25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

COSTA: CHELSEA WANANICHUKULIA KAMA ‘MHALIFU’

LONDON, ENGLAND

MSHAMBULIAJI wa timu ya Chelsea,

Diego Costa, amesema Chelsea wamekuwa wakimchukulia kama ‘mhalifu’ na kuthibitisha kwamba bado anatamani kurejea Atletico Madrid.

Costa mwenye miaka 28, Mei mwaka huu ilikuwa mara ya mwisho kucheza kikosi cha Chelsea katika fainali ya Kombe la FA kabla ya Juni mwaka huu kutumiwa ujumbe wa simu na kocha wake, Antonio Conte, kumfahamisha kwamba hakuwa kwenye mipango yake ya msimu ulioanza siku chache zilizopita.

Costa amesema sasa klabu hiyo inamlazimisha kurejea akafanye mazoezi na wachezaji wa akiba.

“Ni kwanini hawataki kuniacha niondoke iwapo hawanitaki?” Alisema Costa wakati akihojiwa na mtandao wa Daily Mail.

“Lazima nifanye yale yanayonilazimu kuyafanya. Lazima nifikirie kuhusu masilahi yangu. Nimekuwa kijana mwenye tabia nzuri hapa na nilijaribu kufanya kila kitu kiende sawa. Mapenzi yangu ni kwenda Atletico,” alisema Costa.

Costa alisema Januari mwaka huu  alifanya mazungumzo na kocha wa timu hiyo na alikaribia kutia saini mkataba mpya lakini baadaye suala hilo lilisimama.

“Nashukuru kocha alihusika na alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha hili linafanyika. Lakini kwa sasa mawazo ya Conte ni wazi hayabadiliki na inaonesha yeye ni mtu wa aina gani. Ana mtazamo wake na huo hautabadilika.

“Namheshimu sana kama kocha. Amefanya kazi nzuri na naona hilo, lakini kama binadamu si mkufunzi ambaye ana uhusiano wa karibu na wachezaji. Hukaa mbali. Hana sifa za kuhusiana vyema na wachezaji.

“Sijaufuta ujumbe huo wa simu. Watu wakinituhumu kwamba nasema uongo, naweza kuwaonesha. Ujumbe huo ulikuwa wazi, alisema simo kwenye mipango yake na akanitakia kila la kheri siku zijazo,” alisema Costa.

Mshambuliaji huyo mwezi uliopita alipewa muda zaidi wa kupumzika lakini sasa anasema anaadhibiwa kwa jambo hilo.

Costa alisema anatozwa faini kwa kutokuwa kwenye klabu muda huo na amesema anafikiria kwenda mahakamani au kujaribu kumaliza sehemu iliyosalia ya mkataba wake bila ujira nchini Brazil.

“Unajua kocha hanitaki,” aliongeza Costa.

“Nasubiri Chelsea waniachilie huru. Sitaki kuondoka. Nilikuwa na furaha. Lakini kocha asipokutaka ni lazima uondoke,” alisema Costa.

Costa ambaye ni mzaliwa wa Brazil lakini huchezea timu ya taifa ya Hispania, alijiunga na Chelsea mwaka  2014 akitokea Atletico Madrid kwa  uhamisho wa pauni milioni 32.

Nyota huyo alidumu misimu minne Atletico na tayari amedokeza kwamba huenda akarejea katika klabu hiyo. Lakini klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya Hispania ya La Liga imepigwa marufuku kununua wachezaji hadi Januari mwakani.

“Kukaa miezi mitano bila kucheza? Sijui, ni kizungumkuti, lakini watu wanajua kwamba naipenda sana Atletico na kwamba huwa napenda kukaa Madrid,” alisema Costa.

Januari mwaka huu, Costa aliachwa nje ya kikosi cha Chelsea kilichosafiri kucheza mchezo wa ugenini dhidi ya Leicester City baada ya kukorofishana na mkufunzi wa mazoezi wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya England.

Jambo hilo lilitokea baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba alikuwa amepata ofa kutoka China ya kulipwa mshahara wa pauni milioni 30 kwa mwaka. Wakati huo, Chelsea walisema hawakuwa na nia ya kumuuza.

Baadaye Januari mmiliki wa klabu ya Tianjin Quanjian, alisema juhudi zao za kutaka kumnunua Costa zilikwamishwa na sheria mpya kuhusu wachezaji wa nje Ligi Kuu ya China.

Kuanzia msimu ujao, klabu za China zinaruhusiwa kuchezesha wachezaji watatu pekee kutoka nje ya nchi kwenye mechi badala ya wanne kama ilivyokuwa awali.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles