26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yakwamisha wanaosoma China

Ramadhan Hassan na Nora Damian – Dodoma/Dar

WAKATI vifo kutokana na maambukizi ya virusi vya corona vikiongezeka na kufikia 170, Serikali imewataka wanafunzi walioko likizo kutorudi China hadi itakapojiridhisha na mwenendo wa ugonjwa huo.    

Vifo hivyo ni hadi kufikia juzi, huku idadi ya watu waliothibitika kuwa na virusi ikifikia 7,700.

Akizungumza bungeni jana wakati wa maswali ya papo kwa papo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Wizara ya Mambo ya Nje inaendelea kufanya mawasiliano kuhusu mwenendo wa ugonjwa huo.

Majaliwa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosata Chumi (CCM), ambaye alitaka kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema Serikali itakaporidhika na hali inayoendelea nchini China, itatoa tamko kwa Watanzania walioko likizo kurudi kuendelea na masomo na iwapo hali ikiendelea kuwa mbaya itatafuta utaratibu mwingine.

 “Tunatambua kuna wazazi wana watoto wanasoma China na wengine wamesharudi likizo, tunawasihi wasiende kwanza China mpaka hapo tutakapopata mawasiliano ya kidiplomasia.

“Watanzania wanaohitaji kurudi Tanzania na kwa kuwa watalazimika kusafiri kwenye treni na mabasi wawasiliane na balozi namna bora ya kusafiri kwa mawasiliano ya kimtandao,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali imejipanga kuimarisha mawasiliano na ofisi za ubalozi na kwamba Balozi Mbelwa Kairuki amekuwa akitoa mrejesho wa kile kinachoendelea nchini humo.

“Balozi anafanya kazi nzuri ya kutoa elimu kwa Watanzania, kwanza ametafuta madaktari wa Kitanzania ambao wamejifunza ugonjwa huo na kuelimisha Watanzania waliopo China namna ya kujikinga.

“Balozi amewakanya Watanzania wasiwe na mizunguko mingi kwa sababu ugonjwa huo maambukizi yake ni pale watu wanapokutana.

“Kila Mtanzania awe makini na wageni wanaoingia mpakani, na wale wote tuliowaweka mpakani kuhakiki wanaoingia nchini watumie vifaa vyetu kikamilifu ili kubaini wenye dalili za ugonjwa huo kuudhibiti usiingie Tanzania,” alisema Majaliwa.

MASHINE ZAFUNGWA JNIA

Mshine 11 zimefungwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kudhibiti virusi vya ugonjwa huo visiingie nchini.

Mdhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza wa JNIA, Dk. George Ndaki, alisema kati ya mashine hizo, tano zinatumia kompyuta kupima joto la mwili la abiria bila kujitambua na sita ni za mkononi ambazo abiria anapimwa endapo ataonekana kuwa na joto kali zaidi.

“Mashine moja imefungwa kwenye jengo la watu mashuhuri (VIP), nyingine imefungwa jengo la pili la abiria na tatu zipo jengo la tatu la abiria. Zile za mkono zimegawanywa kwenye majengo hayo,” alisema Dk. Ndaki.

Alisema wataalamu wa afya wanaokuwa kwenye mashine zinazotumia kompyuta wanamtambua abiria mwenye joto kali mara anapopita mbele ya kamera na endapo litabainika ni zaidi ya nyuzi joto 37.4 anahakikiwa zaidi kwa kutumia mashine ya mkono, huku akihojiwa kuhusu afya yake na nchi aliyotoka kubaini endapo ana virusi hivyo.

Dk. Ndaki alisema pamoja na kukaguliwa kwa abiria wote wanaowasili kutoka nje ya nchi, pia wanaweka mkazo zaidi kwa abiria wanaotoka nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huo, ambapo abiria wake mbali na kupimwa joto la mwili, pia wanaandikwa majina yao na maeneo wanayokwenda baada ya kutoka JNIA.

“Kuna ndege ambazo zinakuja na abiria waliotoka China baada ya kuunganisha ndege kama Kenya Airways, Qatar, South Africa, Fly Emirates na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), zinakuwa aidha zimebeba abiria waliounganisha ndege kutoka nchi zilizoshambuliwa na homa ya corona,” alisema Dk. Ndaki.

WATANZANIA WANAOSOMA CHINA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kiongozi wa Shirikisho la Watanzania Wanaosoma China (Tasafic), Leila Hassan, alisema vyuo vingi vilipaswa kufunguliwa kati ya Februari 10 na 15, lakini muda umesogezwa mbele.

 “Taarifa ya Waziri Mkuu tumeisikia na hata baadhi ya vyuo katika majimbo mbalimbali wamewataka wanafunzi waliopo nje ya China wasirejee kwa wakati huu mpaka pale hali itakapotulia.

 “Hivyo tunaendelea kusubiri ‘updates’ kwa sababu hata ukiuliza ni lini chuo kitafunguliwa, jibu unalopewa bado haifahamiki,” alisema Leila ambaye anasoma katika Chuo Kikuu cha Henan kilichopo mji wa Kaifeng.

Alisema walitakiwa kufungua Februari 15 waanze usajili wa muhula wa pili, lakini tarehe imesogezwa mbele kwa muda usiojulikana.

 “Chuo chetu kina Watanzania 21 tu, ila kwa idadi ya Jimbo la Henan tupo takribani Watanzania 250. Hili jimbo lipo karibu sana na Jimbo la Hubei ambapo ndani yake kuna mji wa Wuhan ambao ugonjwa ndipo ulipoanzia… Sisi na hilo jimbo ‘tuna-share’ tu mpaka, ni kama vile Dar na Morogoro.

“Kwa sasa tupo tu ndani, tunaambiwa kuwa makini katika nyendo zetu kujizuia na maambukizi, kujikinga kwa kuvaa ‘mask’ na kutojichanganya sehemu zenye mkusanyiko mkubwa wa watu,” alisema Leila.

Alisema pia licha ya Serikali ya China kuruhusu wanafunzi wanaotaka kurudi makwao, lakini changamoto kubwa imekuwa ni kupanda kwa gharama za nauli hali iliyosababisha wengine kuamua kubaki vyuoni.

 “Baadhi ya mataifa wameshachukua raia wao, kwa Watanzania waliopo nje ya Jimbo la Hubei – Wuhan, wanaruhusiwa kurudi makwao kwa gharama zao wenyewe wakiwa na kibali maalumu kutoka chuo husika.

 “Hili jambo limejitokeza ghafla, kwa hiyo muda wa kukata tiketi ni mdogo, mfano mtu anaambiwa akate tiketi kesho aondoke, ukija kuangalia gharama zinakuwa kubwa ukilinganisha na yule aliyekata mwezi mmoja kabla,” alisema Leila.

Kwa mujibu wa Leila idadi ya Watanzania wanaosoma nchini humo ni zaidi ya 4,000 na kwamba hivi sasa wanaendelea kufanya sensa kwa njia ya mtandao kupata idadi kamili.

 “Hii idadi ni kutoka ubalozi wa China katika taarifa zao juu ya wanafunzi waliopo huku kimasomo, ila kwa sisi hapa kwa data zetu bado ‘hatuja-compile’ yote, maana tunafanya ‘online survey’ ya watu wote kwa ‘system’ ambayo imeandaliwa na viongozi.

“Tunafanya viongozi wote wa wanafunzi Watanzania, lengo ya hii ‘survey’ ni kujua watu waliopo China na walioondoka, kujua kama kuna shida yoyote na kufahamu idadi kamili ya Watanzania katika sehemu husika,” alisema Leila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles