NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI ya CRDB imewatahadharisha wateja wake kuwa makini na watu wanaowapigia simu na kujitambulisha kama wafanyakazi wa benki hiyo kuepuka kutapeliwa.
Benki hiyo imesema limeibuka wimbi la matapeli wanaowapigia simu baadhi ya wateja na kuwalaghai wawape namba za akaunti au namba za siri za huduma ya benki inayotolewa kwa kutumia simu ya mkononi (Sim banking).
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dk. Charles Kimei, alisema utapeli wa namna hiyo uko kwenye benki zote hivyo kuna haja ya kuvaliwa njuga kuhakikisha unakomeshwa.
“Sisi huwa tunawapigia simu wateja wetu na kuwaelekeza namna ya kukamilisha usaili wao kwenye huduma ya sim banking lakini hakuna mfanyakazi yeyote atakayekupigia na kukuambia umpe namba yako ya siri au ya kadi,” alisema Dk. Kimei.
Alisema hivi sasa upo mkakati wa kuhakikisha watu wote waliofungua akaunti katika benki hiyo ambao ni zaidi ya milioni moja wanajiunga na huduma ya sim banking.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Hatarishi katika benki hiyo, James Mabula, alisema wizi kwa kutumia mitandao unafanyika kupitia simu, kadi za kutolea fedha, intaneti na mashine ndogo zilizoko kwenye maduka makubwa au hoteli.
Alisema mtu ambaye anabadilisha laini ya simu hataweza kupata huduma ya sim banking hadi atakapotembelea matawi ya benki hiyo kwa sababu ya usalama.