21.1 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Dalili ya wanandoa kufikia ukingoni

CHRISTIAN BWAYA

MARA nyingi watu wanapooana, pamoja na kupendana, bado kunakuwa na hofu fulani ya kutofautiana. Unaweza kwa mfano, usipende tabia fulani ya mwenzako lakini ukashindwa kumwambia kwa sababu unaogopa kumuumiza. Lakini kadiri mnavyoishi pamoja, ndivyo uhusiano wenu unavyokua.


Kukua kwa uhusiano kunatokana na kuaminiana kwa kiwango cha kutokuwa na hofu ya kutofautiana. Ingawa watu wengi huogopa kutofautiana, lakini ukweli ni kwamba tofauti zinapoambatana na upendo, mara nyingi husababisha watu wawili kufahamiana kwa karibu zaidi, kukubali tofauti zao na hivyo kupendana kwa dhati zaidi.

Hata hivyo, zipo tofauti ambazo ni kiashiria cha uhusiano mbaya, tofauti zinazoweza kusababisha kudhalilishana, kukosekana kwa heshima ya ndoa, kubishana kunakozidi mpaka na hata kukosekana kwa uaminifu kati ya watu wawili walioapa kupendana. Hapa ninakuletea baadhi ya dalili hizo.

Tabia hatarishi
Moja ya tabia inayoweza kuwa hatari zaidi ni mwenzako (au wewe mwenyewe) kutokuona jema kwa mwenzako, tabia inayoambatana na ukosoaji uliopindukia. Tunafahamu ni muhimu kukosolewa, lakini inapotokea kwamba mwenzako au wewe mwenyewe unaonekana kuwa na shauku ya kuanika upungufu alionao mwenzako, kwa namna inayolenga kumdhalilisha na kumfanya ajione hana thamani, basi hapo kuna tatizo kubwa mbele yenu.


Huwezi kumkosoa mtu unayempenda, hata kama kuna jambo haliendi vizuri, bado utakuwa na lugha nzuri ya kuwasiliana naye bila kuumiza hisia zake. Unapoona mwenzako au wewe mwenyewe ‘unayashikia bango’ makosa ya mwenzako wakati ya kwako mwenyewe hutaki yajadiliwe, hapo kuna tatizo kubwa.


Kukosoa, mara nyingi kunafuatiwa na tabia kama kufoka kunakoambatana na anayefokewa kujihami kwa maneno makali. Hali inapofikia hapa, kila mmoja huamua kujificha kwenye handaki lake asitake mazungumzo na mwenzake kama namna ya kushughulikia matatizo.

Lakini hali hii si dalili nzuri kwa sababu hamuwezi tena kukaa chini na kujadili jambo na mkafikia mwafaka; kila mtu huanza kufikiri kivyake vyake na hamshikirikishani tena mambo yenu.


Wakati mwingine mnaanza kujiona kama watu wawili wenye ndoto na mipango tofauti. Kile kinachokuvutia wewe na unachokiona cha thamani kinageuka kuwa kero kwa mwingine. Shauri ya kuanza kujiona mpweke uliyeolewa/uliyeoa, taratibu unaanza kutamani kuwa karibu na watu wengine.

Unaanza kufungua moyo wako kwa mtu mwingine, unamsema mpenzi wako kwa watu wengine na unapofanya hivyo unajisikia faraja fulani. Unaanza kutumia kazi au shughuli nyingine kama kichaka cha kutokuwa na mwenzako huo ndio mwanzo wa kukosa uaminifu.

Mtu wa hatari zaidi
Ukiacha hali ya kawaida ya kutokuelewana, wakati mwingine tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi. Mwenzako au wewe mwenyewe unapokuwa na ugonjwa wa nafsi uitwao kisaikolojia, ‘narcissism’ hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Mtu mwenye ugonjwa huu huwa ni mbinafsi kupindukia anayejifikiria yeye mwenyewe zaidi kuliko mtu mwingine.

Ingawa unapokutana naye kwa mara ya kwanza huwa ni mcheshi, mchangamfu, mwenye kila aina ya vionjo vya mtu mwenye mapenzi ya kweli lakini baada ya muda hugeuka kuwa kitu kingine.


Hukosa hisia, hajali tena unajisikiaje, hajali unamwonaje, kwa sababu kinachokuwa muhimu kwake ni kile anachokitaka yeye. Huyu ni mtu anayeweza kuchezea hisia zako ukiwa mpenzi wake, kwa kukufanya uamini ni mtu wa thamani pale anapokuhitaji lakini anapokuwa hana haja na wewe, anaweza kukudhalilisha ukajiona huna maana yoyote.

Ingawa mara nyingi tabia zake zinakuwa ndio chanzo cha tatizo, mfano kukunyanyasa, kutaka kukudhibiti kupita kiasi, wivu uliopindukia, mtu wa namna hii huwa hana uwezo wa kuona uhusiano wa tabia zake na kile unachomfanyia.


Aidha, huyu anaweza kuwa aina ya mtu anayejishtukia, asiyejiamini na hivyo huwa haamini kama mwenzake anaweza kuwa na nia njema na yeye. Kwa sababu hiyo huwa ni mtu mlalamishi, mwenye wasiwasi mara zote akihisi kuna vitu vinafichwa, mnapozungumza hawezi kukiri makosa yake, mnapozungumza kile kinachomtia hatiani, mara zote atafanya jitihada za kukifukia kwa kuibua kingine kitakachoficha udhaifu wako.

Ikiwa anafikia hatua ya kuvuka mipaka anaweza kuwa mgomvi, mkali kupindukia, roho mbaya kwa watu asiowapenda na hata kuwa mkatili.

Ufanyeje?
Wakati mwingine tunakata tamaa kwenye uhusiano kwa sababu hatujui chanzo cha matatizo. Kama tulivyoona, matatizo mengine ni sehemu ya safari ya kufahamiana na kujenga mtazamo wa pamoja kama wanandoa.

Lakini hata inapokuwa ni shauri ya matatizo makubwa zaidi ya nafsi anayokuwa nayo mmoja wenu, bado mnaweza kuchukua hatua za kutengeneza mambo. Kwa mfano, ikiwa mmeanza kuhisi kukosa shauku ya kuwa pamoja kama ilivyokuwa zamani, anzeni kufanya jitihada za kuthaminiana upya.

ITAENDELEA

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,592FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles