Na Ally Badi, Lindi
MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zainab Kawawa, juzi alifukuzwa na vijana wa Kijiji cha Makinda waliokuwa na mawe na magongo wakati akijiandaa kufanya mkutano wa hadhara.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Makinda kilichopo Kata ya Kipule Wilaya ya Liwale, Salum Salum Kachwele, amelithibitishia MTANZANIA Jumamosi kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa Mbunge Kawawa alikutana na zahama hiyo wakati akijiandaa kutangaza nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Liwale.
Kachwele alisema Mbunge Kawawa alifika nyumbani kwake siku ya Alhamisi saa nane mchana na kumuomba aitishe mkutano wa wajumbe wa Serikali ya Kijiji na baadhi ya wananchi hasa wazee maarufu ili awaeleze nia yake ya kuwania ubunge wa Jimbo la Liwale.
“Mbunge Kawawa alifika hapa akiwa ameambatana na mpambe wake anayeitwa Mkopora Mkopara, wakaniomba niitishe mkutano wa wajumbe wa Serikali ya kijiji na wazee maarufu ili awashawishi wamuunge mkono katika harakati zake za kuwania ubunge wa hapa.
“Mimi sikukubaliana naye kwa sababu kabla ya harakati zake za sasa za kutaka kuwania ubunge wa jimbo, hajawahi kufanya kikao chochote wala kutembelea kijiji chetu. Na kabla hajaanza kukutana na wanachi, lilikuja kundi kubwa la likiongozwa na vijana waliokuwa wakizomea huku wakiwa na mawe na magongo mikononi na kumtimua Kawawa,” alisema Kachwele.
Alisema kundi hilo la watu lilitokea katika mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) uliokuwa maalumu kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kukichagua chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alipoulizwa Kawawa iwapo alikuwa kijijini hapo na alifukuzwa na wananchi waliokuwa na mawe na marungu, alisema ni kweli alitembelea eneo hilo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuwatembelea wapiga kura na kuhamasisha maendeleo.
“Ndugu yangu hayo maneno siyo ya kweli, mimi nilikwenda kijijini hapo kufanya kazi za kibunge siyo kufanya kampeni kama ilivyoelezwa na hao watu wasionitakia mema. Ukweli ni kwamba mti wenye matunda matamu ndiyo unaopigwa mawe,” alisema Kawawa.
Katika siku za karibuni kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya wabunge wa CCM kuzomewa wakiwa katika shughuli za kisiasa.
Tukio la hivi karibuni lilimkuta Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, ambaye alizomewa na kunusurika kupigwa na wananchi alipodaiwa kutaka kuharibu uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa za eneo hilo.
Mbali na Mahanga, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, naye ameripotiwa kunusurika kupigwa na wananchi kwa tuhuma za kuingilia mchakato wa uchaguzi wa aina hiyo hiyo katika jimbo lake.