LONDON, England
KLABU ya Manchester City imekamilisha usajili wa beki wa Real Madrid, Danilo Luiz da Silva, aliyesaini mkataba wa miaka mitano kwa kiasi cha ada ya uhamisho ya pauni milioni 26.5.
Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 26, anatarajia kuungana na kikosi cha Manchester City ambacho kipo nchini Marekani kwa maandalizi ya msimu mpya.
Danilo ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali ya ulinzi pamoja na kiungo, usajili wake ni wa nne kwa Manchester City.
“Nilipata ofa nyingi kutoka klabu mbalimbali lakini kila siku nilitamani kucheza chini ya uongozi wa Pep Guardiola,” alisema Danilo.
Hata hivyo, kocha wa timu ya Real Madrid, Zinedine Zidane, alisema baada ya Danilo na Morata kuondoka wanajipanga kuangalia namna mpya ya kusonga mbele.
“Tumekuwa na wachezaji bora sana ambao wameondoka na bado wengine wanakuja. Daima tunataka kuimarisha timu,” alisema Zidane.
Madrid wataikabili Manchester City katika mchezo wa kirafiki unaotarajiwa kuchezwa Jumatano mjini Los Angeles, Marekani.
Danilo amekamilisha kiasi cha pauni milioni 150 zilizotumiwa na Manchester City kuzipata saini za wachezaji wanne wakiwamo Kyle Walker aliyesajiliwa kwa pauni milioni 45, kiungo wa Kireno, Bernardo Silva, pauni milioni 43, kipa Mbrazil, Ederson Moraes, pauni milioni 35.
Klabu hiyo pia imekubali kutoa kiasi cha pauni milioni 52 kuinasa saini ya beki wa Monaco, Benjamin Mendy na kumuuza beki wao wa kushoto, Aleksandar Kolarov, kuelekea klabu ya Roma kwa ada ya uhamisho wa pauni milioni 4.
Hata hivyo, Danilo huenda akakosekana katika mchezo wa Jumatano timu yake mpya itakapokuwa ikivaana na timu yake ya zamani kwa kuwa bado hajakamilisha kibali cha kufanyia kazi England.
Beki huyo wa zamani wa timu ya Santos ya Brazil, alijiunga Real Madrid mwaka 2015 akitokea timu ya FC Port lakini alicheza michezo 17 ya Ligi Kuu Hispania msimu uliopita.
Katika misimu miwili aliyokaa Madrid, Danilo ameshinda ubingwa wa Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) mara mbili, Kombe la UEFA pamoja na Kombe la Dunia la klabu.
“Danilo ni mchezaji mzuri mwenye kipaji,” alisema Mkurugenzi wa ufundi wa Manchester City, Txiki Begiristain na kuongeza kuwa mchezaji huyo ana uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali ndani ya uwanja na kumfanya Guardiola kupata wigo mpana wa kuchagua.