25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Colombia inaweweseka kwa jinamizi lisilotaka amani

COLOMBIA-FARC-PEACE-DEMO
Waandamanaji wanaounga mkono mkataba wa amani na FARC.

VITA haina macho na inapotokea huwakumba waliosababisha, wasiohusika na hata wasiojua kushika silaha kujitetea kutegemeana na mapigano yalivyo. Ungetarajia kuwa watu walioishi vitani kwa zaidi ya miongo mitano wangechagua amani baada ya kupewa fursa ya kuamua, lakini imekuwa kinyume chake nchini Colombia na kuistaajabisha dunia kutokana na wananchi wa taifa hilo kupiga kura ya maoni kukataa mapendekezo ya mkataba wa amani na waasi wapiganaji wa msituni wa FARC, mchakato uliohangaikiwa kwa muda mrefu na Rais wa taifa hilo Juan Manuel Santos aliyezawadiwa tuzo ya amani ya Nobel siku sita zilizopita kwa juhudi zake za kumaliza mgogoro sugu unaoikabili nchi yake.

Tangu aingie madarakani miaka sita iliyopita Rais Santos amefanya juhudi kubwa kumaliza vita na kundi la FARC lililoanzisha mapigano mwaka 1964, hatimaye rasimu ya mkataba ikakamilika mnamo mwezi Agosti lakini katika kura ya maoni siku tano kabla Rais Santos kupata tuzo ya Nobel asilimia 50.2 walipiga kura kukataa mpango huo wa amani dhidi ya asilimia 49.8 walioafiki.  Uhondo wa kutuzwa Rais Manuel ukapungua na kugeuka kuwa ushiriki tu na si ushindi ingawa imechagiza kuanzishwa juhudi za kuokoa mkakati huo wa amani ili Colombia isitumbukie tena katika vita ya wenyewe.

Waliokataa mpango huo wa amani wana sababu zao lakini madhara ya mapigano hayo ni makubwa kwani takribani watu 220,000 wameuawa, wengine milioni sita wakigeuka wakimbizi wa ndani kundi la FARC liliposhambulia vituo vya polisi, kambi za jeshi, kuteka nyara ndege na kufanya mauaji ya kutisha sanjari na kuharibu miundombinu ya mafuta na madaraja muhimu yanayounganisha nchi. Kwa ujumla waliojitokeza kushiriki kura ya maoni walikuwa pungufu kwa asilimia 38 ikimaanisha kuwa mpango huo ulishashindwa mapema, kwani wengi walishaupuuza ingawa awali kulikuwa na matumaini makubwa ya kukubaliwa hususani serikali ilipoandaa hafla kubwa ya utiaji saini mkataba huo ikiwaalika viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani kushuhudia.

Matumaini hayakutimia kutokana na mgawanyiko wa hisia miongoni mwa Wanacolombia, wengi wa waliokubali mpango huo wanaishi katika maeneo yaliyoathirika zaidi na mapigano hayo ambao hawajaisamehe FARC lakini wamechoshwa na athari za mapigano, huku waliokataa wakiishi katika maeneo ambayo hayakuathirika hivyo hawajaonja athari halisi za mapigano hayo. Waathirika wakubwa wa mapigano hayo ni raia wakiwamo watoto waliouawa zaidi na mabomu yaliyotegwa na kundi hilo, wengine wakitekwa na kuachiwa baada ya kulipwa kiasi kikubwa cha fedha na kuingizwa katika vikosi vya wapambanaji na kunyanyaswa kijinsia. Hivyo ndivyo FARC ilivyoendesha mapigano ingawa kwa takriban miaka 15 iliyopita imepungua sana nguvu kutoka kuwa na wapiganaji 20,000 hadi 6000, kutokana na mkakati mahsusi wa kuliangamiza kundi hilo kwa msaada wa Marekani iliyoipa Serikali ya Colombia fedha nyingi kugharamia vita dhidi ya kundi hilo na makundi mengine ya kigaidi.

Licha ya kupungua nguvu lakini FARC iliendeleza harakati zake na makubaliano ya amani yalitarajiwa kumaliza mapigano yaliyoonekana kutomalizika, ambapo chini ya makubaliano hayo wapiganaji wa kundi hilo wanatakiwa kusalimisha silaha kwa wakaguzi wa UN na FARC kiwe chama cha siasa kikihakikishiwa viti kumi katika Bunge la nchi hiyo kwenye uchaguzi wa mwaka 2018 na 2022.

Katika miaka ya hivi karibuni kundi hilo limepoteza vinara wake waliouawa katika mapigano na wengine kufariki dunia kwa sababu za kawaida, hivyo Rais Santos alipoanzisha mchakato wa amani FARC waliukumbatia kwa haraka hadi kufikia utiaji saini uliofanywa na kiongozi wao Rodrigo Londoño Echeverri ‘Timochenko’ na Rais Santos. Lakini kinachosababisha kukataliwa kwa mpango huo wa amani ni msamaha kwa waasi hao ikiwa watatubu uhalifu walioufanya, wakitakiwa kufukua mabomu waliyoyatega ardhini, kukarabati majengo waliyoyaharibu na kuwasaidia walioathirika na mapigano huku Serikali ikitakiwa kutenga fedha za kutosha kuboresha huduma za kijamii katika maeneo yaliyoathirika.

Kinachowakera wananchi wa Colombia akiwamo mtangulizi wa Rais Santos, Rais mstaafu Alvaro Uribe, ambaye aliimarisha mapigano yaliyodhoofisha kundi hilo na kusababisha likubali mchakato wa amani ni FARC kulegezewa kamba kwa maovu iliyoyafanya. Uribe na wafuasi wake wanadai hawapingi mpango wa amani lakini wanataka makubaliano hayo yatathiminiwe upya, ili wenye hatia wasiruhusiwe kugombea nafasi za uongozi wa siasa na wauaji wafungwe ikiwamo kuilazimisha FARC kuwalipa fidia iliowaathiri.

Fuerzas Armadas Revolucionarias de Colombia (FARC) ni kundi lenye mrengo wa philosofia za ki-Marxist lililoanzishwa ili kutetea maslahi ya wanyonge, dhidi ya mabwanyenye ambao nao waliunda vikundi vya wanamgambo ili kujilinda dhidi ya kundi hilo, hivyo kuchochea mgogoro uliobadilika vita vya wenyewe kila upande ukijigharamia kwa kutumia vyanzo tofauti, FARC wakitegemea zaidi biashara ya dawa za kulevya na wanamgambo wa mabwanyenye wakitegemea utajiri waliomiliki. Ni suala la muda ili mkanganyiko huu utanzuliwe huku dunia ikitazama kwa makini kama Colombia itarudi kwenye mapigano au itang’ang’ania amani inayoning’inia kwa uzi kutokana na kukataliwa na wananchi, ingawa kwa sasa hata kundi la FARC linahitaji zaidi usitishwaji wa mapigano kutokana na hali yake ilivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles