Daktari aliyeisaidia CIA kumpata Osama azidi kusota

0
658

ISLAMABAD, PAKISTANI

DAKTARI wa Pakistani, Shakil Afridi aliyeisaidia Marekani kumpata kiongozi wa kundi la al-Qaeda Osama Bin laden bado anazidi kusota jela na sasa amekata rufaa dhidi ya hukumu yake ya miaka 33.

Dk. Afridi ambaye anatajwa kufanya kazi na CIA, inaelezwa kuwa hatua yake ya kuisaidia Marekani kumnasa Osama hakukuifurahisha Pakistan  ambayo iliamua kumshtaki kwa makosa mengine.

Alishtakiwa Mei 2012 kwa kutekeleza uhaini baada ya kupatikana na makosa ya kufadhili kundi la wapiganaji lililopigwa marufuku la Lashkar-e-Islam.

Kesi ya Shakil Afridi itasikilizwa kwa mara ya kwanza katika mahakama ya wazi baada ya Jaji kuahirisha kesi hiyo

hadi  Oktoba 22 kutokana na  ombi la waendesha mashtaka.

Kinachodaiwa kufanywa na Dk. Afridi kilikuwa aibu kubwa kwa Pakistani.

Yeye mwenyewe anadai kwamba alinyimwa haki yake wakati wa kusilikilizwa kwa kesi hiyo ambapo alihukumiwa mika 33 jela.

Hakushtakiwa rasmi kwa jukumu lake katika operesheni hiyo ya mwaka 2011 ya kumsaka na kumuua mtu aliyekuwa akitafutwa sana duniani.

Kufungwa kwake jela kulisababisha hisia kali hatua iliosababisha Marekani kufutilia mbali msaada wake kwa Pakistan wa takriban dola milioni 33 na dola milioni moja kila mwaka.

Rais wa Marekani, Donald Trump aliahidi katika uchaguzi wa 2016 kwamba atamwachilia huru Dk. Afridi baada ya dakika mbili iwapo atachaguliwa – lakini hilo halijafanyika.

Wakati daktari huyo akionekana kuwa shujaa Marekani, nchini Pakistani anaonekana kama msaliti ambaye aliiletea aibu taifa hilo.

ALIVYOSAIDIA KUPATIKANA OSAMA

Makomando wa jeshi la wanamaji la Marekani walisafiri kwa helikopta kutoka Afghanistani hadi Pakistani na kumuua Osama anayedaiwa kupanga njama za mashambulizi ya Septemba 11 na kuondoka na mwili wake bila kuzuiwa.

Osama anadaiwa kujificha  baada ya shambulio la Marekani la Septemba 11.

Hatua ya Osama kukamatwa ndani ya ardhi ya Pakistani ilizua maswali mengi ya iwapo jeshi la Pakistani lilikuwa linajua iwapo alikuwa nchini humo.

Pakistani imesalia kuwa mshirika asiyeaminika katika vita vya Marekani dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu.

DK. SHAKIL

Dk. Afridi alikuwa daktari mkuu katika hospitali ya wilaya ya Khyber na akiwa mkuu wa huduma za afya alikuwa amesimamia baadhi ya mipango kadhaa ya chanjo zinazofadhiliwa na Marekani.

Kama mfanyakazi wa serikali, alianzisha mpango wa chanjo ya Homa ya Ini (Hepatitis B), ikiwemo katika mji wa Abbottabad ili kubaini iwapo waliokuwa wakiishi katika eneo hilo ni ndugu za Osama.

Inadhaniwa kwamba mfanyakazi mmoja wa Dk. Afridi alitembelea nyumba ya akina Osama na kuchukua vipimo vya damu – lakini haijulikani iwapo hilo lilisaidia Marekani kumpata Osama.

Dk. Afridi alikamatwa Mei 23, 2011 siku chache tu baada ya Osama kuuawa. Alidaiwa kuwa na miaka 40 wakati huo.

Ni mambo machache yanayojulikana kuhusu maisha yake, mbali na kwamba alitoka katika familia maskini na kufuzu katika chuo cha matibabu cha Khyber mwaka 1990.

