25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

CRDB yakabidhi madarasa kwa Waziri Mkuu

Na MWANDISHI WETU – LINDI

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa  amepokea msaada wa vyumba viwili vya madarasa vikiwa na  madawati vyenye thamani ya Sh milioni 80 kutoka Benki ya CRDB.

Alipokea msaada huo jana katika Shule ya Sekondari  Kassim Majaliwa iliyopo Kata ya Nachingwea, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi. 

Waziri Mkuu aliushukuru uongozi wa CRDB kwa msaada huo ambao umesaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa unaoikabili wilaya hiyo. 

Kadhalika, alizitaka taasisi nyingine ziige mfano wa benki hiyo kwani imekuwa bega kwa bega na Serikali katika kuchangia shughuli za kimaendeleo nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wanafunzi wa shule hiyo kutumia vizuri madarasa hayo na kutunza mali zilizopo shuleni hapo.

Alisema ujenzi wa shule hiyo ni mradi uliobuniwa na wakazi wa Kata ya Nachingwea ili kuwawezesha watoto wao kupata elimu katika eneo lililo karibu na makazi yao.

Waziri Mkuu alisema awali wanafunzi wa kata hiyo walikuwa wanatembea umbali mrefu hadi Shule ya Sekondari Ruangwa jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kwao.

 “Nawaomba wananchi wenzangu tuendelee kushirikiana katika kuibua na kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha maendeleo kwenye kata yetu ya Nachingwea,” alisema.

 Pia Waziri Mkuu alikabidhi kompyuta 20 kwa shule za sekondari tano ambazo ni Kassim Majaliwa, Likunja, Mnacho, Hawa Mchopa na Ruangwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki yao inathamini elimu na imekuwa ikirudisha kwa jamii faida wanayoipata kwa kuchangia shughuli za maendeleo.

Alisema mbali na msaada huo wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na madawati yake, pia aliahidi kutoa Sh milioni 20 ili zitumike kununulia madawati yatakayosaidia kupunguza changamoto ya madawati wilayani Ruangwa.

Kwa upande wao, wakazi wa Kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa waliishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono katika mradi wa ujenzi wa shule hiyo ya sekondari ambayo imewawezesha watoto wao kusoma karibu na maeneo ya makazi yao.

Mmoja wa wakazi hao, Omari Losi alisema ujenzi wa shule hiyo utawaondolea wanafunzi shida ya kutembea umbali mrefu kwenda Shule ya Sekondari Ruangwa walikokuwa wakisoma awali.

 Mkazi mwingine, Mariam Kingamkono alisema uwepo wa shule ya sekondari katika kata yao kumeongeza hamasa ya wanafunzi kupenda kusoma kwa sababu wameondolewa shida ya kutembea umbali mrefu.

Alisema shule hiyo ina walimu wazuri na wa kutosha na ina mazingira mazuri ya kujifunzia, hivyo aliwaomba wazazi wenzake waendelee kushirikiana na Serikali katika kuboresha maendeleo kwenye kata yao hususan ujenzi wa shule. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles