27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

DALADALA DAR MAWASILIANO WAGOMA KWA SAA 5

CHRISTINA GAULUHANGA NA KASANDRA HASSAN, (TUDARCO)

– DAR ES SALAAM

MADEREVA wa daladala zinazoishia katika kituo cha mabasi cha simu 2000 maarufu kama Mawasiliano jijini Dar es Salaam jana waligoma kwa saa tano wakishinikiza kuondolewa kwa ushuru mpya wa Sh1,000 kwa siku badala ya Sh 500.

Mbali na hilo madereva hao wanashangazwa na hatua hiyo huku barabara inayokwenda kituoni hapo ikiwa ni mbovu na hawaoni juhudi za kuitengeneza.

Mgomo huo ulisababisha usumbufu kwa abiria wengi kuchelewa sehemu mbalimbali za kazi na huduma nyingine.

Akizungumza katika mkutano ulioitishwa jana na  uongozi wa Wilaya ya Ubungo, Mwenyekiti  wa Chama cha Madereva na Makondakta wa Mabasi ya Tegeta na Bunju (Uwastebu), Stanley Kilave, alisema wamelazimika kugoma kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kupanda kwa ushuru huo.

Alisema meneja wa kituo hicho aliwaandikia barua wiki iliyopita akionesha azma ya kupandisha ushuru lakini walimkatalia kwa sababu bado kuna changamoto nyingi ndani ya kituo hicho ikiwamo ubovu wa barabara zinazoingia kituoni hapo.

“Mheshimiwa pale getini kuna majipu, waliopo pale asubuhi tukilipa ushuru na kuacha chenji zetu tukirudi baadaye kudai tunatishwa na wengine hadi kupigwa…ukiingia chooni hata kunawa uso unatozwa faini ya Sh 50,000 hata risiti hatupewi, hii inatuumiza sana,”alisema Kilave.

Akijitetea kuhusu madai hayo, Meneja wa Kituo cha Simu 2000, Grayson Lubaga alisema, hawajawahi kutoza faini ya kunawa uso Sh 50,000 na kuwataka wenye ushahidi wapeleke risiti.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori baadaye aliagiza kuondolewa mara moja kwa wafanyakazi wa getini ambao wamelalamikiwa. Alisema maelezo aliyoyapata yanadhihirisha jinsi watumishi hao ambao wapo chini ya manispaa wanavyojipatia fedha kinyume na sheria.

Alisema kuanzia sasa gharama zitakazoendelea kutozwa katika kituo hicho ni Sh 500 hadi hapo manispaa hiyo itakapojipanga na kurekebisha baadhi ya kero.

“Naomba watumishi hawa waondolewe mara moja na kuletwa wengine ambao watapewa utaratibu kwani hata vitabu vya dini vinasema ukituhumiwa ni dhambi, hivyo kuandaliwe mfumo mwingine ili kuondoa malalamiko pale getini,”alisema  Makori.

Naye Mkurugenzi wa Wilaya ya Ubungo, John Kayombo alisema, wameshindwa kurekebisha mfumo wa taa katika kituo hicho kwa sababu ya kufuata sheria.

Akizungumzia malalamiko hayo, Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob alisema, Baraza la Madiwani halina taarifa za kupanda kwa ushuru katika kituo hicho.

Alisema amesikitishwa na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Ubungo kuwaingiza kwenye mgogoro na watumiaji wa huduma hiyo bila sababu za msingi hivyo ataitisha vikao kuwachukulia hatua kali za kinidhamu  kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu ubovu wa barabara, Jacob alisema: ilikwishatengewa fedha kutoka Benki ya Dunia (WB) kiasi cha Sh bilioni 1.7 tangu mwaka 2015 lakini zimezuiwa kwa sababu za kisiasa. “Kwa sababu Wizara ya Fedha wamezuia fedha za fidia”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles