24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Claudio Ranieri tumaini jipya kwa Fulham FC

NA BADI MCHOMOLOMICHEZO 12 ya michuano ya Ligi Kuu nchini England ambayo imepigwa hadi sasa tangu msimu uanze, imepoteza matumaini ya timu ya Fulham kuendelea na Ligi hiyo msimu ujao kutokana na matokeo waliyoyapata.

Klabu hiyo ambayo imepanda daraja msimu huu, inaonekana kuwa dhaifu kwa kiasi kikubwa huku ikishika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi tano baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoa sare michezo miwili na kufungwa michezo tisa.

Mashabiki wa Fulham walikuwa na furaha kubwa kuona timu hiyo inashiriki Kuu, lakini matumaini ya furaha zao yamepotea kabisa kwa kuwa hawana imani kama timu hiyo inaweza kubaki kwenye Ligi msimu ujao.

Ushindani wa Ligi Kuu ni mkubwa sana, timu zimefanya usajili wa hali ya juu pia zina makocha ambao wana uzoefu mkubwa wa michuano hiyo. Katika kipindi hicho chote tangu msimu kuanza, Fulham FC walikuwa wanamtumia kocha wao Slavisa Jokanovic raia wa nchini Serbia.

Kocha huyo hakuwa na jina kubwa japokuwa alipambana hadi kuhakikisha wanapanda daraja. Timu zenye majina ambazo aliwahi kuzifundisha ni pamoja na Watford na Maccabi Tel Aviv.

Wiki iliopita Fulham walishindwa kuzuia hisia zao, waliamua kumfungashia virago kocha huyo kutokana na matokeo mabaya waliyokuwa wanayapata, hivyo walimtangaza kocha mpya Claudio Ranieri.

Ranieri kwa sasa ni tumaini jipya kwa Fulham, amekubali kubeba msalaba alioushindwa Slavisa Jokanovic, hivyo ana kazi kubwa ya kulinda heshima yake na kuweka historia mpya.

Tayari kocha huyo ana jina kubwa duniani kutokana na kuzifundisha klabu mbalimbali ambazo zinafanya vizuri barani Ulaya kama vile, Napoli, Valencia, Chelsea, Atletico Madrid, Juventus, Inter Milan, AS Roma, Leicester City na zingine nyingi.

Historia kubwa kocha huyo aliiweka msimu wa 2015-16 baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini England akiwa na Leicester City, Je ataweza kuweka historia mpya akiwa na Fulham? Hivi ni baadhi ya vitu ambavyo akivifanya anaweza kufanikiwa.

Kuboresha safu ya ulinzi

Moja ya sababu ambayo inawafanya Fulham kushika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi ni pamoja na ubovu wa safu yao ya ulinzi. Hadi sasa inaongoza kwa kufungwa mabao mengi huku ikiwa imeruhusu mabao 31 na kuwa klabu inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi ndani ya msimamo huo.

Hata hivyo Ranieri tayari ameliona hilo mara baada ya kusaini mkataba wa kuisimamia timu hiyo, hivyo ameanza kuonesha nia ya kutaka kumsajili beki wa kati wa Liverpool, Joel Matip raia wa nchini Cameroon.

Mlinda mlango

Fulham ilifanya usajili wa walinda mlango wawili wakati wa majira ya joto mwaka huu ambao ni Marcus Bettinelli pamoja na Sergio Rico aliyosajiliwa kwa mkopo kutoka Sevilla, lakini inadaiwa hadi sasa haijulikani nani kipa namba moja.

Kama Ranieri atafanikiwa katika suala la beki wa kati, basi lazima apambane kuhakikisha anapata kipa namba moja.

Kumsaidia Ryan Sessegnon

Mmoja kati ya nyota tegemeo wa Fulham ni pamoja na Ryan Sessegnon ambaye amekuwa na mchango mkubwa tangu timu hiyo ikiwa inashiriki Ligi daraja la kwanza, lakini tangu washiriki Ligi Kuu anaonekana kukutana na ushindani wa hali ya juu hivyo kushindwa kuonesha ubora wake.

Mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alitajwa kuwa mchezaji bora wa Ligi daraja la kwanza, amekuwa akifananishwa na nyota wa Real Madrid, Gareth Bale kwa kuanza kucheza beki wa pembeni hadi mshambuliaji.

Mbali na kucheza beki wa kushoto, lakini amekuwa na uwezo mkubwa wa kupachika mabao akiwa anacheza nafasi ya ushambuliaji, hivyo kazi ya Ranieri ni kuhakikisha ananunua mchezaji mwingine ambaye ataweza kucheza nafasi hiyo ya ulinzi ili kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 akasogezwa mbele kwa ajili ya kutafuta matokeo.

Awaamini wachezaji

Ukweli ni kwamba Fulham ni moja kati ya klabu ambazo zimetumia kiasi kikubwa cha fedha wakati wa usajili wa kiangazi, imetumia jumla ya pauni milioni 100 kwa ajili ya kuongeza nguvu.

Hivyo, kitu kikubwa ambacho Ranieri anatakiwa kukifanya ni kuwafanya wachezaji wake wawe na umoja pia anatakiwa kuwaamini huku akiwapa moja ya kuwa wanaweza kufanya mageuzi makubwa kwenye soka.

Historia kubwa ambayo aliiandika akiwa na Leicester City, ilitokana na kuwafanya wachezaji wake kuwa wanatosha kufanya mapinduzi katika soka, aliweza kuwatengenezea umoja, kujiamini pamoja na ushirikiano.

Kwa kufanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kocha huyo kuweza kujitengenezea jina kubwa kwa kipindi kifupi kijacho.

Wanachokiangalia Fulham kwa sasa ni kuhakikisha wanabaki kwenye michuano ya Ligi Kuu England na sio kushuka daraja, kwa hali hiyo Ranieri akifanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuiona timu hiyo ikifanya vizuri katika baadhi ya michezo ya hivi karibuni na kusalia kwenye mchuano ya Ligi Kuu msimu ujao.

Mtihani wa kwanza kwa Ranieri ni Jumamosi hii katika mchezo dhidi ya Southampton nyumbani, kabla ya Desemba 2, kupambana na Chelsea ugenini, huku Desemba 5 akipambana dhidi ya timu yake ya zamani Leicester City na Desemba 8 kucheza dhidi ya Man United kabla ya West Ham, Desemba 15.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles