ELIZABETH KILINDI -NJOMBE
MASHAHIDI wawili, akiwamo daktari aliyemtibu mwanafunzi wa Shule ya Msingi Madeke, Hosea Manga, ambaye anadaiwa kupata ulemavu wa uti wa mgongo kutokana na adhabu, wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe walivyoshudia tukio hilo.
Kesi hiyo namba 141 ya mwaka 2019 ya Jamhuri dhidi ya Focus Mbilinyi, inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Ivan Msaki.
Shahidi wa tatu ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Madeke, aliyekuwa akisoma darasa moja na Hosea, akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Elizabeti Mallya, alidai kuwa mnamo Machi 21, mwaka 2017, Mwalimu Focus Mbilinyi alitoa zoezi la hesabu na baadaye kutoa adhabu kwa waliokosa.
Alidai kuwa yeye na wanafunzi wenzake akiwamo Hosea walipokea adhabu hiyo.
Shahidi huyo alidai kuwa yeye alikosa hesabu sita na akatandikwa viboko vitano, huku akishuhudia mwenzake Hosea aliyekosa hesabu zote akipewa adhabu ya viboko akiwa amening’inizwa kichwa chini miguu juu.
Kwa upande wa shahidi namba nne, Dk. Silvery Mwesige, kutoka Taasisi ya Mifupa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Moi), Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa, alisema kuwa alianza kumuhudumia mtoto Hosea kuanzia mwanzoni mwa Aprili mwaka 2017.
Alidai kuwa baada ya vipimo majibu yalionyesha alikuwa na mgandamizo sehemu ya mwisho ya uti wa mgongo hali iliyofanya damu isiweze kufika eneo hilo.
Baadaye uliibuka mvutano wa kisheria kwa mawakili watetezi ambao awali walipinga na kuhoji uhalali wa taarifa ya matibabu kutoka Taasisi ya Moi, iliyowasilishwa na Dk. Mwesige kwa madai kuwa shahidi huyo hakushiriki katika baadhi ya vipimo vya mtoto Hosea.
Pingamizi hilo lilimalizwa na Hakimu Msaki ambaye alitoa uamuzi mdogo na ufafanuzi wa kisheria kubainisha uhalali wa taarifa na vielelezo viliyowasilishwa na Dk. Mwesige.
Dk. Mwesige alipoulizwa na upande wa utetezi, aliiambia mahakama kuwa hawezi kuthibitisha kuwa adhabu ya viboko alivyopewa mtoto Hosea, inaweza kuwa ndiyo imesababisha tatizo alilonalo.
Lakini alikiri kwamba adhabu ya viboko inaweza kuwa na tatizo la kiafya kama la mtoto Hosea, kutegemeana na nguvu na nyenzo anayotumia mtoa adhabu.
Shauri hilo limeahirishwa na litaendelea kusikilizwa Desemba 2.
Kesi hiyo ni ya pili kufunguliwa kwa tukio lililomkuta mtoto Hosea Manga.
Kesi ya awali namba 83 ya mwaka 2017 ilifutwa kutokana na daktari aliyemtibu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara nane.