CUF LIPUMBA, CHADEMA SASA JINO KWA JINO

1
594
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kutoa tamko kuhusu hujuma alizodai kufanywa na Chadema dhidi ya chama chao. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Jaffary Mkene

PATRICIA KIMELEMETA Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


CHAMA cha Wananchi (CUF), upande unaomuunga mkono Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, kimetangaza mapambano ya jino kwa jino dhidi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hatua hiyo imekuja kutokana na madai yao waliyoeleza kuwa viongozi wa Chadema wamekuwa wakiingilia mgogoro wa ndani wa chama hicho sambamba na kuwatisha wanachama wao waliokuwa matawini.

Msimamo huo umekuja siku chache baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema  Kanda ya Mashariki, Saed Kubenea kutangaza operesheni ya Ondoa Msaliti Buguruni (OMG) kama sehemu ya mkakati wa kumwondoa Profesa Lipumba na wafuasi wake katika ofisi za Makao Makuu ya CUF.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, alisema hatua ya viongozi wa Chadema kujitokeza mbele ya umma kutangaza operesheni hiyo, sasa ni wazi chama hicho kinachochea mgogoro ndani ya CUF.

Alisema hatua hiyo inaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani jambo ambalo nao hawezi kukubali.

Sakaya alisema ni wazi Chadema inajidanganya kwani haina uwezo wa kumwondoa Profesa Lipumba na hata tamko lao ni sawa na sehemu ya genge la watu wanaojifurahisha.

“CUF imekuwa na mgogoro wa ndani tangu mwaka jana, Chadema wamekuwa wakiegemea upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad huku wakishindwa kuwasuluhisha. Pia wamekuwa wakitoa matamko mbalimbali ya kutetea upande mmoja jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa vurugu ndani ya chama.

“Kwa hali hiyo, kuanzia sasa hatukubali kikundi cha watu wachache waliopo nje wakiingilia mgogoro ndani ya chama chetu. Na kuanzia sasa tunatangaza jino kwa jino  na Chadema popote tutakapokutana kati yetu na wao sasa itakuwa vita.

“Wanatujua vizuri jinsi tulivyo, lakini nashangaa wanavyoingilia kati matatizo yetu… kama walidhani CUF itakufa wamefeli, naomba niwaambie ama zao, ama zetu,” alisema Sakaya.

Alisema CUF inatambua mipango ya wazi inayofanywa na Chadema kwa kutaka chama hicho kife ili wao wapate idadi ya wanachama kutoka CUF jambo ambalo ni gumu.

“Tunajua Chadema lengo lao wanataka CUF ife ili wao wabaki kuwa chama cha upinzani chenye nguvu na ndiyo maana wamekuwa wakitia nguvu sana kwenye mgogoro,” alisema Sakaya.

Kutokana na hali hiyo, alisema tayari wameandika barua kwa Jeshi la Polisi ikiwamo kumweleza mkuu wa jeshi hilo, (IGP) Simon Sirro na kueleza azma yao ya kulipiza kisasi dhidi ya Chadema.

“Tayari tumeshawasilisha barua yetu kwa Polisi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kama ushahidi wa hiki tunachokieleza,” alisema Sakaya.

Alisema CUF haikuja kibahati mbaya, bali wananchi wamekuwa wakiamini chama na wanakiunga mkono na si kwa kulazimishwa kama wanavyotaka iwe Chadema.

“Kuna viongozi wachache ambao ni waasi wa chama wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa Chadema kwa ajili ya kuleta mgogoro ndani ya chama, naomba muwape salamu zao kwa sababu uamuzi tutakaochukua siyo mzuri na sisi wanachama wa CUF tunajuana,” alisema.

Aliongeza kuwa muda waliokaa kimya unatosha, kilichobaki ni kufanya uamuzi kulingana na matakwa yao, hivyo basi hakuna mtu atakayeweza kuwalaumu.

“Tupo imara, tuna nguvu, tunafanya kazi kwa moyo, hivyo hatushindwi kufanya lolote tunalolitaka, mwisho wa siku tusije kulaumiana kwa sababu tunaamini kitaeleweka tu hapo baadaye,” alisema.

Alisema kwa sasa wamejipanga na wanaendelea na kazi ya kukijenga chama katika ngazi zote.

1 COMMENT

  1. Kwa Ukweli CUF imejichanganya yenyewe. Je uko radhi kuona Taifa linajigawa kwa sababu ya bendra, pesa, na uongozi. Ni shida kwa Wanasiasa wengi wavivu ambao hawana ubunifu mwingine kimaendeleo dhidi ya siasa. Mtu alijitoa ,wenyewe kwa hiari. Analazimisha mambo. Mtungi ni msajili tu. Si mwidhinishi. Cama kilimkubali kujitoa kwake. Itakuwaje tena afosi mambo. Ni ujinga mtupu na hana haya.Nyinyi wasomi wanasiasa wenye uchu wamadaraka na pesa.
    Hamna hata aibu.
    Nawe Ester unatamani kuwa Waziri, au makamu wa raisi. Ebu acheni mbwimbwi zenu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here