31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CODEINE: DAWA TAMU YA KUTIBU KIFUA ILIYOGEUZWA ‘COCAINE’

KATIKA majiji kadhaa makubwa ya Nigeria, vijana wengi wadogo wameathirika na dawa haramu za kulevya.

Lakini katika miaka ya karibuni, aina ya dawa jamii ya Opioid kwa ajili ya kutibu kifua au kikohozi iyoitwa Codeine ndiyo mchawi mkubwa.

Kupitia kipindi kilichopewa jina la ‘In Sweet Sweet Codeine,’ waandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwa siri walichukua picha za video za kampuni kubwa za dawa zikitoa ofa ya kuuza maelfu ya chupa za dawa hiyo ya Codeine bila maagizo ya daktari.

Kujihusisha kwa kampuni hizi, ambazo zinazalisha dawa ya kifua nchini humo kunasaidia kueleza ukubwa wa tatizo linalotokana na upatikanaji rahisi wa dawa hizo licha ya serikali kupiga marufuku mauzo yasiyozingatia taratibu za sheria.

Kipindi hicho ni cha kwanza kwa BBC-Africa Eye, runinga mpya ya uchunguzi ambayo ni kiashiria cha karibuni cha kuenea kwa BBC barani Afrika.

Wakati watengenezaji wa dawa kisheria wakitakiwa kusambaza katika maduka ya dawa, ambayo ndiyo yanawajibika kuuza kwa wagonjwa walioandikiwa na daktari, wafanyakazi wala rushwa wanachukua fursa ya mahitaji makubwa katika soko jeusi na kuendesha biashara haramu ya magendo.

Kufuatia uchunguzi wa BBC, Emzor Pharmaceuticals, moja ya kampuni kubwa kabisa Nigeria imesitisha usambazaji wa dawa ya Codeine.

Imekuja baada ya mmoja wa watendaji wa Emzor kuchukuliwa kwa siri na video akifanya biashara haramu ya chupa za dawa ya kifua.

Mkurugenzi huyo, ambaye ametimuliwa alinaswa katika kanda ya video akijigamba kuwa anaweza kuuza maboksi milioni moja ya chupa za codeine kwa wiki moja katika soko haramu.

Wizara ya Afya Nigeria pia imetangaza kupiga marufuku uagizaji na uzalishaji wa dawa hiyo ya kikohozi ya Codeine.

Matumizi ya kupindukia ya dawa hiyo yana madhara mabaya kwa ubongo na husababisha mtu kurukwa na akili au kuugua matatizo ya akili.

Soko kuu la biashara haramu ya Codeine kwa kawaida ni vijana wadogo na wakubwa wanaotafuta mihadarati ya bei rahisi kwa ajili ya kuwalewesha. Kwa bei ya Naira 1,000 sawa na Sh 7,000 unaipata kirahisi.

Pamoja na kwamba ni kosa kuuza Codeine bila kibali cha daktari, dawa hiyo imebakia kupatikana kwa urahisi.

Ni kawaida kuzikuta zikitumika kama kawaida, wakati mwingine kama sehemu ya mseto katika baa na au sherehe.

Matumizi ya Codeine yamekuwa kitu cha kawaida kama utamaduni wa pop unavyoonekana kuyachochea hasa katika mapigo yanayotesa sasa ya Afrobeats.

‘Diet’, wimbo wa mahadhi ya Afrobeats unaonesha athari za Codeine, mtunzi akionesha namna asivyoweza kufanya chochote bila Codeine, kiasi kwamba akifariki dunia watu wasishangae kuwa Codeine ndiyo iliyomuua.

Wimbo huo ‘mlo wa Codeine’ umekuwa ukitamba mno hasa kupitia nyota watatu wa muziki wa pop wa Nigeria huku mwingine uliotungwa na Olamide ukipigwa marufuku na waratibu wa vyombo vya habari nchini Nigeria.

Nchini Marekani, neno ‘Codeine’ linatamba katika moja ya vibao vya wanamuziki wa Marekani akiwamo rappa Lil’ Wayne, ambaye kigongo chake kinahamasisha matumizi ya Codeine.

Maelfu ya vijana wa Nigeria walio tayari katika urabu, wapo hatarini kuathirika na madhara ya jamii ya dawa za Opioid kuanzia maradhi ya akili hadi viungo vya ndani kama figo kufa.

Tatizo limekithiri zaidi katika sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mwa Nigeria ambako mamilioni ya vijana hawana ajira.

Kuenea kwake eneo hilo pia kunatokana na ukweli kwamba vileo kama pombe vimepigwa marufuku katika majimbo mengi ya kaskazini kutokana na sababu za kidini.

Kwa sababu hizo, vijana wengi wakubwa kwa wadogo, ambao wamekaa vijiweni tu na kuathirika kisaikolojia kutokana na umsikini na kukosa ajira wanageukia njia mbadala-dawa zinazolenga kutibu maradhi lakini zinazoweza kulevya zikitumika vibaya.

Dawa tamu ya kifua ya Codeine imekuwa kimbilio kubwa zaidi, huku wale wasioweza kuhimili bei yake wakigeukia njia mbaya zaidi ikiwamo kinyesi cha mjusi na buibui.

Isa Mohammed, mfamasia mkazi wa jimbo la Kano anasema ongezeko la uraibu wa dawa za kulevya kaskazini mwa Nigeria unatokana na urahisi wa upatikanaji na usambazaji.

Oktoba mwaka jana, Baraza la Seneti la Nigeria lilisema chupa milioni tatu za Codeine hutumiwa kila siku katika majimbo mawili pekee ya kaskazini mwa nchi.

Katika hatua za kukabiliana na tatizo hilo, mwezi uliopita, shirika la kupambana na mihadarati lilikamata roli lililojaa chupa 24,000 za Codeine katika tukio moja tu.

Athari za upatikanaji wa Opioid rahisi kwa vijana hususani Waislamu umetokana na umasikini na ukosefu wa ajira, Mohammed anasema na kuongeza: “Hakika ni janga.”

Serikali ya Nigeria haikuja na matokeo mazuri katika kukabili tatizo hilo.

Marufuku dhidi ya mauzo yasiyo halali hayakuleta matokeo chanya kutokana na uzalishaji kutoratibiwa huku wanufaika wa biashara ya magendo wakihakikisha dawa zinaendelea kupatikana.

Haitarajii marufuku ya mauzo bila kibali cha daktari kusimamiwa vyema katika maelfu ya maduka ya dawa yaliyotapakaa kote nchini humo.

Serikali imekuwa nzito kuchukua hatua hadi BBC ilipoibua suala hilo na hivyo kupiga marufuku, ikidai imechukua hatua hiyo bila kusukumwa na BBC.

Ukweli ni kwamba, kabla ya BBC, Januari mwaka huu kamati iliundwa kuangalia tatizo la uraibu wa Codeine, lakini matokeo na mapendekezo, yaliyotarajiwa baadaye wiki sita hayajachapishwa na wizara ya afya hadi leo hii.

Katika mipaka ya Nigeria, mataifa jirani pia yanakabiliwa na tatizo kama hilo huku dawa ya kupunguza maumivu ya Tramadol ikitumika zaidi nchini Benin kutokana na urahisi wake wa kupatikana na bei.

Benin, ambayo inapakana na Nigeria upande wa magharibi, ni soko kubwa la pili kwa dawa za Tramadol kutoka India. Baadhi ya nchi zilizoathirika zaidi Afrika Magharibi bado hazijaweza kukabili tatizo la uraibu wa Opioid.

Makundi ya ushawishi ya ndani yamependekeza uratibu wa karibu wa uzalishaji na usambazaji wa dawa kuwa ndiyo suluhu bora ya tatizo la uraibu wa Opioid.

Adeyemi Oluwatosin, mhariri mkuu wa jarida la Jumuiya ya Wafamasia Nigeria, anasema moja ya njia za kufanya hivyo ni hatimaye kuasili mwongozo wa taifa wa usambazaji wa dawa— sera ya kuratibu usambazaji wa dawa na kukomesha masoko ya wazi pamoja na dawa feki.

Miaka mitano sasa tangu kupendekezwa kwa mara ya kwanza hata hivyo, sera hiyo imebakia bila kutekelezwa.

Kwa Mohammed, kupiga marufuku moja kwa moja pekee si suluhu la kudumu iwapo Serikali haitachukua hatua zaidi za kuratibu.

Waraibu, anasema wana uhakika wa kugeukia dawa nyingine, baadhi zikiwa na madhara mabaya zaidi.

“Kupiga marufuku Codeine si hoja, uratibu wa dawa ndicho tunachohitaji. Iwapo hatusimamii, tunapoteza muda tu na watu wataendelea kuharibika na kufa,” anasema.

Mbali ya mataifa ya Magharibi, nchini Kenya hususan katika eneo la kaskazini mashariki Serikali tayari imetoa onyo kuhusu matumizi mabaya ya dawa ya Codeini.

Kwa sasa Kenya imepiga marufuku uuzaji wa dawa hiyo baada ya utafiti uliyofanywa na bodi ya kudhibiti uzajiwa wa dawa nchini Kenya kubaini dawa hiyo inatumiwa vibaya.

Dk. Anthony Martin Kiprotich, Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Kimataifa katika bodi hiyo anasema:“Matumizi ya dawa hiyo yaliongezeka mwaka jana kwa zaidi ya asilimia 100 na kutokana na ripoti ya utafiti tumesitisha matumizi yake kwa sababu dawa hiyo ilikuwa inauzwa kwa urahisi madukani bila ya maagizo ya daktari.”

Na katika baadhi ya visa imegunduka kwamba raia huzitumia dawa hizo wakati wa kutafuna majani ya miraa, kama kiburudisho au kileo.

Dk. Anthony Toroitich, anaeleza kwamba kiwango cha mililita 171 000 za dawa zilizo na Codeini ziliuzwa nchini katika muda wa miezi 11.

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles