelea kufanya mazoezi yake binafsi ili kujiweka fiti huku akisubiri kufahamu hatma yake ndani ya kikosi hicho cha Jangwani.