31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CONSOLER WILBERT: NILIACHISHWA SHULE NIOZESHWE KISA MWANAMUME ANAMILIKI BAISKELI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


MILA na tamaduni mbaya zimesababisha wanawake wengi kuathiriwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimewasababishia kupata maumivu au athari za kimwili na kisaikolojia.

Suala la mahari ni mojawapo ya tamaduni mbaya ambazo zimegharimu maisha ya watoto na wanawake wengi hivyo kujikuta wakishindwa kufikia ndoto zao.

Mathalani kilio cha ndoa za utotoni kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya kuendelea kukumbatia mila na tamaduni ambazo zimeendelea kuacha madhara ya ukatili kwa wanawake na watoto.

Ingawa baadhi ya jamii zinaendeleza utamaduni huo kwa kufanya mambo kisasa; yaani kumwozesha mtoto akiwa tayari anajitambua ama amehitimu elimu ya juu, hali bado ni mbaya kwa jamii zingine hasa za vijijini.

Baba anaweza kuamua kumkatisha masomo mwanawe kwa sababu ya kutaka ng’ombe ama kumshawishi afanye vibaya katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi ili afeli kisha aolewe.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Consoler Wilbert (34) mkazi wa Tabata Dar es Salaam ambaye alinusurika kuozeshwa akiwa darasa la nne.

Consoler anasema akiwa na miaka 11 shangazi yake aliyekuwa akiishi naye alimshawishi aache shule na kuolewa.

Consoler alitoa ushuhuda huo hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Tunaweza iliyoandaliwa na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) ambayo inalenga kukomesha vitendo vya ukatili kwa wanawake.

 

BAISKELI KAMA KIGEZO

Anasema shangazi yake alimweleza kuwa yeye ni mtoto wa kike hivyo ni lazima aolewe na kwamba alimtafutia mwanamume ambaye alikuwa anamiliki baiskeli.

 “Niliishi katika mazingira ya manyanyaso kwa kupigwa kupita kiasi lakini pia kukosa haki ya kwenda shule. Niliwahi kupigwa kwa kosa dogo nikiwa uchi wa mnyama na nilikuwa nikinyimwa chakula na kuambiwa kwamba sitakiwi kula kama watoto wengine.

“Kuna siku nilipigwa hadi nikaamua kukimbia lakini nilipofika mlangoni nilibanwa na mlango na katika harakati za kutaka kujitoa nilianguka chini. shangazi yangu alikuja akanikanyaga mgongoni na kiatu kirefu.

“Nilipokuwa na miaka 11 shangazi aliniambia si lazima nisome mimi ni mtoto wa kike hivyo amenitafutia mwanamume anauza magazeti na ana baiskeli atanioa,” anasema.

Anasema siku iliyofuata alichukuliwa na kupelekwa katika nyumba iliyokuwa haijakamilika ujenzi wake na kukutanishwa na kijana huyo.

“Nilikuwa nalia nikawa nasema mimi sitaki kuolewa…baadaye yule kaka aliondoka na mimi nikarudi nyumbani. Niliendelea kujitengenezea mazingira magumu zaidi na ilifika wakati nikawa nakosa ada ya shule nikawa naenda mtaani kuomba.

“Nilikuwa napita katika mitaa mbalimbali hasa kule Posta nikiwa nimevaa sare za shule na kuomba msaada, wengine walinipa na wengine waliona kama naigiza. Lakini namshukuru Mungu baadaye nilipata ada na kurudi shuleni,” anasema.

Anasema aliendelea kuishi kwenye mateso makubwa huku akilala katika chumba kidogo cha stoo na kumwagiwa maji ya baridi wakati wa kuamshwa.

“Ilifika wakati jamii ilichoka na kupitia kwao wazazi wangu waliweza kuja kutoka Bukoba, mama alipokuja vikao vya familia vilifanyika na mimi nikaondoka,” anasema.

Hata hivyo, anasema licha ya kuondoka shangazi yake alimfuata tena katika shule aliyokuwa akisoma na kuwaambia walimu wamwadhibu.

“Nilifungiwa kwenye chumba na kupigwa na walimu, nilitoka nikiwa na maumivu makali. Niliamua kutoroka kuelekea Bokoba kwa wazazi wangu,” anasema.

Anasema wakati akiwa njiani kuelekea Bukoba alipofika jijini Mwanza alikutana na baba mmoja ambaye alimuahidi kuwa atamsaidia ili aweze kufika kwa wazazi wake.

“Aliniambia atanipeleka nyumbani kwake nikalale ili kesho yake anikatie tiketi niende Bukoba lakini kumbe alikuwa ni muongo, usiku alinipeleka katika nyumba ya kulala wageni na kutaka kunibaka.

“Aliniambia nisiogope atatumia kondomu. Nililia sana nikamwambia wewe ni zaidi ya baba yangu kwanini unataka kunifanyia hivyo na alipotaka kunikamata kwa nguvu nilipiga kelele akaninyanyua na kufungua mlango kisha kunirusha nje,” anasema.

Anasema baada ya hapo aliomba wasamaria wema wakamsaidia kuweza kufika nyumbani kwao Bukoba na kutokana na maumivu aliyokuwa nayo ya kipigo cha walimu alipelekwa katika Hospitali ya KCMC ambapo alilazwa kwa muda wa miezi sita.

“Sikuweza kutengamaa tena hadi leo kwa sababu kipigo kile kilinisababishia majeraha kichwani, nilifanyiwa upasuaji mkubwa wa mgongo na nilipelekwa India kufanyiwa upasuaji wa kichwa,” anasema.

Anasema baada ya kupata nafuu alirudi kuendelea na masomo huku akiishi Sinza kwa msamaria mwema aliyejitolea kumsaidia.

“Niliendelea kusoma katika mazingira magumu hadi alipomaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Moa ambapo nilifaulu kwa kupata daraja la kwanza.

“Niliwaomba watu wanishauri kozi ya kusoma kwa kuwa nataka kuwasaidia wasichana na waliniambia nisome Sociology hivyo, niliomba nafasi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo nilichaguliwa na kuanza kusoma mwaka 2005,” anasema.

 

AJITOA KUWASAIDIA WASICHANA

Anasema kutokana na matatizo aliyoyapata alijiwekea ahadi ya kuja kuwasaidia wasichana wanaopitia mazingira magumu kama aliyopitia yeye.

Ambapo harakati hizo alianza tangu alipokuwa masomoni UDSM mwaka 2005.

Anasema wakati anaishi Sinza alikuwa akikutana na watoto wenye mazingira magumu na kuwaahidi wamwombee akimaliza masomo atawasaidia.

“Nilipita katika mazingira magumu na nilimuahidi Mungu kama atanisaidia nitayatoa maisha yangu yote kuwahudumia wasichana. Niligundulika kuwa nina tatizo kubwa la kichwa na mgongo na nilitakiwa kusoma kwa muda mfupi tu kwakuwa siwezi ‘ku-concentrate’. Pale chuoni nilipewa chumba katika sehemu ambayo walikuwa wanakaa wanafunzi wenye ulemavu.

“Na kwa sababu nilipata ufadhili wa serikali nilipopata ‘boom’ Sh 360,000 niliamua kutumia kiasi kidogo cha fedha kuanza kusaidia wasichana. Na kutokana na matatizo niliyokuwa nayo niliruhusiwa kuchagua watu wa kukaa nao hivyo nilitafuta wasichana wa kukaa nao.

Anasema alianza kumsaidia msichana wa kwanza mwaka 2005 ambapo alimpeleka kwenda kusoma masomo ya sekondari katika vituo vya QT na hadi anamaliza chuo mwaka 2008 alikuwa akiishi na wasichana watano.

“Waden (Mwangalizi wa wanafunzi) alikuja kugundua akaniita na kunihoji, nilimwambia ukweli kwamba mimi nimemwahidi Mungu kusaidia wasichana, ni kweli hawa si wanachuo lakini nawasaidia wanasoma. Alinielewa na hakunisumbua tena,” anasema.

 

FAMILIA

Anasema alikutana na mumewe mwaka 2003 akiwa kidato cha tano na wakakubaliana akimaliza chuo ndipo waoane.

“Tumekaa kwenye uhusiano kwa muda wa miaka mitano na baada ya kumaliza masomo yangu tulifunga ndoa Julai 2008.

“Najivunia mno mume wangu, nilikuwa siwezi ku–concentrate (kutuliza kichwa) nisome kutokana na matatizo niliyokuwa nayo hivyo, ilibidi Elia (mume wake) aje asome masomo ya Sociology na kunisaidia niweze kuingia darasani kufanya mtihani. Yeye taaluma yake ni mhasibu na wakati mimi nasoma yeye alikuwa ameshamaliza.

“Kwa kawaida mwaka wa pili shule huwa ngumu na unaweza kukosa watu wa kukaa na kusoma nao hivyo nilikuwa nampa vitabu ama vitini anaondoka navyo, anakwenda kutengeneza summary (muhtasari) rahisi kisha anakuja kunielezea halafu mimi nakwenda kufanya mtihani.

Anasema baada ya kuhitimu shahada yake ya kwanza alipata ufadhili kutoka kwa mtu binafsi na kwenda kusoma Shahada ya Uzamili ya Social Work.

“Yule mtu aliguswa na kazi nilizokuwa nafanya na kwa sababu siwezi ku-concentrate ilibidi tena mume wangu aweze kusoma na mimi, alijitoa akasoma na ndiye alikuwa research assistant (mtafiti msaidizi) wangu hadi nilipomaliza na kufanya vizuri.

“Nilimwambia mume wangu hata kama nisome nifike wapi maisha yangu nitayatoa kwa ajili ya wasichana sitajali nalipwa au silipwi. Baada tu ya kutoka kwenye fungate nilikuwa na wasichana saba, watano ni wale niliokuwa nao chuoni na wawili nilikuwa nimewaombea kwa kaka yangu mkubwa,” anasema.

Anasema walipoanza maisha walikuwa na vyumba viwili na aliendelea kuishi na wasichana hao ambapo yeye na mumewe walikuwa wakilala chumbani na wasichana wanalala sebuleni.

“Ile barua niliyomuahidi Mungu ilikuwa kama inanifuata utafikiri labda nimewekewa kibandiko kichwani, wasichana walikuwa wananifuata kokote ninapokuwa. Mwaka 2010 niliamua kushirikisha watu wakiwamo niliosoma nao Mlimani wakanisaidia nikasajili kituo.

Anasema kituo hicho New Hope for Girls hadi sasa kina wasichana 32.

“Mabinti wengi ninaoishi nao ni yatima na wengine familia zao hazina msimamo na hivyo kujikuta mtaani. Nawasaidia mwenyewe bila kupata msaada wa serikali au taasisi za wafadhili.

“Kama nikipata watoto wana shida sana huwa naenda serikali za mitaa ama Manispaa ya Ilala na unaweza kuambiwa serikali haina uwezo, nami huwa siwezi kumuacha mtoto aende huwa namuomba mume wangu nirudi naye na tunaishi nao kama sehemu ya watoto wetu,” anasema.

Kwa mujibu wa Consoler mabinti wote wanasoma kwenye shule za sekondari za serikali na binafsi. 

Consoler anasema kutokana na matatizo aliyopitia hawezi kufanya kazi ngumu hivyo mume wake ndio tegemeo kubwa kwake na kwa mabinti anaowasaidia.

Anasema wamefanikiwa kupata watoto wawili ambapo mmoja ana miaka saba na mwingine ana miaka mitano.

 

KAMPENI YA TUNAWEZA

Kaimu Mkurugenzi wa WLAC, Wigai Kisandu, anasema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha umma kuondoa aina zote za ukatili.

Anasema kampeni hiyo ya miaka mitano inalenga kuleta vuguvugu la watu katika jamii wanaopinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

“Watekelezaji wakuu wa kampeni hii ni watu wanaojulikana kama wanamabadiliko pamoja na asasi rafiki. Mwanamabadiliko ni mtu wa jinsi yoyote ambaye ameweka dhamira kubadili tabia na mienendo yake juu ya ukatili dhidi ya wanawake kisha kushawishi watu wengine 10 au zaidi ili wabadili mienendo na tabia zao dhidi ya ukatili,” anasema Kisandu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles