23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Daktari aeleza sababu wagonjwa wa ini kupewa ARV

Na AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM

DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Mfumo wa Chakula, Tuzo Lyuu, amesema sababu za wagonjwa wa homa ya ini (hepatitis B) kupewa dawa za ARVs ni kuwaondoa katika hatari ya kupata madhara zaidi kama kansa ya ini na ini kusinyaa.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu jana, Dk. Lyuu alisema dawa za ARVs zinazotumika sio zote ila ni za aina mbili; Tenofovir na Lamivudine ambazo pia husaidia kuzuia wadudu kuzaliana, hivyo kusababisha kinga za mwili kuzalishwa.

“Ni kweli dawa hizo zinatumika na zinafanya kazi kwa HIV na hepatitis B, lengo kubwa ni kumwondoa mgonjwa kwenye ‘risk’ ya kupata madhara au matatizo zaidi kama kansa ya ini na kusinyaa kwa ini, kwahiyo mtu anavyoanza matibabu tunategemea wadudu watapungua sana.

“Pia tunategemea ini litarudi katika hali ya kawaida na  matumizi hayo yatafanya wadudu kuacha kuzaliana,  lengo jingine ni mgonjwa kuzalisha kinga inayowazuia wadudu wasizaliane.

“Kwahiyo tuna makundi mawili ya wagonjwa wanaoanza dawa. ‘Group’ la kwanza ni yule ambaye ana madhara makubwa (big complication), mfano kusinyaa ini. Huyu atatumia dawa maisha yake yote.

“W pili ni yule ambaye ini limeanza kuharibiwa, lakini halijasinyaa. Huyu atatumia dawa mpaka afikie malengo yote. Hapa kila mtu ana muda, tutakuwa tunamwazishia dawa na tunaendelea kumfuatilia, tukiona amefanikiwa tunamwongezea tena miaka mingine kama mwaka mmoja hadi miwili,” alieleza Dk. Lyuu.

Alibainisha kuwa kwa sasa mwitikio wa watu kujitokeza kupima homa ya ini umeongezeka tofauti na zamani kutokana na kupata wagonjwa ambao wako katika hatua za awali.

“Watu wengi kwa sasa angalau wana mwamko, kwa sasa tunapata wagonjwa ambao hawajaathirika sana kama zamani ambapo walikuwa wanakuja wakiwa wameathirika zaidi, wapo walioenda kupima kwa hiari yao wakakutwa na ugonjwa na sasa wameanza matibabu,” alisema.

Dk. Lyuu aliitaka jamii kuachana na imani potofu kuwa mate, jasho na kumgusa mtu kunaambukiza homa ya ini kitu ambacho sio kweli kwani ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia ya damu na kemikali.

“Kemikali zinazosababisha ugonjwa huo ni matumizi ya pombe na pia matumizi ya dawa kuzidi kama Paracetamol, kwa wale wanaotumia kwa kiwango kikubwa inaharibu seli,” alisema.

Hata hivyo Dk. Lyuu aliwashauri watu kujitokeza kwa wingi kupima afya zao ili waweze kupata matibabu ya mapema na chanjo ya ugonjwa huo.

“Watu wakapime afya zao ili waweze kujua hali yao, pili kuna zile njia ambazo zinajulikana kama kujamiiana na njia ya damu, watu wajitahidi kuepukana, kujamiiana inajulikana, watu watumie kinga au kuwa mwaminifu kwa mpenzi mmoja.

“Tafiti zinaonyesha kuwa katika nchi zinazoendelea maambukizi kwa kiasi kikubwa yanatoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa sababu kina mama hawapimi hepatist B, kina mama wajawazito ni vizuri wakapima ili waweze kupata chanjo ya kumkinga mtoto,” alisema Dk. Lyuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles