22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Daktari: Mwanga mkali husababisha uoni hafifu

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

DAKTARI bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam, Cprian Ntomoka amesema matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali kama simu na kompyuta yanaweza kusababisha tatizo la uoni hafifu au hata upofu wa muda.

Dk. Ntomoka ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Macho katika  hospitali hiyo, aliiambia MTANZANIA, Dar es Salaam jana kuwa ni kweli kuna hatari kubwa ya kutumia vitu hivyo kwa muda mrefu huku akisema kuwa kuna haja ya watu kubadili mfumo wa matumizi ya muda mrefu wa vifaa hivyo.

“Kuna haja sasa ya watu kuangalia tatizo hili kwani hili linaweza kuwa janga kwa watu wengi, hivyo kila mtu ajifunze matumizi sahihi ya vitu hivi, waelewe sio sahihi kutumia simu kwa muda mrefu hasa wakati wa giza,” alisema Dk. Ntomoka.

Alisema matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali vinaumiza macho, kwa sababu uteute unaolainisha macho unakauka, na endapo macho yakiwa makavu yanaweza kuwasha, kutoa machozi, kuumia na wakati mwingine kuwa mekundu.

“Hii tunaita ‘Computer Vision Syndroms’, ni mkusanyiko wa usumbufu ambao mtu anapata kutokana na matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali kama hivyo.

“Ni changamoto kubwa, tunapokea wagonjwa wengi wanaofanya kazi za kutumia kompyuta, hata wa simu huwa wanakuja wakilalamika kuumwa macho, ni muhimu watu wakajua kuwa matumizi ya muda mrefu ya kompyuta, simu na vifaa vingine vyenye nwanga mkali ni hatari kwa macho,” alibainisha Dk. Ntomoka.

Katika kliniki yake, Dk. Ntomoka alisema anawaona wagonjwa watano hadi 10 kwa siku moja, ambao wamepata madhara ya macho kutokana na matumizi ya vitu vyenye mwanga mkali.

“Madhara yanaweza yasionekane kwa sasa ila baada ya miaka kadhaa ukaanza kuumwa macho, katika kliniki yangu napata watu wengi wenye tatizo hilo. Kila siku naona wagonjwa 40 ambapo kati yao watano hadi 10 wanakabiliwa na matatizo hayo,” alifafanua.

Aliwataka watu kufuata ushauri wa matumizi sahihi wa vifaa vyenye mwanga kama kupunguza mwanga na kupumzisha macho kwa dakika 20 kila baada ya saa moja.

“Watu wapate ufahamu juu ya matumizi sahihi ya kompyuta ili wasiweze kupata matatizo ya macho, wafuate ushauri wa kutumia simu janja, kompyuta, TV, Tablet na zingine. Kama watu wanahitaji ushauri waende kwa madaktari wa macho ili washauriwe.

“Pia ni muhimu kupumzisha macho kwa kila baada ya dakika 20 hadi 30, kuweka ‘screen’ za kuzuia mwanga mkali au kuvaa miwani inayochuja kiasi cha mwanga,” alisema Dk. Ntomoka.

Ripoti iliyosomwa na Shirika la Utangazaji la Idhaa ya Kiswahili (DW) hivi karibuni,  inasema tafiti zinaonyesha kuangalia kwa muda mrefu kwenye kioo cha simu kunaweza kukusababishia upofu wa muda na hata wa kudumu.

Ripoti hiyo ilisema mtu mmoja  kutoka kaskazini magharibi mwa China, alijikuta akiwa katika hali ya kushindwa kuona baada ya kucheza michezo ya kwenye simu maarufu kama ‘game’ kwa saa kadhaa akiwa gizani

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,415FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles