RAMADHAN HASSAN-DODOMA
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema kinaifanyia kazi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu matumizi ya mali na fedha.
Pia kimesema kupitia Bodi ya Wadhamini, kitaendelea kulinda na kutetea masilahi na mali za walimu nchini.
Hayo yalielezwa jana jijini hapa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa CWT, Clement Mswanyama, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mswanyama alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu umiliki wa mali za CWT.
Pia alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu majengo, mali za chama hicho na Benki ya Walimu (MCB) kutumiwa vibaya, pamoja na umiliki wa Kampuni ya Teachers Development Company Ltd (TDCL).
Mswanyama alisema kwamba CWT itaendelea kulinda na kutetea mali za walimu nchini kwa kuhakikisha zinakuwa katika mikono salama.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CWT toleo la sita la mwaka 2014, mali za chama zitaandikishwa kwa jina la Bodi ya Wadhamini, pia mikataba yote, hati na dhamana za fedha za chama zote zitamilikiwa kwa jina hilo na kuhifadhiwa kwa Katibu Mkuu wa CWT.
Mswanyama alisema wanaishukuru ofisi ya CAG kwa kufanya ukaguzi katika chama chao na kwamba wanaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ambayo yamependekezwa katika usimamizi wa fedha na mali.
Alisema Benki ya Walimu inamilikiwa na walimu kwa asilimia 51.35 kwa mchanganuo wa CWT asilimia 12.94, TDCL asilimia 3.23 na walimu asilimia 35.18 na kufanya jumla ya asilimia 51.35.
Aliwataja wengine wanaohusika katika umiliki wa hisa ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF asilimia 16.17, Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF) asilimia 16.17, Public asilimia 16.31 hivyo kufanya asilimia 48.65 na kuunganisha asilimia 100.