27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Daktari ashauri watoto wanaokoroma kupelekwa hospitali

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

DAKTARI bingwa wa magonjwa ya pua, koo na mdomo  kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, Perfect Godfrey, ameishauri jamii kuwapeleka watoto wanaokoroma hospitali kupata matibabu kwani kukoroma ni ugonjwa kama magonjwa mengine.

Dk. Godfrey alisema zipo jamii zinazoamini kuwa kukoroma ni kitendo cha asili au kurithi kitu ambacho sio kweli.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu jana Dar es Saalaam, Dk. Godfrey alisema ni bora mtoto akapelekwa hospitali  ili kupata vipimo na kugundulika ana tatizo gani.

 “Kuna jamii zinadai kuwa  kukoroma ni kitendo  cha  asili na  kwa  mtoto anayekoroma wengine huamini kuwa  ni tatizo la kurithi,  wengine wanakwambia babu au bibi au baba yake anakoroma  kwahiyo wanasema mtoto amechukua hilo kutoka kwa babu au baba,  kwahiyo wanakuwa hawawaleti hospitali.

“Niwaambie tu kuwa kuja hospitali ni muhimu zaidi  ili tuweze kujua tatizo ni nini kwa sababu sio wote wanaokoroma ni tatizo la nyama ya pua, yapo matatizo mengine,” alishauri Dk. Godfrey.

Alisema kuwa nyama za pua huwa watoto wanazaliwa nazo na kumsaidia kukabiliana na magonjwa ya koo na pua,  lakini kuna umri ukifika zinatakiwa kusinyaa.

“Wakati watoto wakiwa wachanga pale anapotoka kwa mama na kuja duniani huwa anatakiwa atafute kinga yake, nyama hizo zinakuwepo kwa ajili ya kumsaidia katika kinga yake kutokana na magonjwa ya pua na koo.

“Na kwa kadiri anavyokua kama mwaka mmoja hivi, nyama hizo zinaanza kunyauka,  kwahiyo anapoendelea kukua  tunategemea kazi yake inapungua kidogo kidogo,   baada muda zinasinyaa na zinakuwa hazimletei matatizo na kama hazisinyai ndo tunasema mtoto atolewe,” alisema Dk. Godfrey.

Alieleza kuwa kama nyama hizo hazisinyai mtoto anaanza kupata matatizo ikiwemo kukoroma.

“Matatizo  makubwa ni kukoroma  na wakati mwingine anashindwa kupumulia pua anapumulia mdomo na ndio utakuta anaacha mdomo wazi zaidi, sana pale anapokuwa amelala.

“Katika  hali ya kawaida mtoto hatakiwi  kukoroma  na ndio maana anapokoroma  tunatafuta sababu,  na sio kukoroma tu  hata mzio wanaweza kupata, lakini kiujumla pamoja na kupata hiyo shida sio wote wanahitaji kufanyiwa operesheni,” alisema Dk. Godfrey.

Alisema wapo wanaotibiwa kwa dawa na kupona  huku ambao hawaponi kwa dawa wanafanyiwa upasuaji.  

 “Wito kwa jamii ni kwamba mtoto akiwa na tatizo  aletwe hospitali aweze kuchunguzwa ili aweze kutibiwa kama ni kwa dawa au matibabu mengine.

“Kwa sababu zile nyama huwa zina madhara yake, endapo kama mtoto atakuwa anabanwa sana anaweza  kupata matatizo mengine  ya upumuaji,” alisema Dk. Godfrey.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles