SEKTA ya elimu nchini Cuba imekuwa ikizidi kupiga hatua tangu mapinduzi ya nchi hiyo miaka ya 1950.
Shiriki la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), limeitaja Cuba kama nchi yenye mfumo bora kabisa wa elimu kwa upande wa Latin Amerika, pamoja na kuwa miongoni mwa nchi ambazo hazijaendelea katika ukanda huo.
Hata hivyo, hili linaonekana kutoshangaza, kwani kama ilivyo katika sekta ya afya, sekta ya elimu ipo chini ya serikali na imekuwa ikitenga asilimia 13 ya Pato la Taifa (GDP).
Kama ilivyo katika huduma ya afya nchini humo, elimu pia inatolewa bure kwa raia wote ambapo watu wenye uwezo wa kusoma na kundika ni asilimia 99.8.
Kabla ya mabadiliko makubwa ya kimapinduzi yalipofanyika, yalikuwa ni maeneo ya vijijini pekee ambayo yalishindwa kupata elimu ya msingi kwa kiwango stahiki. Lakini kwa sasa, kumekuwa na shule za kutosha kutoa elimu katika kila kona ya kisiwa cha Cuba.
Ikumbukwe kuwa, kwa sababu elimu na nyenzo zake zote huendeshwa na kutolewa na serikali, kuna idadi ndogo sana ya shule za kimataifa na hata zile za watu binafsi.
Cuba kuna shule mbili tu za kimataifa ambazo ni Shule ya Kimataifa ya Havana (International School of Havana) na Shule ya Kifaransa ya Havana (École Française de La Havana).
Iwapo raia wa nchi hiyo atashindwa kumpeleka mtoto wake katika moja ya shule hizo mbili, anaweza kufikiria kumpeleka kupata masomo ya Kihispania ili kumwandaa mtoto kwa ajili ya shule za nchi hiyo.
Kwa ujumla, mfumo mzima wa elimu nchini Cuba unagharimiwa na serikali kwa asilimia 100, hiyo ikiwa na maana kwamba wanafunzi wa nchi hiyo wa viwango vyote wanaweza kupata elimu bila malipo yoyote.
Serikali ya Cuba imekuwa ikiwekeza sehemu ya bajeti yake katika elimu, ikifanya hivyo kwa miaka mingi.
Pamoja na uwekezaji wake huo, Cuba pia imekuwa ikipata sapoti katika kuboresha elimu kutoka kwa marafiki zake, mfano ukiwa ni kwa Marekani.
Mapema mwezi uliopita, Rais Barack Obama wa Marekani na Rais wa Cuba, Raul Castro walikutana katika mkutano wa kihistoria baina yao uliolenga kuangalia ni vipi nchi hizo zinaweza kushirikiana katika mambo mbalimbali, ikiwamo elimu.
Mkutano huo umekuja ikiwa ni baada ya mwaka 2011 Serikali ya Cuba kufanya mabadiliko makubwa ambayo yalisaidia kuboresha maisha ya raia wake kupitia sekta mbalimbali, ikiwamo ya elimu.
Lakini, ushirikiano wa nchi hizo mbili, haukuanza leo, bali ni wa muda mrefu japo kwa nyakati kadhaa ulionekana kama kuzorota.
Tangu nchi hizo zilipoanza ushirikiano rasmi katika sekta mbalimbali, miongoni mwa mabadiliko yaliyofanyika ni kuzidi kusambaa kwa madarasa ya Kiingereza, huo ukiwa ni moja ya mpango uliofikiwa katika makubaliano ya ushirikiano baina ya Cuba na Marekani.
Shule kadhaa zimeanzishwa, zikiwa zinafundisha masomo ya Kiingereza na sanaa chini ya uratibu wa Cuba na Marekani.
Hadi sasa, tayari kuna shule nne za aina hiyo katika mji wa Havana na nyingine mbili zinatarajiwa kufunguliwa katika Jimbo la Pinar del Rio.
Shule zote hizo zimekuwa zikifanya kazi kwa kushirikiana na shule mojawapo ya serikali iliyopo katika eneo husika.
Sambamba na hilo, shule hizo zimekuwa zikitoa mwalimu mmoja kwenda kufundisha somo la Kiingereza kwenye shule za serikali.
Takribani wanafunzi 800 katika maeneo mbalimbali nchini Cuba, wanapata masomo yao kwa njia ya mtandao.
Shule zimekuwa zikitoa huduma ya somo la Kiingereza kwa kufundisha sarufi na uandishi wa insha.
Pia, kumekuwapo na madarasa maalum kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta mbalimbali, kuanzia za biashara hadi afya, utalii, chakula na usafiri.
Kwa siku za hivi karibuni, Serikali ya Cuba imekuwa ikisisitiza juu ya umuhimu wa kujifunza Kiingereza, ili kuwawezesha raia wake kukabiliana na changamoto mbalimbali pale linapokuja suala la mawasiliano na mataifa mengine au raia kutoka nje ya nchi hiyo.
Lakini pia, mkakati huo umekuja kutokana na jinsi sekta ya utalii ilivyopanuka ambapo watu kutoka mataifa mbalimbali, wamekuwa wakiingia nchini humo ili kufanya utalii.
Kati ya Januari na Mei 2015, kulikuwa na ongezeko la asilimia 14 katika sekta ya utalii huku raia wengi wa Marekani wakijiandaa kwenda kutembelea kisiwa hicho.
Takwimu zinazonyesha kuwa mwaka jana asilimia 36 ya Wamerakani walitembelea Cuba kati ya Januari na Mei.
Usikose mwendelezo wa makala haya Ijumaa ijayo.