24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dakika za mwisho za Mkapa

Elizabeth Hombo

VIONGOZI mbalimbali nchini wamemzungumzia Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, huku Rais wa awamu ya pili, Jakaya Kikwete akizungumzia alivyoonana naye siku moja kabla ya kifo chake.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mkapa Masaki jijini Dar es Salaam,  alisema juzi alikwenda hospitali kumwona na wakazungumza kwa muda wa saa moja.

“Jana (juzi) nilienda kumwona hospitali alikuwa na maumivu lakini yalikuwa ya kawaida, tukazungumza mambo mengi, sasa usiku wa manane nilipoambiwa amefariki nikasema imekuwaje tena, kwakweli kifo ni siri kubwa,”alisema.

Alisema taifa limepoteza moja wa kiongozi mkuu ambaye alilitumikia taifa vizuri kwa heshima, uadilifu mkubwa na moyo wa upendo.

MSEKWA afichua waliyoteta naye Dodoma

Naye Spika Mstaafu, Pius Msekwa alisema msiba huo umemwumiza sana kwa sababu ya mahusiano yake ya kikazi yalikuwa ya karibu.

Alisema zaidi kinachomtesa ni walipokuwa kwenye mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma, ambapo Mkapa alimwomba wakae kuzungumza na kutafakari hali ya kisiasa kwa kutumia jopo la wazee wastaafu.

“Na akaniambia kwamba mbona kipindi hiki cha miaka mitano ya Rais John Magufuli hatujakutana kumshauri, ‘je ni sawa si lazima tuishauri Setikali?’ Nikamwambia Mzee Mkapa sisi ni baraza la ushauri hajatuomba ushauri hivyo hatuwezi kutunga ushauri tukampelekea na akautekeleza na anaweza kuutuma kapuni,”alisema Msekwa.

Alisema walikubaliana kuwa hadi hapo Rais Magufuli atakapohitaji ushauri ndipo watafanya hivyo.

Kuhusu anavyomkumbuka Mkapa, Msekwa alisema marehemu alikuwa kiongozi mahiri na kwamba alitambua umuhimu wa mihimili ya dola hasa mahusiano baina ya Serikali na Bunge.

“Mihimili inayoendesha shughuli za kisiasa ni Serikali na Bunge, yeye alitambua umuhimu wa mhimili wa Bunge katika kufanikisha shughuli za Serikali kwa sababu Bunge ndio inapitisha bajeti ya Serikali, Serikali haiwezi kufanya chochote bila sheria kwa sababu ni suala la utawala bora. 

“Ili Serikali iweze kutawala vizuri lazima kuwe na sheria, hivyo Bunge likikwamishwa na Serikali itakuwa imekwama, marehemu alijenga mahusiano mema kati ya mihimili hiyo, kwakweli kipindi cha utawala wake tuliendesha nchi vzuri sana,”alisema Msekwa.

Vilevile alisema katika kuthibitisha kuwa Mkapa aliamini ushauari wake, mwaka 1995 alipoingia madarakani na kumchagua Frederick Sumaye kuwa Waziri Mkuu, alimfuata na kumwomba ushuari.

“Wakati ule alipomchagua Sumaye alikuwa ni kama anabahatisha, kama hana uhakika akaniita kuwa wewe ndio unawajua wabunge wako, unafikiri huyu mtu atakubalika na atapita kwenye kura za wabunge.

“Nikamwambia Rais chaguo lako lazima litapita tu, hawawezi kukuangusha na kweli, japo Sumaye alikuwa hajuliakani sana wakati ule ingawa alikuwa Waziri wa Kilimo lakini hakujulikana sana kwenye duru za kisiasa.

“Lakini nilipoenda bungeni na niliposoma jina lake wabunge wakakubali wakapiga kura za kumthibitisha ndio mahusiano yangu mimi na marehemu yalivyokuwa, kwakweli nitaendelea kumkumbuka,”alisema Msekwa.

Alipoulizwa ni jambo gani kubwa analikumbuka wakati wa utawala wa Mkapa, alisema ni mambo mawili makubwa yote kuhusu Zanzibar kwa sababu kwa wakati huo siasa za visiwa hivyo zilikuwa zikiwaumiza sana.

Alisema ulipokaribia uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 wakatokea kikundi cha wazee kutoka Pemba na wakati huo walikuwa wakielekea Dodoma kwa ajili ya kikao cha Halmashauri Kuu, lakini wazee hao walieleza wazi kwamba wanataka katiba ibadilishwe ili Rais wa wakati huo wa Zanzibar, Salmin Amour apewe kipindi cha tatu.

“Na wale wazee walisema endapo hawatakubaliwa watarudi na chama cha Afro Shiraz yaani wataondoka CCM, hivyo Mkapa akaniomba ushauri wakati huo nikiwa spika na mjumbe wa kamati kuu, nikasema kwanza katiba inasema hivyo na zaidi ya katiba, Mwalimu Julius Nyerere ndiye muasisi wa wazo hili kwamba msimwachie kiongozi mmoja akaamua atoke madarakani lini.

“Bali ni uamuzi wa katiba na lazima tumuenzi Mwalimu Nyerere, tuisimamie katiba tukakubaliana, tukakwenda kwenye kikao kwa msimamo huo, mimi nikawasilisha jambo hilo kwenye kikao nikasema hili ni wazo zuri na linazungumzika lakini huu sio wa wakati kwa sababu tuna pressure ya uchaguzi hivyo wazo hilo likakubaliwa na wengi na Rais wa Zanzibar naye akawa mstaarabu na baadaye mapendekezo hayo ndio yakaleta utulivu,”alisema. 

Alisema jambo la pili ambapo hasahau ni baada ya uchaguzi huo wa mwaka 2000 kumalizika, CUF ikakataa matokeo na ikatokea vurugu hadi kufikiwa raia wengi kuuawa.

“Mkapa akaniomba ushauri kwamba tufanyeje tunapokwenda kwenye kikao nikamwambia tutafute chanzo hasa kilichotufikisha, basi akaunda tume hiyo kamati ikaingia kwa undani kuchambua sababu iliyotufikisha hapo mapendekezo yale tukayafanyia kazi yakaleta utulivu na ninapoyakumbuka yananitesa sana,”alisema Msekwa.

HUSSEIN MWINYI

Kwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Mwinyi alisema Mkapa kiongozi mzalendo na alikuwa mstari wa mbele kutetea masilahi ya nchi na kwamba wamejifunza mengi kupitia utendaji wake uliotukuka.

MBATIA

Naye Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Mkapa ameondoka katika mazingira ambayo ni ghafla na alikuwa tofauti na viongozi wengi kwa sababu aliweza kuacha zawadi ya maisha yake ya namna aliyoyafanya na anayoyajutia.

Mbatia aliwataka Watanzania kutumia mambo yote  mazuri ya Mkapa hasa alipopata kueleza kuwa kuna umuhimu wa kufanyika mjadala wa kitaifa kuhusu mfumo wa elimu wa hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles