23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Daktari bingwa aeleza madhara ya kukoroma

AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

DAKTARI Bingwa wa Upasuaji Magonjwa ya Koo, Masikio na Pua wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili –Mloganzila, Godlove Mfuko, amesema kukoroma ni tatizo ambalo linaweza kusababisha magonjwa ya moyo, huku athari nyingi zaidi zikiwa kwa watoto.

Alisema tatizo hilo la kukoroma linatibika na kwamba utafiti wa kidunia unaonyesha asilimia 4 ya wanaume wana tatizo hilo huku wanawake wakiwa ni asilimia 2.

Pamoja na ukubwa wa tatizo hilo, Dk. Mfuko alisema hata katika Hospitali ya Mloganzila ni asilimia 6 ya watu hufika kupata matibabu kwa mwaka.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu, alisema madhara mengine ya tatizo hilo hasa kwa watoto ni kufanya vibaya darasani, kukojoa kitandani na utundu uliopitiliza.

“Kukoroma ni dalili ya ugonjwa, hii inatokana na tatizo la mfumo wa upumuaji, mtu anapokuwa na tatizo la kukoroma kwa muda mrefu husababisha ubongo kukosa oksijeni, hali hiyo huathiri ubongo na madhara yanaenda hadi kwenye moyo.

“Tatizo hili husababisha moyo kufeli kufanya kazi zake kwani na wenyewe unahusika na mfumo huo wa oksijeni,” alisema Dk. Mfuko.

 Alisema kukoroma pia kunafanya watoto washindwe kuwa vizuri darasani kwa sababu wanakuwa hawajapata usingizi vizuri.

Dk. Mfuko alisema kutokana na tatizo hilo la kukoroma, katika Hospitali ya Mloganzila wanafanya upasuaji kwa watoto 30 hadi 40 kwa mwezi na wengine wanatibiwa kwa dawa.

 “Licha ya tatizo hilo kuonekana katika jamii, bado watu wengi hawaji hospitali kutokana na kuchukulia tatizo hilo kuwa la kawaida au kwa wengine kutokuwa na elimu kuhusu tatizo hilo,” alisema.

Dk. Mfuko alisema sababu ya tatizo la kukoroma ni maumbile ya shingo, unene uliopitiliza, magonjwa ya mfumo wa hewa hasa kwenye mapafu.

“Sababu zingine ni shinikizo la damu, asilimia 50 ya watu hawa hukoroma, kuna matumizi ya vilevi kama pombe, sigara na dawa za kulevya. Pia utafiti unaonyesha watu wenye shingo nene wako hatarini kukoroma zaidi,” alieleza.

Kwa mujibu wa Dk. Mfuko, dalili za tatizo hilo ni kulala hovyo mchana hali ambayo wakati mwingine husababisha ajali za barabarani kwa sababu ya madereva kusinzia na kichwa kuuma, hasa nyakati za asubuhi.

“Mtu kama huyu anaweza kupata tatizo la kisaikolojia na kuathiri kumbukumbu, pia dalili nyingine za tatizo hili ni kushtuka mara kwa mara wakati umelala usiku, kupaliwa wakati wa kulala, kukojoa mara kwa mara na tatizo la mafindofindo.

“Na utafiti unaonyesha asilimia 80 ya watoto wanaotibiwa mafindofindo wanaacha kukojoa kitandani,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,712FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles