29.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 17, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Crdb sasa kusimamia mikopo ya asilimia 10 Dar

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wakati Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikijiandaa kuanza kukopesha Sh bilioni 15 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Crdb ni mojawapo ya benki itakayosimamia utoaji wa mikopo hiyo.

Benki hiyo imetambulishwa leo Februari 24,2025 wakati wa mkutano maalumu wa utambulisho wa benki katika usimamizi na utoaji mikopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tully Mwambapa, amesema watatoa elimu kwa wananchi kuhusu upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 na umuhimu wa kurejesha kwa wakati ili wengine waweze kunufaika.

“Tunadhamiria kuimarisha juhudi zetu ili kuhakikisha kwamba kila mwanamke, kijana na mjasiriamali katika makundi maalumu anapata fursa ya kuboresha maisha yake kupitia programu ya asilimia 10 ya Serikali na programu yetu ya Imbeju.

“Tutahakikisha kuwa matumizi ya mikopo hii yanachangia maendeleo ya walengwa kupitia usimamizi na tathmini za mara kwa mara. Tutashirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi katika kuimarisha utekelezaji wa mpango huu,” amesema Mwambapa.

Aidha amesema walibaini bado kuna uhitaji mkubwa wa kuwafikia wanawake, vijana na makundi maalumu hatua iliyosababisha kuanzishwa kwa kampuni tanzu ya Crdb Bank Foundation mwaka 2023 yenye jukumu la kukuza ujumuishi wa kifedha na kiuchumi kupitia programu maalumu ya Imbeju.

“Programu ya Imbeju imejikita katika kuwafikia wanawake, vijana na makundi maalumu katika sekta zote za kiuchumi ikiwemo biashara, kilimo, ufugaji, uzalishaji na ubunifu wa kiteknolojia. Tunapanua wigo wa fursa na kuhakikisha huduma zetu zinawafikia walengwa wote nchini na kuwawezesha wanawake na vijana kuuza bidhaa zao kwenye masoko nje ya Tanzania,” amesema.

Kulingana na Mkurugenzi huyo hadi kufikia Januari 2025 kupitia Programu ya Imbeju Crdb Bank Foundation imefanikiwa kutoa elimu ya fedha na mafunzo ya biashara kwa zaidi ya wanawake na vijana wajasiriamali 800,000 na mitaji wezeshi yenye thamani ya Sh bilioni 20.2 ikiwemo zaidi ya Sh bilioni 14.1 kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Benki hiyo pia imekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya Sh milioni 45 kwa maofisa maendeleo ya jamii ili kuongeza ufanisi wao kwani wanaamini vitanachangia kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha utoaji wa mikopo hiyo na utunzaji wa taarifa unafanyika kwa ufanisi.

Vifaa hivyo ni kompyuta 21 zikiwemo 18 za mezani kwa ajili ya maofisa maendeleo wa kata 18 na kompyuta mpakato tatu kwa waratibu wa maendeleo wa Jiji la Dar es Salaam.

Kulingana na mkurugenzi huyo, hadi kufikia mwaka 2024 mikopo ya Sh trilioni 10.4 ilitolewa na benki hiyo kwa sekta zote ambapo asilimia 30 ya mikopo hiyo zaidi ya Sh trilioni 3.1 zilielekezwa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema zaidi ya wananchi 945 wameomba mikopo hiyo na kutoa wito wa kuzingatiwa kwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anataka kila Mtanzania mwenye sifa apate.

“Tukasimamie na kutenda haki, tusije tukaangalia makosa madogo madogo kama sababu ya kuwakata watu, tusome dhamira ya mheshimiwa rais, tukasimamie maagizo ya Wizara ya Tamisemi…watu wanataka kupima matokeo baada ya kuchukua mkopo ambayo yanatakiwa yawe chanya,” amesema Mpogolo.

Aidha amesema kuchaguliwa kwa Benki ya Crdb ni ishara inayoonyesha kwamba inafanya vizuri na wanaamini itakwenda kufanya kwa vitendo ili kukidhi matarajio ya Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
595,000SubscribersSubscribe

Latest Articles