26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yabadili utaratibu Siku ya Mazingira

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

KUTOKANA na changamoto ya ugonjwa wa corona, Serikali imeamua mwaka huu hapatakuwa na mikusanyiko kwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na badala yake yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari.

Maadhimisho hayo ambayo yalipangwa kufanyika kitaifa mkoani Lindi yanatarajiwa kufanyika Juni 5.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Zungu, alisema kuwa kwa kuwa suala la janga la corona limekuwa ni changamoto kubwa, Serikali imeamua kwamba mwaka huu hakutakuwa na mikusanyiko kwa maadhimisho hayo.

“Kwa muhtadha huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wamekubaliana kuwa maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Mazingira Duniani yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari vilivyopo katika maeneo yao pamoja na mitandao ya kijamii kuelimisha jamii kutunza mazingira,” alisema Zungu. 

Alisema kila mkoa utafanya shughuli za maadhimisho hayo kwa kutumia vyombo vya habari vilivyopo maeneo husika.

“Ni vyema ikafahamika kwamba hifadhi ya mazingira si kazi ya Serikali peke yake, bali ni jukumu letu sote katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kaya. Nitoe wito kwa taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia tusaidiane katika kuhifadhi  mazingira,” alisema Zungu.

Alisema kila mmoja ana wajibu na fursa muhimu katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira hapa nchini.

“Ningependa kusisitiza kuwa tushirikiane katika kufanya juhudi kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchini.

“Kila mwananchi akiwajibika katika nafasi yake, tutalinda mazingira yetu na jamii kwa ujumla.

“Kwa muhtadha huo shughuli za maadhimisho zitalenga kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuwaelimisha jinsi ya kuepuka corona,” alisema Zungu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles