28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

DAKIKA 90 ZA UBINGWA YANGA * yaikamia Polisi Moro leo.

yangaABDUCADO EMMANUEL NA THERESIA GASPER, DAR

NI sherehe tu! Timu ya Yanga imepanga kufungua champagne endapo watapata pointi tatu dhidi ya Polisi Morogoro leo, zitakazowafanya kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu.

Yanga itashuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini hapa ikisaka pointi tatu dhidi ya Polisi Moro zitakazowafanya kufikisha pointi 55 ambazo hazitaweza kufikiwa na mabingwa watetezi Azam FC wenye pointi 45 katika nafasi ya pili.

Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, jana alilihakikishia MTANZANIA kuwa wameandaa champagne na jezi za kutosha kwa ajili ya kusherehesha ubingwa huo kama watautwaa leo.

“Tunajua umuhimu wa mchezo huo (Polisi Moro) ambao utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wetu kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini sisi lengo letu ni ushindi ili kutangaza ubingwa mapema.”

“Kama unavyojua ubingwa unaambatana na sherehe, hivyo kesho (leo) kutakuwa na fulana za kutosha na champagne za kusherehesha ubingwa, japokuwa tutakuwa tumebakisha mechi mbili, hivyo nawaomba wapenzi wa Yanga waje kwa wingi uwanjani kuona burudani hiyo,” alisema.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm, naye alisema: “Mechi ya kesho (leo) ni muhimu sana mbali ya kuwa ya ubingwa, nimepanga kuitumia kukisoma kikosi nitakachokipanga kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Etoile du Sahel.”

Wakati Yanga ikitamba hivyo, kocha wa timu ya Polisi Morogoro, John Tamba amedai kuwa hawatakubali kuwa ngazi ya Yanga kutangaza ubingwa, wamejipanga kushinda ili kujinasua kwenye janga la kushuka daraja.

“Tumeshakamilisha maandalizi yetu na tumejiandaa kwa ajili ya kuzoa pointi tatu ili tuendelee kupanda juu na sio kushuka daraja,” alisema.

Yanga itakuwa na kibarua kigumu kupata pointi hizo kutokana na Polisi Moro kuwa kwenye vita ya kuwania kutokushuka daraja, hivyo Polisi wataingia uwanjani kwa lengo la kushinda na kutoka katika nafasi ya 12 wakiwa na pointi 25.

Hata hivyo, kwenye mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Yanga ilishinda kwa mbinde bao 1-0 lililofungwa na Danny Mrwanda wakati huo Polisi Moro ilikuwa ikinolewa na kocha Adolph Rishard aliyetimuliwa mwezi uliopita.

Kwenda Tunisia na watu 70

Yanga inatarajia kuondoka na msafara wa watu 70 keshokutwa kuelekea Tunisia kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile utakaofanyika jijini Sousse nchini humo Jumamosi hii.

“Ndege tutakayotumia itakuwa na watu 68, wawili tutawapitia Afrika Kusini na kufanya idadi ya watu 70, lakini kuna wengine wanne watatokea Ubelgiji kuja kuisapoti Yanga Tunisia. Katika idadi yote hiyo watu 29 ni wachezaji, benchi la ufundi pamoja na sisi viongozi, waliobakia wote watakuwa mashabiki (45),” alisema Tibohora.

Katibu Mkuu huyo alisema wamejipanga kukabiliana na hujuma zote za Etoile, ambapo leo wanatarajia kumtanguliza mtu Tunisia atakayekwenda kuweka mambo sawa kabla ya wao kutua nchini humo Alhamisi asubuhi.

“Popote hujuma zipo tulikutana na hayo mambo Botswana, Zimbabwe na hata huko tumejipanga kupambana nazo, tunatarajia baada ya mtu wetu kufika kule atatuwekea mambo yote sawa lengo ni timu kufika eneo zuri bila kubughudhiwa,” alisema.

Yanga iliyolazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani, inahitaji ushindi wowote au sare ya kuanzia mabao 2-2 ugenini ili kusonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano kabla ya kuingia robo fainali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles