28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

DAKTARI ATAJA SABABU MTOTO KUTOKWA UTUMBO NJE

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaituni Bokhary

 

 

NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM

HALI ya mtoto kuharisha muda mrefu imetajwa kuwa hatari kwani inaweza kumsababishia kupata tatizo la kutoka utumbo mkubwa katika njia ya haja kubwa.

Akizungumza na na MTANZANIA katika mahojiano maalumu ofisini kwake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaituni Bokhary alisema tatizo hilo kitaalamu linaitwa Retal Prolapse.

Alisema kila mwezi wamekuwa wakipokea watoto kati ya wanne hadi watano wanaokabiliwa na tatizo hilo na kuwapatia matibabu.

“Ni hali ambayo sehemu ya utumbo mkubwa huwa unatoka nje katika njia ya haja kubwa, bado hakuna  chanzo maalumu tunachoweza kusema kwamba ndicho husababisha hali hiyo kutokea.

“Lakini kuna visababishi kadhaa ambavyo huchangia mtoto kupatwa na hali hiyo ikiwamo kuharisha muda mrefu, maambukizi katika utumbo mkubwa au mtoto kutokwa na vinyama katika sehemu ya haja kubwa,” alisema.

Alisema hali hiyo huweza pia kujitokeza iwapo mtoto atapata maambukizi ya virusi (Rota virus) ambacho huenda kula baadhi ya seli za utumbo mkubwa.

“Virusi hivi hushambulia seli za utumbo mkubwa, lakini hapa Muhimbili tunaona watoto wengi tunaowapokea chanzo ni kuharisha,” alisema.

Alisema dalili za kuwapo kwa tatizo hilo zipo katika hatua nne na kwamba ni rahisi kulitibu katika hatua ya kwanza na ya pili.

“Katika hatua ya kwanza na pili ikiwa mzazi atamuwahisha mtoto hospitalini linatibika kwa dawa na uangalizi maalumu, lakini katika hatua ya tatu na nne ni lazima mtoto afanyiwe upasuaji,” alisema.

Dk. Bokhary aliwashauri wazazi kuhakikisha wanawawahisha mapema watoto wanaopata hali ya kuharisha ili wapatiwe matibabu sahihi.

“Ukikaa naye nyumbani na kuishia kumpa dawa mwenyewe ni hatari, lakini pia ni vema mazingira yakawekwa safi na watoto walindwe ili wasiende kucheza kwenye maji machafu.

“Ni vigumu mtoto kujilinda, unakuta amechezea maji machafu halafu anaweka vidole mdomoni baadae anapata ‘infection’ anaanza kuharisha lakini pia ni vizuri maji ya kunywa nayo yakachemshwa,” alishauri.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles