30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 19, 2021

Corona imeathiri uchangiaji damu nchini

Elizabeth Kilindi, Njombe

CHANGAMOTO ya uwapo wa virusi vya corona imeathiri kwa kiasi kikubwa uchangiaji damu Wilaya ya Makete, mkoani Njombe, na kusababisha kutokufikia lengo lililokusudiwa.

Kwa sasa, kiwango cha uchangiaji damu kimepungua kwa sababu wachangiaji wakubwa walikuwa ni wanafunzi wa sekondari na vyuo ambao wamerudi majumbani baada ya masomo kusitishwa kwa lengo la kuepuka msongamano unaoweza kuchangia maambukizi mapya ya virusi hivyo.

Akizungumza na Mtanzania, Mratibu wa Damu Salama Wilaya ya Makete, mkoani Njombe, Sergio Mkwama, anasema ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona umeathiri kwa asilimia 80 suala la uchangiaji damu wilayani humo.

“Hii ni kwa sababu yale maeneo ambayo tulikuwa tunatarajia kwa kiasi kikubwa kukusanya damu au kuhamasisha utoaji wa uchangiaji damu ilikuwa ni sehemu za shule na vyuo mbalimbali,’’ anasema Mkwama.

“Sasa tangu ulipoingia huu ugonjwa hizi sehemu zimefungwa ili kuepuka mikusanyiko. Kwa hiyo, ile nafasi ya kwenda kuwafikia hao wachangiaji damu imekuwa ni ngumu, tunapata changamoto,’’ anasema Mkwama.

Anasema njia wanayotumia kuhamasisha jamii ni kufika katika vituo vya afya ili kuweza kuchangia licha ya kuwa muitiko sio mkubwa kama ilivyokuwa hapo awali.

“Njia ambayo tunahamasishana na jamii ni kufika kwa wataalamu kwenye vituo vya afya, wakifika pale wanaweza wakachangia damu kwa kufuata taratibu zote na Wizara ya Afya au mpango wa taifa wa kuchangia damu sambamba na serikali kufuata taratibu zote na kuchukua tahadhari zote kwa kufuata taratibu zote za uchangiaji damu salama kwa hiyo, watu wasiogope kwamba pengine nikifika kule ndio nitapata ugonjwa,’’ anasema Mkwama.

Anaongeza: “Mchangia damu hawezi kupata ugonjwa wa corona kwa sababu mazingira ni salama na tahadhari zote zinachukuliwa kwa hiyo tunahamasisha wananchi wote kuona umuhimu wa kuchangia damu.

“Tunapambana na corona ndio, lakini upande wa pili tunaathirika, kuna watu watakosa huduma ya damu kwa sababu ili ipatikane inatulazimu kwenda kuwahamasisha watu kuchangia kwa kufuata kundi au taasisi Fulani. Sasa hivi imekuwa ni shida kwa sababu mikusanyiko haipo kwa hiyo tunashindwa kuwapata watu kwa urahisi.’’

Anasema kufuatia hali hiyo imewalazimu kutembea katika taasisi mbalimbali ikiwamo makanisa.

“Huko huwa tunapopata nafasi ya watu zaidi ya watano au watatu, tunatoa elimu ya kuhamasisha juu uchangiaji damu kwa wale wenye nafasi na afya njema wanaweza wakafika hospitalini na kuchangia. Kwa wale ambao hawana nafasi za kufika hospitalini tunafanya mawasiliano na wataalamu wa afya wanafika eneo ulilopo na tunafanya utaratibu wa wao kuchangia damu na zitaweza kufika hospitalini ili kuweza kusaidia watu,’’ anasema Mkwama.

Mkwama anasisitiza kuwa hali ni mbaya kwa sababu wachangiaji damu hawapatikani.

Kwa upande wake Yona Luvanda, anasema elimu ya uchangiaji damu itolewe kwa msisitizo kwa jamii kama ilivyokuwa vyuoni ili kusaidia makundi yenye uhitaji.

“Elimu ya uchangiaji damu ihamie kwa jamii na kampeni hii iwe kama walivyokuwa wakifanya shuleni, jamii itajitokeza watachangia bila ya kujali tatizo hili la corona linalotukabili hivi sasa,’’ anasema Luvanda.

Naye Mery Lwiva, anasema kutokana na uwapo wa virusi vya corona, watu wengi wamekuwa wakijilinda wao na kusahau wajibu wao.

“Tumesahau wajibu wetu wa kuchangia damu, tunapojilinda sisi tukumbuke na makundi ambayo yalikuwa yakitutegemea kwenye suala la damu, tubadilike la sivyo tutasababisha vifo vya wajawazito, watoto wachanga na hata wale wanaopata ajali kutokana na kukosekana kwa damu,’’ anasema Mary.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,848FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles