Na WAANDISHI WETU,
MSHTUKO. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa miaka 15, Philemon Ndesamburo, kufariki dunia ghafla jana.
Vilio, huzuni na simanzi vimetanda ndani ya mji wa Moshi na vitongoji vyake, baada ya kusambaa taarifa za kifo cha Ndesamburo maarufu ‘Ndesapesa’.
Ndesamburo ambaye pia ni Mweneyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, alifariki dunia baada ya kuanguka ofisini kwake akitekeleza majukumu yake ya kila siku.
Akizungumza na MTANZANIA, mtoto mkubwa wa marehemu, Sindato Ndesamburo, alithibitisha baba yake kufariki dunia.
Sindato alisema baba yake alianguka ghafla ofisini kwake akiwa anatekeleza majukumu yake ya kila siku, japo hakujua mara moja tatizo lililomsibu.
Alisema wamepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa, ikizingatiwa baba yake aliondoka nyumbani asubuhi akiwa mzima wa afya.
“Kifo hiki kimekuwa pigo kubwa kwa familia nzima, baba yetu alikuwa mzima, asubuhi alitoka nyumbani vizuri kama kawaida yake kuelekea ofisini kwake Keys, baadae tuliambiwa ameanguka ghafla akiwa ameketi kwenye kiti, inasemekana alifariki dunia papo hapo,” alisema
UCHUNGUZI WA KIFO
Akizungumzia taarifa za awali za uchunguzi wa kifo hicho, Profesa Elisante Massenga wa HospItali ya Rufaa ya KCMC, alisema walimpokea Ndesamburo akiwa tayari amefariki dunia.
Alisema baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi wa awali, ilibainika alikuwa na tatizo kubwa kwenye moyo.
“Uchunguzi wa vipimo vingine bado, ila kwa taarifa za awali, kama wataalamu tumebaini alikuwa na shida kubwa kwenye moyo, vipimo vingine vikikamilika tutatoa taarifa rasmi,” alisema.
MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alielezea namna Ndesamburo alivyofariki dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Mbowe alisema kabla ya kufariki, Ndesamburo alikuwa anajiandaa kusaini hundi ya fedha za rambirambi za wanafunzi waliofariki katika ajali ya basi la Shule ya Lucky Vincent mwanzoni mwa mwezi huu, wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha.
“Nimewaita hapa kuwathibitishia juu ya taarifa za kifo cha mwasisi wa chama chetu, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, mjumbe wa Kamati Kuu na mbunge wa vipindi vitatu katika Jimbo la Moshi Mjini, mzee wetu, Philemon Ndesamburo, kilichotokea leo (jana) saa 4.45 asubuhi.
“Chadema tumepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa kwa sababu mzee Ndesamburo alikuwa ni nguzo, alikuwa msaada kwa chama chetu na alikuwa msaada kwa wabunge pia.
“Juzi, alikuwa hapa Dodoma kwenye kikao cha Baraza Kuu, tulipomaliza alirudi nyumbani kwake Moshi ambako jana jioni alimpigia simu Meya wa Jiji la Arusha, Lazaro na kumuuliza waliofariki kwenye ajali ya basi la Lucky Vincent ni wangapi.
“Meya akamwambia ni watu 35, kwa hiyo, akamwambia leo saa tatu asubuhi (jana), meya aende Moshi Mjini ili amkabidhi fedha za rambirambi Sh milioni 3.5 kwa sababu alisema angechanga shilingi laki moja kwa kila familia ya mfiwa.
“Kwa bahati mbaya, meya hakufika saa tatu kama walivyokubaliana na badala yake alifika saa nne. Hivyo basi, waliingia ofisini kwake na mazungumzo yakaanza. Wakati mazungumzo yakiendelea, mzee Ndesamburo alichukua kalamu ili aandike cheki ya rambirambi hizo na kabla hajaijaza, kalamu ikamdondoka mkononi, na hapo akaanza kulegea.
“Meya alipoona hivyo, akamuuliza ‘mzee uko salama’, naye akajibu ‘niko salama’. Pamoja na kusema yuko salama, mzee alizidi kulegea. Kwa hiyo, meya alinyanyuka na kumfuata na alipoona hali inazidi kuwa mbaya, akawaita wahudumu wa pale hotelini kwa mzee, Keys Hotel maana ndiko walikokuwa.
“Wahudumu walipofika, walishirikiana na meya kumchukua na kumkimbiza Hospitali ya KCMC kwa matibabu, ambako aliwekewa mashine ya oxygen kumsaidia kupumua. Lakini baada ya nusu saa tangu alipopokewa, madaktari walitoa taarifa kwamba mzee amefariki dunia,” alisema.
MWENYEKITI WA BUNGE
Wakati Mbowe akisema hayo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliliambia Bunge jinsi alivyopata taarifa za msiba huo, muda mfupi kabla ya mtoto wa marehemu ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (Chadema), hajachangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2017/18.
“Waheshimiwa wabunge, nina tangazo hapa la tanzia ambalo nimelipata muda si mrefu kutoka kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mheshimiwa Freeman Mbowe.
“Aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka 2000 hadi 2015, Philemon Ndesamburo, amefariki dunia leo asubuhi saa 4.45.
“Wakati napata taarifa hizi, binti wa marehemu alikuwa ameomba kuchangia, lakini nikaruka jina lake makusudi na mmesikia alivyolalamika hapa, ndipo nikalazimika kumruhusu achangie.
“Kwa hiyo, mipango ya mazishi tutaendelea kujulishana kwa sababu huyo mzee tulikuwa naye hapa kwa miaka mingi,” alisema Chenge.
IKULU
Naye Rais Magufuli amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndesamburo.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema Rais Magufuli alieleza namna alivyomfahamu Ndesamburo kutokana na kufanya naye kazi wakati wote wakiwa wabunge.
Alisema kuwa walishirikiana, kutaniana na anamkumbuka kwa namna ambavyo alitumia muda wake bungeni kupigania mambo yenye masilahi kwa wananchi wa jimbo lake.
Rais ameitaka familia ya marehemu Ndesamburo na wote walioguswa na msiba kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu.
CHADEMA KILIMANJARO
Akizungumzia kifo hicho, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basili Lema, alisema chama kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo hicho na ni pigo ambalo kamwe halitazibika.
Alisema Ndesamburo amekuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa zaidi ya miaka 20, alikilea kwa nguvu na mali zake kama baba.
“Chadema tumepata pigo kubwa, Ndesamburo alikuwa baba kwetu, alilea chama vema na siasa zake zilikuwa si kutetea masilahi yake binafsi, bali masilahi ya wananchi wa Jimbo la Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro na taifa kwa ujumla,” alisema Lema.
MEYA WA MOSHI
Meya wa Mji wa Moshi, Raymond Mboya, alisema Ndesamburo alianguka ghafla akiwa ofisini kwake, wakati akiandika hundi ya Sh milioni 3.5 kutoa rambirambi yake kwa vifo vya wanafunzi 32 wa Shule ya Lucky Vincent ya mkoani Arusha iliyotokea hivi karibuni.
“Akiwa ofisini kwake na Meya wa Jiji la Arusha, Calisti Lazaro akisaini hundi ya rambirambi, ghafla alianguka, alipokimbizwa Hospitali ya KCMC alikutwa tayari amefariki dunia. Hili ni pigo kwetu, alitulea vijana kwenye maadili mema ya kisiasa,” alisema.
NATSE
Aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema), alisema kifo hicho kimekishtua chama na taifa zima.
Aliwataka wana familia na jamii nzima kutafakari kwa kina juu ya kifo hicho na kuiga mfano wa mambo yote aliyofanya Ndesamburo, ikiwa ni pamoja na kuishi vema na jamii.
ZITTO KABWE
Naye Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo hicho.
“Ni msiba mzito kwa watu wa Kilimanjaro, hasa Moshi Mjini. Ndesapesa alikuwa mwakilishi wao bungeni kuanzia mwaka 2000 hadi 2015, Kilimanjaro imepoteza mtu ambaye aliweka masilahi ya mkoa wake mbele kuliko kitu kingine chochote,” aliandika Zitto katika ukurasa wa Facebook.
WANANCHI
Nao baadhi ya wananchi wa mjini hapa, wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema Ndesamburo alikuwa miongoni mwa wanasiasa wanaopaswa kuigwa kutokana na namna alivyoendesha siasa zake bila kuwa na chuki wala kinyongo na mtu au chama kingine.
Teresia Urio, alisema enzi la utawala wake, Ndesamburo alijitahidi kuhakikisha jimbo lake linakuwa tofauti na majimbo mengi.
Aliweza kuwafundisha wananchi wake kuendesha siasa kwa hali ya amani na utulivu.
“Kwa namna alivyotulea Ndesamburo, ni vigumu kuona Moshi kuna maandamano au uvunjifu wa namna yoyote ile wa amani zinazotokana na siasa, licha ya jimbo hili kuwa la upinzani tangu mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini mwaka 1992,” alisema Wilson Kusekwa.
WASIFU WAKE
Ndesamburo alizaliwa Februari 19, 1935.
Alikuwa Mbunge wa Moshi Mjini tangu mwaka 2000 na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro.
Desemba mwaka jana, alitunukiwa PhD ya heshima ya utu (Doctor of Humanity na chuo Kikuu cha Biblia cha Japan, ambacho kilitambua mchango wake katika medani ya uongozi, hasa kujitolea na kuhudumia wengine pamoja na jitihada zake za kuhubiri amani wakati wote.
Habari hii imeandaliwa na Upendo Mosha (Kilimanjaro), Maregesi Paul (Dodoma) na Asha Bani (Dar es Salaam)