28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

COSTECH: SERIKALI ITUSHIRIKISHE KUJENGA UCHUMI WA VIWANDA  

Na ASHA BANI


UKUAJI wa kasi wa matumizi ya sayansi na teknolojia utachochea zaidi  ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini  mpaka kufikia 2025.

Serikali imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili kuongeza kasi ya kufikia lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo imedhamiria kuifikisha Tanzania kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati na kuondokana na umasikini kufikia mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, aliwahi kusema kuwa hali ya viwanda tangu kuanza ubinafsishaji wa mashirika ya umma mwaka 1992 , viwanda 106 vimebinafsishwa kwa wawekezaji wa ndani na kutoka nje  ya nchi, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa usimamizi, uzalishaji ajira, kupunguza uagizaji wa bidhaa na kwamba nyingine ziweze kuzalishwa hapa nchini na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Katika kufanikisha lengo la Tanzania ya Viwanda, Tume ya Sayansi na Teknolojia  (Costech) ni lazima iwe katika mstari wa mbele kuhakikisha hilo linafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na Serikali katika mambo mbalimbali ya ushauri na ubunifu wa teknolojia .

Mkurugenzi wa Idara ya Uhawilishaji na Uendelezaji Sayansi na Teknolojia  wa Costech, Dk. Dugushilu Mafunda, anaelezea jinsi tume hiyo itakavyoweza kusaidia ukuaji wa viwanda na uchumi kwa kushirikishwa vilivyo.

Anasema ili kufanikiwa kuwa na uchumi wa viwanda, lazima nchi iwe na vipaumbele vyake vya kuanza navyo ambapo zamani havikuwepo lakini kwa sasa vipo.

Anasema Costech inatakiwa kuwa katika mstari wa mbele  katika kufanikisha uchumi wa viwanda kwa kuishauri Serikali  mambo mbalimbali ya teknolojia ambayo itawafikia walaji ndani na nje ya nchi.

Anasema suala la teknolojia na ukuaji wa viwanda nchini unahitaji mambo mengi ambayo Serikali ikishirikiana na taasisi zake, watafanikiwa katika hilo na maendeleo yatapatikana kwa haraka.

Akiendelea kuelezea jinsi tume inavyofanya kazi, anasema jambo la msingi ni katika usimamizi wa suala la uwekezaji na jinsi  teknolojia itakavyoweza kubaki nchini pindi mikataba itakavyoisha au wawekezaji watakavyoamua kuondoka nchini.

Anasema Tanzania ili iweze kunufaika ni lazima suala la ubinafsishwaji liangaliwe kwa umakini, ikiwa ni pamoja na kitendo cha kusaini mikataba ya uwekezaji uwajumuishe wao na wanasheria ambao wamebobea na kuielewa technolojia.

Anaeleza katika hilo  Costech wanatakiwa kupewa kipaumbele katika kusimamia mikataba ili kuhakikisha wawekezaji wale wanapoondoka nchini ujuzi uendelee kubakia kwa wafanyakazi wa Kitanzania kwa kuajiri watu wa kujifunza au kuwaendeleza katika viwanda au makampuni yao.

Anasema sababu za kutaka wao waweze kusimamia mikataba ni kutokana na kuwa na uwezo wa kujenga hoja kuliko kuwategemea wanasiasa kama ilivyotokea hapo awali kuingia mikataba isiyokuwa na manufaa ya kukuza uchumi na kubakisha teknolojia nchini.

“Unajua kwa sasa Tanzania tunafurahia wawekezaji wakija nchini kwamba wanatoa ajira nyingi kwa Watanzania, lakini tusifurahie ajira tu bali tunatakiwa kufurahia pindi wanapoondoka, lakini wanashindwa kuacha ujuzi waliokuja nao.

“Suala la wawekezaji kuacha teknolojia, uzoefu, uwezo  kwa wafanyakazi lazima uwepo na suala hilo ni lazima pia kuwepo kwenye mikataba ya wawekezaji hao kuwajengea uwezo watu pindi wanapoondoka wawe wameacha wataalamu,” anasema Dk. Mafunda.

Anasema  hilo linaangaliwa hasa katika  uwekezaji mbalimbali uliopita ikiwemo wa makaa ya mawe, Liganga na Mchuchuma  kwa kushindwa kujiandaa kutokana na mikataba  kutosimamiwa na kuonyesha vyema kipengele cha kuacha teknoloji na ujuzi nchini.

Anasema  katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, tayari Serikali imejipanga  na kuanza na reli ambayo itahakikisha inabeba mizigo mikubwa , tayari barabara za mwendo kasi, bandari na miradi ya Liganda na Mchuchuma.

“Miradi hiyo itafungua milango lakini kuna uhitaji mkubwa wa kuangalia suala la uhimilishwaji wa teknolojia kwa kuhusisha Costech katika mikataba yao  kwa ajili ya usimamizi na kuishauri Serikali kusimamia hilo,” anasema Dk. Mafunda.

Anasema Serikali imeweka nia ya viwanda  katika kukuza viwanda  lakini pia wanashirikiana na vyuo vikuu kuhakikisha hilo linafanikiwa.

“Wenzetu teknolojia inaingia sokoni bila tatizo ila ni lazima kuwepo na mkono wa Serikali kwa kuwepo mfumo ambao teknolojia yake itaingia sokoni,” anasema.

Anasema ni lazima teknolojia hiyo iweze kuwafikia wengi ikiwa ni pamoja na kupanua wigo ili kuangalia dunia  inavyokwenda na mataifa mengine.

Dk. Mafunda alihoji  kuwa Tanzania ni nchi iliyojaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za Taifa lakini wanapenyea wapi? Alitolea mfano maliasili za Taifa hili kwamba huwezi kukwepa kutumia dawa za Kiafrika  ambazo Tanzania imejaaliwa kuwa na misitu  na ndio sababu wageni wanaingia nchini kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali za ugunduzi wa dawa hizo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles