27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Daniel Sillo: OSHA ni wadau wakubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Baran Sillo amesema kuwa taasisi ya OSHA ni mdau mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kwa sababu wanalinda nguvu kazi ya taifa kwa kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa salama dhidi ya vihararishi vya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Sillo ametoa kauli hiyo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikihitimisha ziara ya kutembelea viwanda mkoani Arusha na Kilimanjaro kwa lengo la kujionea utekelezaji wa sheria na miongozo mbalimbali ya usalama na afya mahali pa kazi katika viwanda hivyo wakiambatana na Naibu wa Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, Katibu Mkuu na watumishi wa Ofisi hiyo pamoja na Wakaguzi wa OSHA.

“OSHA ni wadau wakubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi hii kwa sababu wanalinda nguvu kazi ya taifa ambayo ndio inazalisha hivyo wawekezaji hawa wanapokuwa na nguvu kazi inayozalisha faida inakuja kwa serikali, muwekezaji na kwa wananchi pia kwahiyo niwapongeze sana OSHA kwa kazi hii kubwa mnayoifanya na sisi kamati ya bajeti ambayo jukumu letu kubwa ni kuishauri Serikali nasi tutaishauri serikali ili taasisi hii ya OSHA iendelee kuyafikia maeneo ya kazi mengi zaidi nchini ili nguvu kazi hii iendelee kuwa salama na yenye afya na iendelee kuzalisha na kukuza uchumi wa taifa letu,” alisema Sillo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Baran Sillo (katikati) na Naibu Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi (kulia) pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wakipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilimanjaro Plantation Limited, Calthon Rabenold kuhusu hatua za uzalishaji wa bidhaa ya kahawa katika kiwanda hicho na namna ambavyo wanazingatia miongozo ya usalama na afya katika hatua zote za uzalishaji.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Patrobas Katambi ametoa rai kwa wamiliki wa maeneo ya kazi nchini kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa taasisi ya OSHA kwa sababu taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kulinda usalama na afya za wafanyakazi pamoja na maeneo yao ya kazi.

“Nguvu kazi ya taifa letu tusipo ilinda athari zake hata uchumi wetu utashuka kwasababu tutakosa wataalam na nguvu kazi itakuwa tegemezi kwa taifa na ndio maana taasisi ya OSHA inafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha maeneo ya kazi yote yanakuwa salama dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa, nitoe wito kwa wamiliki wa maeneo yote ya kazi, kuwachukulia OSHA kama marafiki pindi wanapofika katika maeneo ya kazi kwaajili ya shughuli zao za ukaguzi,” alisema Katambi.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakijionea hatua za kuchakata mbegu za matunda na mbogamboga na namna ambavyo masuala ya usalama na afya yanazingatiwa katika hatua zote za uzalishaji katika cha Rajik Zwaan Arusha.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema kuwa taasisi ya OSHA imekuwa ikipokea shuhuda mbalimbali kutoka kwa wamiliki wa maeneo ya kazi wakikiri kuwa kaguzi za usalama na afya pamoja na ushauri wa kitaalamu unaotolewa na OSHA vimesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ushindani wa bidhaa wanazozalisha katika masoko ya kimataifa.

“Wawekezaji wamekuwa wakikiri kwamba ukaguzi wa usalama na afya tunaoufanya pamoja na ushauri wa kitalaam tunaowapatia wawekezaji hawa vimewaongezea tija hususan katika kushindanisha bidhaa zao katika masoko ya kimataifa kwasababu ili uweze kushindana na masoko ya nje ni lazima ukidhi matakwa ya sheria za ndani ikiwemo Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003,” alisema Khadija Mwenda.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilimanjaro Plantation Limited, Calton Rabenold ambayo ni miongoni wa eneo ya kazi lililotembelewa na Kamati hiyo ameishukuru serikali kupitia taasisi ya OSHA kwa kuendelea kuboresha mifumo ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.

Katibu Mkuu – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati wa ziara ya kamati hiyo katika kiwanda cha kuzalisha mbegu za matunda na mbogamboga cha Rijk Zwaan Mkoani Arusha.

“OSHA imetusaidia sana kuboresha mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi katika kampuni yetu kupiti kaguzi, mafunzo pamoja na ushauri wanaotoa baada ya kubaini mapungufu na changamoto mbalimbali za kiusalama kupitia kaguzi wanazozifanya na sisi tumekuwa tukifanya maboresho kila tunaposhauriwa,” alisema Rabenold.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru sana Kamati hiyo ya Bajeti kwa kufanya ziara ya kutembelea viwanda hivyo pamoja na kushiriki semina elekezi ya mafunzo ya usalama na afya iliyofanyika tarehe 10/09/2023 mkoani Arusha huku akiiomba kamati hiyo kuitikia wito pindi ofisi yake itakapo wahitaji tena. 

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akieleza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti namna ambavyo OSHA imekuwa ikipokea ushuhuda kwa wamiliki wa maeneo mbalimbali ya kazi nchini juu ya namna ambavyo kaguzi za usalama na afya pamoja na ushauri wa kitaalamu unaotolewa na OSHA umesaidia katika kuwaongezea ushindani wa bidhaa zao katika masoko ya kimataifa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imetembelea Kwanda cha kuzalisha mbegu na mbogamboga cha Rajik Zwaan kilichopo mkoani Arusha pamoja na kiwanda na mashamba ya Kilimanjaro Plantation Limited kilichopo mkoani Kilimanjaro.

Mkamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Omary Kigua (aliyevaa kofia) pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo wakifuatilia maelezo kutoka kwa muwakilishi wa kiwanda cha kuzalisha mbegu za matunda na mbogamboga cha Rijk Zwaan kuhusu taratibu na miongozo ya usalama na afya inavyotekelezwa na kiwanda hicho katika hatua zote za uzalishaji.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles