CUF UBUNGO WATANGAZA JINO KWA JINO NA KUBENEA

0
481

 

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


CHAMA cha Wananchi (CUF) Kata ya Makurumla wilayani Ubungo, kimetangaza mapambano na mbunge wa jimbo hilo, Saed Kubenea (Chadema).

Hatua hiyo imetolewa  siku chache baada ya Kubenea kutangaza  Oparesheni Ondoa Msaliti Buguruni (OMB) na kuunga mkono upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF Kata ya Makurumla, Issa Njoka, alisema  anashangazwa na hatua ya Kubenea kuizungumzia  CUF wakati   hana uhusiano nayo.

Alisema watapambana na mbunge huyo kwa kila hatua  atakapojaribu kwenda kwenye matawi ya CUF yeye pamoja na genge lake ambao wapo ndani ya chama hicho.

“Tulisikia tamko la Kubenea kama Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Mashariki ya Chadema eti wanataka kuvamia Buguruni ikiwamo kuja kwenye baadhi ya matawi yakiwamo ya Kata yetu ya Makurumla. Tunamkaribisha kwa mikono miwili na akijaribu kufanya hivyo tutamuonyesha tafsiri sahihi ya ngangari.

“Kubena hana tena nasaba na CUF.  Je, anapatwa na nini kuisemea CUF?

“Ajue tulikutana kwenye Ukawa mwaka 2015 na baada ya uchaguzi kuisha kila chama kimerudi kujenga harakati zake na kwa tafsiri nyepesi hapo ndipo Ukawa ilipoishia.

“…ila kama anataka kuja CUF anakaribishwa maana huku nyuma alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti Profesa Lipumba na aliondoka mwenyewe.  Hivyo kama anataka CUF kwanza anarudi  tujue kama ni mwanachama na si vinginevyo,” alise Njoka

Alisema  anaunga mkono hotuba ya Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya  kutangaza mapambano ya jino kwa jino na Chadema kwa kudai kuwa ndiyo wamekuwa wakichochea mgogoro ndani ya chama hicho.

Alisema kwa sasa kuna hujuma za wazi ndani ya CUF ikiwamo watu wa nje kuchochea mgogoro huo  kutafuta huruma ya kuonekana ni nani anayefaa kupendwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif.

“Wapo wanachama na viongozi ambao sasa kazi yao ni matusi dhidi ya Profesa Lipumba.

“Tunawaambia vitendo vyao hivyo chini ya  uratibu wa Chadema katu haviwezi kumuondoa Mwenyekiti wetu, warudi tujenge chama   badala ya kuendeleza matusi amhayo si misingi ya kuanzishwa kwa CUF,” alisema.

Wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Saed Kubenea alitangaza msimamo wa kumuunga mkono Maalim Seif kwa kutangaza oparesheni Ondoa Msaliti Buguruni kwa lengo la kuisaidia CUF.

Mbali na hilo alitangaza kuitembelea matawi ya Ukanda wa Gaza, Mashujaa wa Mwembe Chai, Chechinia na Cossovo kuhuisha matawi hayo na kurudisha hamasa ya CUF.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here