26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

DAKTARI: MAGONJWA SUGU YA FIGO YANA UHUSIANO NA MAGONJWA YA AKILI

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WATU wanaougua ugonjwa sugu wa figo wana uwezekano mkubwa wa kushambuliwa na magonjwa ya akili kama sonona, wasiwasi na kuchanganyikiwa.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Omar Ubuguyu, katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam, ambapo alifafanua kwamba watu wanaosumbuliwa na ugonjwa sugu wa figo ni rahisi kuandamwa na maradhi ya akili kuliko wale wanaougua kisukari, shinikizo la damu na magonjwa mengine ambayo ni sugu.

Katika maelezo yake alisema asilimia 29 ya wagonjwa wa figo barani Afrika hupata magonjwa ya akili ikiwamo sonona, wasiwasi na kuchanganyikiwa. Kiwango hicho ni sawa na theluthi ya watu wanaougua magonjwa ya figo barani hapa.

Dk. Ubuguyu alisema mbali na wagonjwa wa figo, takwimu za kidunia zinaonyesha kuwa asilimia 14 ya watu wote wanaougua magonjwa sugu ya aina tofauti nao hupatwa na ugonjwa wa akili.

Alisema hali hiyo ni ya kawaida kwa sababu mtu yeyote anapopewa taarifa ya kukutwa na ugonjwa sugu huishia kupata wasiwasi, hofu na huzuni.

“Sasa unaweza kujiuliza kwanini idadi ya wagonjwa wa figo wanaougua magonjwa ya akili ni kubwa kuliko ya wale wanaougua magonjwa mengine, hii ni kwa sababu ile hali ya figo zenyewe zinaposhindwa kufanya kazi yake sawa sawa huacha taka mwili (urea/ uraemia).

“Na taka mwili hiyo inapokuwa mwilini kwa kiwango kikubwa ikifikia hatua ya kutapakaa hadi kwenye ubongo, mtu huchanganyikiwa,” alisema.

Alisema magonjwa ya figo yamegawanyika katika sehemu mbili, ya mshtuko (acute) na sugu (cronic), mara nyingi wale wanaogua magonjwa sugu ya figo ndio ambao huwa katika hatari ya kupata magonjwa ya akili.

Aliongeza kwamba mtu anavyopokea taarifa ya kwamba ana tatizo kubwa hupata mshtuko na matokeo yake hujikuta anashambuliwa na ugonjwa wa hisia kitaalamu ‘emotional au mood problems’.

“Katika hali ya namna hiyo ni rahisi mtu kupata sonona (depression), kwa hiyo kuna vitu viwili ambavyo vinaweza kumsababishia mtu mwenye tatizo la figo kupata ugonjwa wa akili, namna anavyoipokea taarifa ya kuugua kwake na kiwango cha taka mwili kilichopo mwilini mwake,” anasema.

Anasema msongo wa mawazo nao huweza kusababisha hali hiyo hasa kwa wale wagonjwa ambao huhitaji msaada wa kupata figo ya kupandikiza.

“Huwa wanajiuliza itakuwaje, je, atapata mtu wa kumsaidia au la, ile hali tu ya kusubiri kupata mchangiaji inaweza kumwathiri,” alisema.

Matibabu

Dk. Ubuguyu alisema kwamba, wanatumia njia mbili katika kufanikisha matibabu ya mgonjwa wa figo.

“Kwanza tunatibu ugonjwa halisi, kama hautibiki basi tunamshauri na kumwandaa kisaikolojia (mazungumzo ya kiwango cha juu) ili aweze kuelewa kila hatua ya matibabu atakayokuwa akipatiwa, ni vizuri kuwaeleza kila hatua inayofuata,” alisema na kuongeza:

“Lakini kama mtu amepata tatizo la akili yaani sonona au kuchanganyikiwa, tunamtibu kwanza kwa kumpatia dawa maalumu.

“Tunatumia pia tiba ya ‘relaxation’, tunafanya shughuli ambazo zinampa faraja na furaha, kwa mfano kama anapenda muziki, kukaa ufukweni, tunashauri wapelekwe huko ili ku-relax na wapo ambao huamua kumrudia Mungu wao yote hayo ni sehemu ya matibabu.

“Jambo la muhimu ni azingatie kufuata zile taratibu na masharti ya matibabu, ili zile taka mwili zisiendelee kubakia mwilini mwake ni lazima ahudhurie kliniki ya kuchuja damu (hemdialysis).

“Tiba zetu huwa hazina muda maalumu, sisi tunamtibu hadi atakapokaa sawa, kwa hiyo siwezi kueleza tunamtibu kwa muda gani, huwa inategemeana wengine ile hali ya kuzidiwa huondoka kati ya miezi mitatu hadi sita na ukakuta tena ile hali imejirudia hivyo tunaendelea kumtibu,” alisema.

Changamoto

Katika hatua nyingine alisema matibabu ya mgonjwa wa figo aliyepata ugonjwa wa akili huwa yana changamoto nyingi.

“Wengi hushindwa kujilinda, kuna baadhi ya vitu hutakiwa kujiepusha navyo kwa mfano kunywa maji mengi na matumizi ya chumvi, lakini kwa sababu anachanganyikiwa au kukata tamaa ile nia ya kuendelea na matibabu inaweza kushuka akajikuta akitumia vitu hivyo na kuhatarisha afya yake,” anasema na kuongeza:

“Si dawa zote ambazo tunatumia kuwatibu wagonjwa wa akili huwafaa wagonjwa wa figo, hii ni changamoto, ndiyo maana hatushauri mtu kutumia dawa ya kutibu sonona kwa sababu kama atakuwa na ugonjwa wa figo zinaweza kumwathiri zaidi, lazima itolewe na daktari.”

Alisema wale ambao hujitolea kuchangia figo nao huwa wanazungumza nao ili wasije wakafikia hatua ya kupata sonona.

Hali ilivyo MNH

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa Muhimbili, Jacqueline Shoo, alisema katika kliniki yao wanaona wagonjwa wengi kila mwezi wakiwamo watoto.

“Tunapokea watoto kati ya 30 hadi 40 kila mwezi ambao wanaugua magonjwa ya mshtuko na asilimia kubwa wana sugu. Watu wazima tunaona wagonjwa kati ya 120 hadi 150 kila mwezi.

“Tangu mwaka 2006 hadi 2017, wagonjwa 220 tayari wamepandikizwa nchini India na wote wapo hai wanaendelea vizuri, wagonjwa 132 wanafanyiwa ‘dialysis’, asilimia 50 kati ya hawa wapo kwenye mchakato wa kupandikiza figo, wanatafuta watu watakaowasaidia kupata figo ya kupandikizwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles