26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

CWT yaomba Serikali kulipa madeni

Na Ranadhan Hassan, Dodoma

Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimeiomba Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kulipa madai mbalimbali ya walimu ambayo bado yapo kwenye Halmashauri ili kuongeza ari ya kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.

Pia, imeiomba kuwajengea nyumba walimu wa shule za pembezoni ili iwe rahisi kufika na kuwafundisha watoto shuleni.

Hayo yameelezwa jana jijini hapa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Deus Seif  wakati akizungumza katika  hafla  ya utoaji wa tuzo za ubora wa Taaluma kwa matokeo ya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi, Kidato cha Nne na Kidato cha sita kwa Mwaka 2021 kwa mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Katibu Mkuu huyo amesema CWT kinatambua jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika kuboresha maisha ya watanzania wakiwemo walimu hivyo ameiomba kulipa madai mbalimbali ya walimu ambayo bado yapo kwenye Halmashauri ili kuongeza ari ya kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.

“Pia kuna madai mbalimbali ya walimu bado yapo katika Halmashauri zetu na hata Wizarani, likizo, matibabu, uhamisho, malimbikizo ya mishahara, madaraja, masomo tunaomba uhakiki wa mara kwa mara ufanyike na walimu walipwe ili kuongeza ari ya kufanya kazi,”amesema.

Amesema jitihada inazofanya chama  ni kuhakikisha miundombinu katika sekta ya elimu inaimarika kwa kuweka  mikakati  ya kuwasaidia walimu hivyo wameiomba Serikali iwasaidie hasa walimu wa pembezoni waweze kupata nyumba ambazo zipo karibu na shule.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Innocent Bashungwa amewataka wakuu wa shule zote nchini kusimamia miradi yote kwa ufasaha ili iendane na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali.

“Wapo baadhi yenu hawana mahusiano mazuri na jamii hivyo hukwamisha utekeleaji wa baadhi ya shughuli za serikali hasa miradi mnapokuwa na mahusiano mazuri na viongozi katika jamii hii pia inarahisisha katika utekelezaji na hata utunzaji wa majengo ya serikali,”amesema.

Amesema ili kufikia malengo ya serikali ni lazima kusimamia miradi yote kwa ufasaha na iendane na thamani ya fedha, na mali za shule zitunzwe kwa ufasaha ili ziweze kutumika na vizazi vijavyo.

“Natoa maagizo kwa wakuu wote wa shule nchini kuhakikisha kwamba wanasimamia sheria, miongozo na taratibu katika sekta ya elimu, kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao, pamoja na kutunza majengo ili yatumike hata katika vizazi vijavyo,”amesema

Naye, Kaimu Rais wa CWT, Dina Mathamani amesema wao kama walimu wameona umuhimu wa kutoa tuzo na pongezi kwa walimu waliofanya vizuri na kuwafanikisha wanafunzi kufaulu vizuri.

Mathamani amesema CWT kinafanya  kazi kwa weledi ili kuhakikisha ufaulu unaongezeka ili tupate wataalamu katika sekta mbalimbali

“Ufaulu unaendelea kupanda siku hadi siku taaluma zinapanda na mazingira ya walimu yataendelea kuboreshwa na niahidi kwa niaba ya CWT tutafanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha ufaulu unaongezeka ili tupate wataalamu katika sekta mbalimbali,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles