MARGRETH MWANGAMBAKU (TUDARCO) Na TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM
DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo, ameshinda tuzo ya watafiti vijana wa Afrika kwa mwaka 2017 (Young African Researchers Awards 2017).
Daktari huyo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo JKCI ameshinda tuzo hiyo inayotolewa na Taasisi ya Sayansi na Utafiti ya Misri.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa JKCI, Anna Nkinda alisema Dk. Pallangyo alishinda tuzo hiyo baada ya kufanya utafiti wa sayansi katika masuala ya afya na dawa za binadamu.
Nkinda alisema mshindi huyo atapewa zawadi ya Dola za Marekani 15,000 (zaidi ya Sh milioni 30 ), ngao na cheti.
Alisema Dk. Pallangyo aliandika machapisho 16 katika majarida (Journal) saba ya Kimataifa ya Afya ya Marekani.
“Licha ya kukabidhiwa tuzo hiyo, mshindi huyo atapewa zawadi ya Dola za Marekani 15,000 (zaidi ya Sh milioni 30), ngao na cheti,” alisema Anna.
Alisema tuzo hiyo itakabidhiwa Agosti mwaka huu Jijini Cairo na Rais wa Misri, Abdi El- Fattah Al-Sis.
Dk. Pallangyo ni Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo hiyo tangu ianze kutolewa mwaka 2014. Mshindi wa mwaka jana alitoka Ghana.
Wakati huo huo, watoto 30 wenye vichwa vikubwa wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji Agosti 26, mwaka huu katika Taasisi ya MOI.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Jumaa Almas alisema jana kuwa upasuaji huo unafanyika kila mwezi kwa ufadhili wa Jumuiya ya Waislamu wa Madhehebu ya Shia.
Alisema gharama za upasuaji kwa watoto hao pamoja na vifaa vya kutolea maji kichwani vinavyojulikana kitaalamu kama ‘Shunt’ vinatolewa na Jumuiya hiyo.
“Tunashukuru wenzetu Washia wameendelea kutusaidia katika kupata fedha za vifaa tiba na posho kwa ajili ya upasuaji wa watoto,” alisema Almas.
nampongeza ndugu yetu dr pedro parallangyo kwa ushindi na kuipeperusha bendera juu nchi yetu TANZANIA.