Familia yake imekuwa ikiishi katika maficho tangu kukamatwa kwake , ikihofia shambulio la kijeshi.

Mkewe ni msomi kutoka Abbotabad ambaye alikuwa mwalimu mkuu wa Shule ya serikali kabla ya kwenda mafichoni.

Wawili hao wana watoto watatu – wavulana wawili na msichana mmoja – watoto wawili wakiwa watu wazima sasa.

Januari 2012 , maofisa wa Marekani walikiri hadharani kwamba Dk. Afridi alikuwa akikifanyia kazi kikosi cha Ujususi cha Marekani.

Lakini haijulikani jukumu lake lilikuwa ni lipi katika CIA.

Hakusema lolote kuhusu jukumu lake wakati kesi yake ilipokuwa ikisikizwa na tume ya Abbottabad kuhusu mauaji hayo.

Dk. Afridi hakujua ni nani aliyekuwa akilengwa katika operesheni hiyo wakati alipoajiriwa na CIA kulingana na uchunguzi wa Pakistan.

HUKUMU YAKE

Japokuwa awali alikuwa ameshtakiwa kwa kutekeleza uhaini, Dk. Afridi alifungwa Mei 2012, baada ya kupatikana na makosa ya kufadhili kundi la Lashkar-e-Islam, kundi la wapiganaji lililopigwa marufuku.

Alihukumiwa kifungo cha miaka 33 jela kwa madai ya kushirikiana na kundi hilo na mahakama moja ya kikabila, ijapokuwa hukumu hiyo ilipunguzwa na kufikia miaka 23 baada ya kukata rufaa.

Daktari huyo pia alishutumiwa kwa kutoa msaada wa dharura kwa wapiganaji hao na kuyaruhusu makundi kama hayo katika hospitali ya serikali aliyokuwa akisimamia.

Familia yake imekana mashtaka hayo na mawakili wake wanasema kwamba fedha alizotoa ni kikombozi cha dola 6,375 ili kumwachilia baada ya kutekwa 2008.

Alidaiwa kuliambia shirika la habari la Fox News kwamba alikuwa ametekwa na kuteswa na majasusi wa Pakistan.

Mwaka mmoja baadaye alifanikiwa kupeleka barua aliyoandika kwa mkono kwa wakili wake akisema kwamba amenyimwa haki.

SAKATA LA OSAMA

Japokuwa maofisa walikasirishwa na kile walichokiona kama ukiukaji wa haki ya uhuru wa taifa hilo, shirika la ujasusi lililazimika kukiri hadharani hawakujua kwamba mwanzilishi huyo wa kundi la al – Qaeda alikuwa akiishi kwa siri katika eneo hilo katika nyumba ya ghorofa tatu ambayo ilikuwa imezibwa na kuta ndefu kwa miaka kadhaa.

Hadi kufikia sasa , mchakato mzima wa kesi yake umeanzishwa chini ya usimamizi wa sheria za uhalifu za Uingereza , ambazo zilitawala maeneo ya kikabila karibu na mpaka na Afghanistan hadi mwaka uliopita.

Mahakam za kikabila zilisimamiwa na maafisa wa utawala, zikisaidiwa na baraza la wazee wa kikabila na hawakuwa wakifuata sheria inavyohitajika.

Hiyo ilionekana kuwa njia rahisi ya kukabiliana na Afridi, ikiwa sio suala la kufanyika hadharani.

Lakini kuunganishwa kwa maeneo ya kikabila na mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa mwaka uliopita kunamaanisha kwamba kesi hizo zimerudishwa katika mahakama za kawaida.

Katika siku ya kusikilizwa kwa kesi yake hukumu yake inaweza kupunguzwa ama kuongezwa , kwa kuwa waendesha mashtaka watahoji.

Tangu alipohamishwa mwaka uliopita kutoka Gereza la Peshwar hadi Punjab, kumekuwa na madai kwamba huenda akaachiliwa, ikiwezekana kupitia kubadilishana wafungwa na Aafia Siddiqui , mtu aliyedaiwa kuwa mshirika wa al – Qaeda ambaye kwa sasa yuko gerezani nchini Marekani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here