32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Daktari feki akamatwa wodi ya wagonjwa mahututi

Daktari feki akihojiwa na Polisi baada ya kukamatwa
Daktari feki akihojiwa na Polisi baada ya kukamatwa.

Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

UKISTAAJABU ya Mussa utayaona ya Firauni. Ndivyo unaweza kusema baada ya Polisi Mkoa wa Morogoro kumtia mbaroni Benjamin Zakaria kwa tuhuma ya kuingia katika hospitali ya mkoa na kujifanya daktari ndani ya wodi ya wagonjwa mahututi.

Akiwa ndani ya hospitali hiyo, Zakaria anadaiwa alijifanya daktari mgeni na kuanza kukagua huduma zinazotolewa na hospitali hiyo.

Zakaria ambaye ni mkazi wa Tungi mjini hapa, aliingia katika hospitali hiyo na kuvaa vazi la kidaktari, kisha kutembelea wodi mbalimbali akiwahoji wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema kuwa daktari huyo feki alitiwa mbaroni baada kutiliwa shaka na muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, ambaye alitoa taarifa polisi.

“Alifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na kujifanya kama madaktari wengine waliokuwa wakiendelea kutoa huduma kwa wagonjwa. Alipofika wodi ya wagonjwa mahututi, alikutana na muuguzi wa zamu na kudai yeye ni daktari mgeni.

“Hata hivyo, muuguzi huyo alimtilia shaka na aliufahamisha uongozi wa hospitali juu ya uwepo wa daktari huyo feki, na kisha tukafahamishwa polisi na kufanikiwa kumkamata,” alisema Kamanda Matei.

Mmoja wa wauguzi katika wodi ya wagonjwa mahututi, Expiransa Mtama, alisema kuwa alibaini daktari huyo feki hana sifa za kitabibu baada ya kumuhoji maswali ya kina ya kitaalamu ambayo alishindwa kuyajibu.

Tukio hilo ni la pili kutokea hospitalini hapo baada ya Julai 12, 2014, kijana mwingine mkazi wa Liti, Manispaa ya Morogoro, Karume Kauzu, kukamatwa kwa tuhuma za kujifanya daktari.

Kijana huyo ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma,  alikamatwa na uongozi wa hospitali hiyo baada ya muuguzi mmoja aliyekuwa zamu, kumuhisi hakuwa daktari wa kweli, na kuamua kutoa taarifa kwa uongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles