23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Corona yasababisha panga pangua afya

 FARAJA MASINDE Na TUNU NASSORO– DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amempongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akisema wakati mwingine alikuwa anaona kama amesimama mwenyewe kushughulikia suala la corona.

Alisema licha ya kwamba Ummy ni mwanasiasa tu na si mtaalamu wa afya, wasaidizi wake ni wataalamu katika sekta hiyo, lakini muda mwingi alionekana akisimama na kutoa maelezo ya kitaalamu.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo ikiwa ni hivi karibuni alitengua uteuzi wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Faustine Ndugulile na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Godwin Mollel ambaye aliapishwa jana.

Pia Rais Magufuli alimteua Profesa Mabula Mchembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuchukua nafasi ya Dk. Zainabu Chaula ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Mawasiliano.

Jana Rais Magufuli alisema wakati mwingine alikuwa akimpigia Waziri Ummy simu hata mara nane kwa siku, na kumpongeza kwa namna alivyoweza kusimamia suala hilo. 

“Ugonjwa huu ni vita na katika vita kuna mbinu nyingi, niwaombe Wizara ya Afya, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote msikubali kupokea vifaa vya kupambana na corona vinavyogawiwa na taasisi na watu mbalimbali. 

“Jana nimemuona wa NIMR (Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu) anasema anapokea sijui vifaa gani, vitu hivi hapana.

“Kama ni kupokea kifaa chochote cha kupambana na corona lazima kipitie Wizara ya Afya na kiwe kimethibitishwa, sio mtu amekaa huko na kitaasisi chake, tunaomba michango mingine ya watu ya kupambana na corona, kuna mahali fulani waliitisha mradi tutachangia hivi? Hapana.

“Hii ni vita, katika michango hii mingine mnaweza kuletewa barakoa zenye corona na hasa kwa sababu tunakwenda vizuri na tunakwenda vizuri kutokana na hatua tunazozichukua, yako mengi tunachukua, mengine hata hatuzitangazi, vya bure vibaya.

“Ndiyo maana nawapongeza Wizara ya Afya na watendaji wengine, kwa sasa barakoa zinashonwa hapa hapa Jeshi la Wananchi linafanya kazi nzuri, PPE zinashonwa Muhimbili na ni rahisi,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, aliagiza fedha zilizotolewa na Global Fund kutumika kutengeneza vifaa vya afya nchini kwa kuwa itazalisha ajira na kuhifadhi fedha ambazo zitatumika kwa watu wengi. 

“Kwa mtu yeyote atakayepewa vifaa vya kuzuia corona na vikapimwa vikawa na corona, huyo mtu apelekwe kwenye kesi ya jinai, hata ya mauaji kama wauaji wengine, kwa hiyo watendaji wajiepushe kupokea.

“Ndiyo maana waziri amesema ‘tunataka hela’, tutatengeneza barakoa zetu wenyewe, tutanunua vifaa vitakavyofanyiwa vipimo na maabara zetu wenyewe na kuthibitisha ni vifaa kweli vinavyofaa kwa matumizi ya Watanzania.

“Niwaombe Watanzania kwenye hili tuchukue tahadhari kubwa, corona imeshuka chini, inaelekea kuisha, lakini tusije tukapandikiziwa corona kwa uzembe wetu au kwa uzembe wa mtu yeyote.

“Mtu akitaka kutoa msaada apeleke Wizara ya Afya, kuna watalaamu watafanya uhakiki wa kifaa hicho, ndiyo ipo pale wizara kwa ajili ya kulinda afya, vya dezo vinaua. Tunawashukuru wanaotusaidia; Canada, Umoja wa Ulaya,” alisema Rais Magufuli. 

NDEGE ZA WATALII

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema kuanzia Mei 27 na 28 ataruhusu ndege za watalii kuja nchini na kwamba tayari kuna maombi mengi ya mashirika ya watalii na kusisitiza kuwa wageni hawatawekwa karantini kwa siku 14 kama ilivyokuwa awali.

“Pia kuanzia Mei 27 na 28, mwaka huu tutaanza kuruhusu ndege za watalii kuja Tanzania na bahati nzuri wapo wengi tu walioweka nafasi (booking), kuna mashirika mengine yamejaa mpaka karibu mwezi wa nane, hatuwezi tukaachia fursa hii kwa kuendelea kujifungia wakati wao wameona mahali pa kuja kustarehe ni huku.

“Na labda utalii mwingine watafanya na huu wa nyungu kama alivyouelezea Mheshimiwa Jafo (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tamisemi, Seleman Jafo), nao ni utalii wa aina yake, kwa hiyo kuanzia tarehe 27 au 28 ndege zitakuja kwa ajili ya kutalii na hatutawafungia kwa siku 14, hapana, akishatoka huko akishapimwa hapa joto likawa kwenye kiwango kinachokubalika na amelipa hela yake kwa kuja huku, mwache aje.

“Akitaka kujifukizia ajifukizie huko huko na porini huko miti mingi na ile mnaweza kuitoa kama zawadi kwa watalii, itawasaidia pia kuona kwamba kutalii siyo kuona wanyama tu, hata kuona mtu anavyoweza kujifukizia na akanywa madawa ya kienyeji na akapona, inawezekana hii nayo ikawa sekta nayo mojawapo ya kusaidia watu ambao wamekaa wamefungiwa kwa miezi wanakuja Tanzania kuona jua na kuona utukufu wa Mungu kwa kuwaona wanyama walivyo.

“Kwa hiyo niombe vyombo vinavyohusika viwezeshe hili, visiwe tena kama pingamizi, sisi tunataka biashara iende kama ilivyopangwa, kwa hiyo kuanzia tarehe 27 na 28 ndege za watalii zitaanza kuja nchini na tutaendelea hivyo, wao wameamua kuja Tanzania wameichagua Tanzania kwa sababu Tanzania sisi ni wakweli na Tanzania ni pazuri,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, aliwataka viongozi wa mikoa watakayotembelea watalii ikiwamo viwanja vya ndege na wengineo wawezeshe suala hilo huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama wasimamie utalii nchini.

“Nataka kuwahakikishia kuwa Tanzania tunaenda vizuri, tuko vizuri na Mungu wetu ameendelea kutusimamia, tulianza na Mungu na nina uhakika tutamaliza na Mungu.

“Hakuna mahali popote taifa lililomtegemea Mungu likashindwa, na mimi ninawahakikishia kwa dhamira yangu, mawazo yangu yanavyonituma Mungu amejibu maombi yetu, amejibu kwa kiasi kikubwa na amejibu kwa kishindo yale tunayoyaona ni muujiza wa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo tuendelee kumshukuru,” alisema Rais Magufuli.

Alisema maandiko ya vitabu vya Mungu yanasema shukuruni kwa kila jambo, ndiyo maana amewaomba Watanzania watakaoguswa watumie siku ya leo (Ijumaa), kesho (Jumamosi) na keshokutwa (Jumapili) kumshukuru Mungu,’’ alisema Rais Magufuli.

MAAGIZO KWA WATEULE

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwaomba wateuliwa wapya kufanya kazi kama walivyoaminiwa na taifa kwa kuwa anaamini ni wachapa kazi na watu wazuri.

“Nawaomba wateule wapya msiliangushe taifa hili, tufanyeni kazi, nyinyi ni watu wazuri, ni wachapakazi kila mmoja katika eneo lake, nina uhakika mkienda kujituma mtafanya makubwa, kila mmoja akasahau yaliyopita, mkaangalie sasa mnakwenda kuifanyia nini Tanzania,” alisema Rais Magufuli.

Akitolea mfano Taifa la Algeria kuwapo na elimu nzuri inayohusu mafuta na gesi, alimtaka balozi aliyepangwa kuhakikisha ndani ya miezi sita ya uteuzi wake awe amefanya kitu kwa Tanzania.

“Amezungumza profesa pale kuwa Algeria ni mahali ambapo kuna elimu inayohusu gesi, petrol, iko mbele sana na Tanzania kuna gesi nyingi, huu ndio wakati.

 “Wewe ni Meja Jenerali, huko Algeria tuna mahusiano mazuri katika masuala ya kijeshi na tuna wanajeshi wengi walipelekwa mafunzo kule na wanafanya vizuri, huu ndio wakati wa kutengeneza muunganiko mgumu kama za kikemikali kati ya Algeria na Tanzania,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa Msumbiji ni nchi marafiki wa karibu na majirani kwa Tanzania, hivyo akamtaka Balozi Phaustine Kasike kwenda kutatua matatizo yao kwa kukuza biashara na ushirikiano.

Pia, alimtaka balozi atakayekwenda Kenya kuimarisha uhusiano wa kibiashara kwa kuwa ni moja ya nchi ambazo zimewekeza zaidi nchini.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru kushughulikia rushwa zote ambazo zinawasumbua wananchi kwa nguvu zote kwa kuwa amekaimu kwa muda mrefu hivyo asiende kulala.

“RAS (Katibu Tawala Mkoa wa Pwani), Dk. Delphine Magere wewe ni mchumi, sasa tunataka kuona kuwa uchumi wa Pwani utapanda kweli, tumewaamini na mkatimize hayo, ofisi zetu zipo, mko huru kuzungumza na yeyote,” alisema Rais Magufuli.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,426FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles