DANGOTE KUANZA KUZALISHA SARUJI KWA KUTUMIA GESI

0
686

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM                  |                    


KIWANDA cha saruji  cha Dangote Tanzania Ltd kimekubaliana na Serikali kuanza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia baada ya kusaini mkataba wa miaka 20.

Akizungumza   Dar es Salaam jana wakati wa   makubaliano hayo, Mwakilishi wa Kiwanda hicho, Jagat Singh Kathel, alisema makubaliano hayo yatasaidia kuongeza uzalishaji kutoka tani 2500   kwa siku hivi sasa na kufikia tani 6000 kwa siku.

Alisema pia matumizi ya gesi hiyo asilia katika kiwanda hicho yatasaidia kuondoa changamoto ya matumizi makubwa ya   dizeli.

Kathel alisema hivi sasa hutumia  lita 160,000 kwa siku hali iliyokuwa ikisababisha hasara kwenye uendeshaji wa kiwanda hicho.

“Mkataba huu umefikiwa  wakati mwafaka kwetu kwa sababu  tulikuwa tunausubiri kwa hamu. Kwa kuwa utaongeza kasi ya uzalishaji wenye gharama nafuu,” alisema Kathel.

Alisema kwa sasa Dangote kitaweza kuzalisha bidhaa zenye ubora kwa wingi na kwa wakati.

Akizungumza kuhusu kukabiliana na mfumko wa bei ya saruji  nchini, alisema kuanzia wiki hii  uzalishaji umeongezeka kutoka tani 2000 hadi tani  3300 kwa siku.

“Kwa sasa angalau nasi tunatarajia kuzalisha bidhaa bora sokoni na kupata faida tofauti na miaka iliyopita,” alisema Kathel.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),  Kapulya Musomba, alisema kuunganishwa kwa Kiwanda cha Dangote kunafanya idadi ya viwanda vinavyotumika gesi asilia nchini kufikia 42.

Alisema kiwanda cha kwanza kuunganishwa katika mfumo huo kilikuwa cha vigae cha Good Will.

“Kwa sasa tuna viwanda 42 ambavyo vimeunganishwa katika mfumo wa gesi asilia na katika mwaka huu wa fedha matarajio yetu tutaunganisha vingine saba,” alisema Musomba.

Alisema Kiwanda cha Dangote kinaendelea kukamilisha ujenzi wa miundombinu na ndani ya mwezi mmoja na nusu kitakuwa kimeanza kutumia gesi hiyo.

Alisema kwa sasa viwanda hivyo 41 vinatumia mita za ujazo   milioni  15 hivyo kuingia mkataba wa kiwanda hicho cha Dangote itafikia mita za ujazo milioni 23.

Alisema matarajio ya TPDC ni kufikia matumizi ya ujazo wa milioni 40 hadi 50 ya gesi hiyo.

Hivi sasa nchini bei ya mfuko mmoja wa saruji imepanda kutoka Sh 13,000 hadi kufikia 18,000 na  Sh 20,000 kwenye baadhi ya maeneo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here