23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Corona yakwamisha mradi wa matibabu ya kina ya saratani

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

MRADI wa matibabu ya kina ya ugonjwa wa saratani ulioandaliwa na Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan (AKHST) umeshindwa kuanza kutekelezwa kwa wakati kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Hospitali ya Aga Khan, Olayce Lotha, alisema maandalizi ya awali ya mradi huo yamekamilika.

Alisema tayari maandalizi yote yamekamilika ikiwamo kuajiri watumishi wa kutosha watakaotekeleza mradi huo na kuandaa vifaa tiba vitakavyotumika.

“Programu hii inahusisha watu kukutana jambo ambalo linatutia hofu kutokana na kuwapo kwa mlipuko wa virusi vya corona, tunasubiri hali itakapokuwa shwari tufanye uzinduzi rasmi,” alisema Lotha.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Matibabu ya Saratani ya Hospitali ya Aga Khan, Dk. Harrison Chuwa, alisema mradi huo utatekelezwa katika wilaya 13 za mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza katika kipindi cha miaka minne.

Alisema japokuwa mradi huo utatekelezwa katika mikoa miwili, manufaa yake yatakwenda nchi nzima ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 60 ya Watanzania watafikiwa na kampeni ya uhamasishaji.

“Kwa kutumia kliniki za upimaji zinazotembea, zaidi ya watu milioni 1.7 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa saratani baada ya kusogeza huduma hizo,” alisema Dk. Chuwa.

Alisema hiyo itasaidia kuongeza idadi ya wagonjwa watakaofika hospitalini mapema kwa matibabu kutoka asilimia 20 hadi kufikia asilima 40 na kupunguza idadi ya wagonjwa wa saratani wanaogundulika na hatua za tatu na nne za ugonjwa kuanzia sasa hivi, ni asilimia 75 hadi kufikia nusu yake baada ya kukamilika kwa mradi.

“Mradi huu utaboresha maabara ya MNH kuiwezesha kuwa kitovu cha maabara ya kisasa ya pathiolojia ya molekuli na vinasaba ambayo itahudumia nchi nzima kusaidia madaktari kuchagua aina ya matibabu na dawa sahihi,” alisema Dk. Chuwa.

Aliongeza kuwa mradi huu utaongeza mashine mpya za kisasa za tiba ya mionzi kwa matibabu na hivyo kupunguza mrundikano wa wagonjwa wanaosubiri tiba hiyo.

“Walau vituo 100 vya afya katika ngazi ya jamii vitafikiwa na mradi huo kwa kujengewa uwezo wa kutoa baadhi ya huduma za saratani hususani uchunguzi wa awali.

“Watumishi 330 wa afya watawezeshwa na kusomeshwa kwa nia ya kuongeza ufanisi wa kutoa huduma za matibabu,” alisema Dk. Chuwa.

Aliongeza kuwa kupitia mradi huo utapunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na ugonjwa huo.

Mradi huo unaogharimu Sh bilioni 38 umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na unatarajiwa kutekelezwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Roads (ORCI), AKHD na Hospitali ya Bugando.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles