27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yasababisha mkutano SADC kufanyika kwa mtandao

DAR ES SALAAM

KASI ya kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona (Covid-19) imesababisha kubadilishwa kwa utaratibu wa uendeshaji wa vikao ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambavyo sasa vitaendeshwa kwa njia ya televisheni, badala ya kukutana katika nchi kiongozi kama ilivyokuwa awali.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge alisema kutokana na ushauri uliotolewa katika maazimio ya kikao cha dharura cha mawaziri wa afya wa SADC kilichofanyika juzi.

 “Kufuatia ushauri uliotolewa katika maazimio ya kikao cha mawaziri wa afya wa SADC, Kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC kilichopangwa kutanguliwa na kikao cha maofisa waandamizi Machi 12 hadi 14, kimefupishwa na sasa kitafanyika kwa njia ya video kuanzia Machi 16 hadi 18. 

“Kwa hiyo utaratibu wa mkutano wa Baraza la Mawaziri unaotarajiwa kufanyika Tanzania kama mwenyekiti wa jumuiya hiyo utabadilika kwa kuufanya mkutano huo kwa njia ya video ambapo mawaziri watafanya mkutano wakiwa katika nchi zao,” alisema Kanali Ibuge.

Alisema utaratibu huo wa kuendesha mkutano kwa njia ya video umeridhiwa na Sekretarieti ya SADC pamoja na nchi mwenyekiti kwa kuwa unalenga kuondoa hatari ya kuenea kwa ugonjwa wa corona endapo mmoja kati ya washiriki atakuwa amepata maambukizi. 

Kanali Ibuge alisema uamuzi huo unatokana moja kwa moja na ushauri wa kikao cha dharura cha mawaziri wa SADC wanaoshughulikia sekta ya afya kilichojadili hali halisi ya Covid -19 duniani na katika nchi za SADC, maandalizi ya nchi za SADC katika kukabiliana na ugonjwa huo na hatua za kuchukuliwa kuzuia kuenea kwa Covid-19 katika nchi za SADC.

Kanali Ibuge alisema Serikali haina namna kwa kuwa inatambua kuwa utaratibu huo mpya wa kufanya mkutano kwa njia ya video kwa namna moja au nyingine utaleta athari kwa nchi yetu ambayo Serikali na wananchi wake walishajiandaa na mapokezi ya wageni hao kwa kuwa wafanyabiashara wa hoteli, usafiri na chakula vitu ambavyo Watanzania wamekuwa wakifaidika navyo katika mikutano hiyo. 

“Pamoja na athari hizo, Serikali inaungana na nchi wanachama wa SADC kuona umuhimu wa kulinda afya za wananchi wake kwa kuepuka mikusanyiko yoyote inayohatarisha kuenea kwa ugonjwa huo,” alisema Kanali Ibuge.

Alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba kasi ya kusambaa imekuwa kubwa na sasa tayari nchi 101 kati ya 194 duniani zimeshaathirika ikiwemo Afrika Kusini, ambayo ni mwanachama wa SADC.

Alieleza kuwa kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo ambacho sasa kitaendeshwa kwa njia ya video, kitakuwa chini ya Mwenyekiti wake ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na kushirikisha mawaziri wanaoshughulikia mambo ya nje, viwanda, biashara, fedha na mipango kutoka nchi wanachama wa SADC.

“Mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo endelevu na jumuishi ya viwanda, kukuza biashara na ajira ndani ya SADC,” alisema Kanali Ibuge. 

Alisema ajenda nyingine ni pamoja na masuala ya fedha na michango ya jumuiya, tathmini ya utangamano itakayowezesha nchi wanachama kujipima kuhusu utekelezaji wa malengo ya SADC baada ya 2020 (Post 2020 agenda), Dhima ya SADC hadi kufikia 2050 na Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC 2020-2030. 

“Agenda nyingine ni maadhimisho ya miaka 40 ya SADC, upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia ujumbe wa SADC wa waangalizi wa uchaguzi, pasi za kusafiria za SADC na uanzishwaji wa Shirika la Utalii kwa nchi za Kusini mwa Afrika,” alisema Kanali Ibuge. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles