23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

CUF walia mkwamo wa kisiasa Z’bar

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Salim Biman.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Salim Biman.

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kuwa mkwamo wa kisiasa uliopo visiwani Zanzabar, unatokana na kutoheshimiwa misingi ya demokrasia nchini.

Kutokana na hali hiyo chama hicho kimesema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, imekuwa ikichangia hali hiyo kutokana na kauli za mkuu huyo wa nchi.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Salim Biman, ilieleza kuwa pamoja na hali hiyo wataendelea kusimamia msimamo wao wa kutomtambua Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kama Rais halali wa visiwa hivyo.

Alisema kwa sasa nchi imeingia katika mtanziko mkubwa wa kiuongozi kutokana na Serikali ya Rais Magufuli kuonekana kwa kiasi kikubwa kushindwa kuheshimu misingi ya utawala bora.

“Ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na vitisho vya matumizi ya nguvu za vyombo vya dola imekuwa kwa kasi kubwa katika kipindi cha Desemba 2015 hadi Augosti 2016 zaidi ya viongozi na wananchama wa vyama vya upinzani 946 wamekamatwa, wamewekwa maabusu bila kufunguliwa mashataka, huku wakinyimwa dhamana na wengine kufunguliwa kesi zisizokuwa na madai ya msingi.

“Wazanzibari walifanya maamuzi halali ya kidemokrasia Oktoba 25 mwaka jana kwa kukipa ridhaa CUF na Maalim Seif Sharif Hamad kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

“Maamuzi yao yameporwa na Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi (ZEC) kwa maelekezo maalumu ya kufuta matokeo hayo bila ya sababu zozote za msingi, za kisheria na taratibu za uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.

“Tume za uchaguzi haziko huru wala hazitendi haki, washirika wa maendeleo kutoka Jumuiya ya kimataifa ikiwemo  Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU),” alisema Biman katika taarifa yake.

Alisema hotuba aliyoitoa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli hivi karibuni katika mikutano yake Kisiwani Unguja ilijaa ukakasi mkubwa na kuivunjia heshima hadhi na nafasi ya taasisi ya urais kwa kuchochea na kuhamasisha kuendeleza mgogoro wa kisiasa badala ya kuwa sehemu ya ufumbuzi amekuwa sehemu ya tatizo.

 

“Awali alisema yeye hana mamlaka ya kuingilia masuala ya Zanzibar na kumpongeza Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha pamoja na kumweleza Dk. Shein kuwa anasapoti yake yote na kusema kuwa. ‘Ukiona umemshindwa mtu, nambie mimi uone kama itapita hata Dakika 5’ kwa hakika kwa kauli hizi bado taifa letu limepata janga na kupita katika msukosuko wa kiuongozi,” alisema Bimani.

Kutokana na hali hiyo, alisema CUF inaungana na wazanzibari wote wapenda haki, amani, na mabadiliko, kuendelea na msimamo wake uliotolewa na kikao cha Baraza Kuu Aprili mwaka huu wa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi huo waliouita ni batili.

“Tunalaani vitendo vya ukiukwaji na ukandamizaji wa haki za binaadamu unaoendelea kufanywa na Serikali zote mbili ikiwemo ubaguzi katika kutoa ajira, wananchi kuvunjiwa makazi yao na sehemu zao za biashara kutokana na sababu za kisiasa,”alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles