25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DADA WA RAIS MAGUFULI AZIKWA CHATO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mama yake mzazi Suzana Magufuli wakati wakitoa heshma za mwisho katika jeneza lenye mwili wa Marehemu Dada yake Monica Magufuli nyumbani kwao katika kijiji cha Mlimani Chato mkoani Geita jana.

 Na MWANDISHI WETU-CHATO                |                     


DADA wa Rais Dk. John Magufuli, Monica Joseph Magufuli aliyefariki dunia Agosti 19, mwaka huu katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza amezikwa jana katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Mazishi hayo yalitanguliwa na misa takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Mhashamu Severine Niwemugizi aliyeandamana na maaskofu wengine saba.

Pamoja na hilo pia mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Viongozi wengine ni Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, Katibu Mkuu Kiongozi,  Balozi John Kijazi, mawaziri, wabunge, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Awali akisoma wasifu wa marehemu kwa niaba ya familia, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,  Gerson Msigwa alisema marehemu Monica Magufuli alizaliwa Novemba  25 mwaka 1955 na ni mtoto wa kwanza wa Mzee Joseph Magufuli na Mama Suzana Ngolo.

Msigwa alisema Monica ameacha mume, watoto tisa na wajukuu 25.

Akitoa salamu zake Rais Dk. John Magufuli, aliwashukuru viongozi na wananchi wote waliojitokeza kuungana na familia yake katika kumsindikiza dada yake katika safari yake ya mwisho.

Alisema familia inatambua upendo, heshima na mshikamano mkubwa ambao wameuonesha kwao.

“Mmetuonesha upendo mkubwa sana na kweli ujio wenu na kuungana nasi katika tukio hili mmetufariji sana, asante sana kwa upendo huu na Mungu awabariki sana,” alisema Rais Magufuli.

Akimwelezea dada yake, alisema alikuwa mtu mwenye upendo kwa familia nzima na alikuwa tegemeo kubwa la kumtunza mama yake mzazi Suzana Ngolo na kwamba alikubali kuondoka nyumbani kwa mumewe kwa zaidi ya miaka miwili na kurudi nyumbani kumlea mama yao mzazi.

“Marehemu Monica ameacha somo kwa watoto wote na wanandoa kuwa tayari kujitolea kuwalea wazazi wao wanapokabiliana na changamoto za uzee badala ya kuwaacha wakitaabika,” alisema Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles