28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Corona: Biashara Dar-China ngoma nzito

Faraja Masinde -Dar es salaam

WAKATI Balozi wa China nchini, Wang Ke akisema baadhi ya viwanda nchini humo vimeanza kufanya kazi, Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo imesema hali bado ni mbaya, na si rahisi kuagiza mizigo kutoka nchini humo kwa kuwa hata mawakala waliokuwa wakiwatumia waliondoka.

Tangu kuanza kwa virusi vya corona nchini China Desemba mwaka jana, watu walioambukizwa wamefikia 90,870 katika nchi 72 huku vifo vikiwa ni zaidi ya 3,100 hali iliyozua hofu miongoni mwa wafanyabiashara.

Ili kukabiliana na virusi hivyo, nchi mbalimbali zimekuwa zikichukua hatua za kupunguza maambukizi hayo, ikiwamo Italia ambayo imetangaza kufunga shule na vyuo.

Akizungumza jana na waandishi wa habari Dar es Salaam, balozi huyo aliwatoa hofu wafanyabiashara nchini, akisema shughuli za uzalishaji katika taifa hilo lililokumbwa na virusi vya corona mwanzoni mwa mwaka huu zimeanza kurejea.

Balozi Ke alisema soko la Karikoo ni moja ya sehemu ambazo zimekuwa zikitegemewa kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara wa mataifa mbalimbali, hasa ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema pamoja na kuwapo kwa changamoto hiyo ambayo imesababisha shughuli nyingi za kiuchumi kusimama nchini humo, lakini taratibu uzalishaji utarejea kwenye hali yake ya kawaida.

“Ni kweli kwamba changamoto hii ilisababisha mtikisiko wa kiuchumi kutokana na kusimama kwa uzalishaji nchini China, hatua ambayo ilitikisa biashara za miji mingi, ikiwamo Kariakoo, hata hivyo jambo la kushukuru ni kwamba kwa sasa baadhi ya shughuli za uzalishaji ambazo zilikuwa zimesimama nchini China taratibu zinaanza kuendelea.

“Hivyo ni matumaini yetu kuwa hata katika soko kuu la Kariakoo hali itaendelea kuimarika kwani tathmini yetu inaonyesha kuwa kumeanza kuwapo kwa ahueni, pamoja na kwamba uzalishaji bado siyo wa kuridhisha, lakini tunatazamia kuona hali ikiimarika siku hadi siku kwa wafanyabiashara,” alisema Ke.

Alisema kuwa pamoja na virusi hivyo kutikisa uchumi wa China, lakini wanaamini kuwa haitachukua muda mrefu kurudi kwenye hali yake ya kawaida huku akitolea mfano virusi vya sars.

“Kama mtakumbuka mwaka 2003, China ilikumbwa na virusi vya sars vilivyotikisa uchumi wake, lakini baada ya kipindi kifupi uchumi wake ulirejea kwenye hali ya kawaida na pato lake kukua hadi kufikia asilimia 10 hali ambayo iliwezesha nchi kufikia malengo yake.

“Leo ni miaka 17 baadaye China inashikia nafasi ya pili kwa uchumi mkubwa na imara duniani, hata sasa hivi tayari Shirika la fedha la Kimataifa (IMF) limebainisha kuwa uchumi wa China utaimarika kwa mara nyingine tena, hivyo hata sisi tunaamini kuwa tutarejea kwenye kuendelea kuwa injini ya uchumi kwenye mataifa mengi siku si nyingi.

“Hivyo pamoja na kwamba kumekuwa na changamoto kwenye sekta ya utalii na biashara, lakini hali itakuwa njema muda si mrefu, kwani tunaona kuwapo kwa maendeleo makubwa,” alisema Ke.

WAFANYABIASHARA KARIAKOO

Akizungumzia kauli hiyo ya Balozi Ke, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabishara Kariakoo, Abdallah Mwinyi, alisema kauli ya kuwatoa hofu haisaidii kwa sababu kwa sasa hali ya biashara ni mbaya.

“Hata kama ni mimi ningesema tu nawatoa hofu, lakini kiuhalisia hali ni mbaya, mzunguko umesimama, watu wana marejesho benki na kwa sasa watu wanauza bidhaa zile zile za nyuma huku wanalipa kodi, umeme, marejesho ya benki na mengineyo,” alisema Mwinyi.

Kutokana na hilo, alisema Serikali inapaswa kutoa kauli kwa taasisi za fedha, hasa benki ili wafanyabiashara hao wapewe kipindi cha mpito kulipa marejesho.

“Serikali inatakiwa kusema kitu kwenye hizi taasisi za fedha, yaani benki ili wafanyabiashara wapewe kipindi cha mpito kuhusu muda wa marejesho. Tunaiomba Serikali ifanye jambo kwa taasisi hizi za fedha,” alisema Mwinyi.

Alipoulizwa kuhusu namna ya kuagiza bidhaa kupitia wakala alisema; ”Wakati ugonjwa huu unatokea ni kipindi ambacho kilikuwa ni Sikukuu ya Wachina ambapo huwa viwanda vyote vinafungwa na wanapokua wanafunga kunakuwa hakuna mzigo wowote.

“Sasa wakati huo ugonjwa ulipotokea mawakala wote waliondoka,” alisema Mwinyi.

Kuhusu kuagiza bidhaa kupitia wakala wa China, alisema; “Ni vigumu kwa sababu huyo Mchina anapotaka kupakia mizigo kontena haliwezi kujaa kwa sababu mizigo ipo kidogo – hakuna. Pia ukisema tu uagize huko, kuna kutapeliwa, kwa hiyo kwa ujumla hali ni mbaya sana,” alisema Mwinyi.

BALOZI NA WANAFUNZI

Akizungumzia kuhusu wanafunzi 400 wa Kitanzania wanaosoma katika mji wa Huwan, Balozi Ke alisema kuwa wako salama na kwamba wamekuwa kwenye uangalizi wa hali ya juu.

“Jambo hili najua wazazi, ndugu na jamaa watakuwa na hamu ya kutaka kulifahamu, lakini niseme tu kwamba wanafunzi wote wako kwenye uangalizi wa hali ya juu, kwani mbali tu na wale wa Tanzania, wanafunzi kutoka Afrika kwa ujumla wanaangaliwa kwa jicho la karibu na wamekuwa wakipatiwa huduma zote muhimu.

“Na jambo tunaloshukuru ni kwamba hadi sasa hakuna hata mwanafunzi mmoja wa Tanzania ambaye ameweza kushukiwa kwa namna yoyote ile kuwa na virusi vya corona, hivyo wanaendelea na masomo na tumekuwa tukiwapelekea wataalamu mbalimbali wakiwamo wanasaikolojia kwa ajili ya kuwaangalia wakati wote, hivyo wazazi hawapaswi kuwa na wasiwasi juu wa watoto wao,” alisema Ke.

Aidha, alimshukuru Rais Dk. John Magufuli ambaye amekuwa na taifa lao bega kwa bega hata ilipopata changamoto hiyo.

“Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kwenye kutupa pole na kushikamana na sisi, na hata nilipozungumza naye alisema kuwa yupo tayari kutupatia madaktari kwa ajili ya kutusaidia kukabiliana na hili, lakini tukasema hapana kwani kwa sasa tunao madaktari wa kutosha ambao wanakidhi changamoto iliyopo.

“Lakini pia tunashukuru kuona kwamba kwa sasa maambukizi ya virusi yamepungua kwa asilimia 90 ikilinganishwa na wiki chache nyuma,” alisema Ke.

Kwa upande wake, Dk. Ligi Vumilia, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania waliosoma China, alisema kuwa wao wamekuwa wakiwasiliana na wanafunzi wanaosoma huko ambao wanasema kuwa wako salama na kwamba hali inaendelea kuimarika kila kukicha.

“Tunafanya mawasiliano na wenzetu wanaosoma huko na jambo la kushukuru ni kwamba wamedai wako salama na hali inazidi kuimarika kwani maambukizi yamekuwa yakipungua kila kukicha, hivyo wazazi hawapaswi kuwa na wasiwasi,” alisema Dk. Vumilia.

MSIMAMO WA TEC

Katibu Mkuu wa Baraza la Maskofu nchini (TEC), Dk. Charles Kitima alisema furaha yao ni kuona wanaokoa maisha ya watu kwa kuwa lengo la ibada ni kuokoa nafsi na maisha ya watu, hivyo hawawezi kufanya ibada ambayo inahatarisha uhai wa watu.

“Ni jambo zuri kufuata wataalamu kwa sababu lengo ni kuokoa maisha na katika shughuli zote za ibada zinalenga kumfanya mtu awe na maisha mazuri, hivyo hatuwezi kupinga lolote na tunafurahi kupewa maelekezo, tayari tumeelewa na tunaendelea kueleweshwa, na juzi tulikuwa na kikao na tulipewa maelekezo na wizara, kwa hiyo tunashukuru sana kwa maelekezo na lengo ni kuona balaa hili haligusi nchi yetu,” alisema.

Alisema wanaliona tishio hili la virusi vya corona kwa sababu hata kwa China kuna Wakristo wenzao ambao wameathirika na huko Italia pia, hasa katika Jimbo Kuu la Milan kuna Jumapili kama mbili sasa wamesitisha hata ibada za mikusanyiko na wanaendesha ibada kwa mtindo wa tofauti kabisa.

“Huko kuna vitu ambavyo wameambiwa visifanyike na hata mikusanyiko ya watu imedhibitiwa, kuwa wasikusanyike zaidi ya watu kadhaa.

“Tunaona pia hata shule zimefungwa, kwa hiyo tunahitaji kuwa waangalifu sana na kusikiliza wataalamu wanatuambia nini na tuna imani hili tishio litadhibitiwa.

“Lazima sisi tuone huduma za kiroho zinawafikia watu kwa namna gani katika mazingira kama hayo, kwenye nchi yetu hatujapata tatizo hilo, lakini ni lazima tuchukue tahadhari kubwa kwa sababu tuna mwingiliano na nchi mbalimbali ikiwemo China na hatuwezi kukwepa kuingiliana na watu kwa sababu tunategemeana.

“Tanzania inategemea kwa kiwango kikubwa ushirikiano wa kibiashara na China, kwa hiyo hatuwezi kusema hili tatizo halituhusu, linatuhusu sana kwa sababu shughuli zao na zetu zinaendana,” alisema Dk. Kitima.

Alisema TEC kama baraza linalosimamia taasisi ya kidini, wanatambua kuwa wanatakiwa wafuate sheria za nchi, kwa hiyo watafuata maelekezo yote watakayopewa na Wizara ya Afya na vigezo vingine vilivyowekwa na kutoa tahadhari ambazo wataambiwa, hasa katika yale yanayoainishwa kuwa yanaweza kuwaletea watu matatizo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles