LONDON, ENGLAND
HATIMAYE uongozi wa klabu ya Fulham umethibitisha kumfukuza kocha wao, Claudio Ranieri, baada ya kuisimamia timu hiyo kwa michezo 17 tangu apewe jukumu la kuinoa kwenye viwanja vya Craven Cottage.
Hatua ya kocha huyo kufukuzwa imekuja mara baada ya Jumatano wiki hii kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Southampton na kuifanya timu hiyo ishike nafasi ya 19 katika msimamo wa ligi England ambapo ni nafasi ya pili kutoka chini.
Matokeo hayo yanawafanya wawe kwenye hatari ya kushuka daraja huku ikiwa imesalia michezo 10 kumalizika kwa ligi. Uongozi wa timu hiyo umelitangaza jina la Scott Parker kuwa kocha wa muda.
Ranieri amekuwa kocha wa Fulham kwa siku 106 na kumfanya awe miongoni mwa makocha saba ambao wamekaa kwa muda mfupi kwenye klabu kabla ya kufukuzwa.
Mmiliki wa klabu hiyo, Shahid Khan, ameweka wazi kuwa wameamua kumfukuza kocha huyo kutokana na kushindwa kufanya kile walichokubaliana kwenye mikataba yao.
“Mipango ya Claudio ndani ya Fulham haijaenda kama tulivyokubaliana na vile tulivyotegemea mara baada ya kumchagua kuwa kocha wetu Novemba mwaka jana, lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kumtupia lawama kwa nafasi tuliopo kwa sasa.
“Claudio amefanya kazi kwenye mazingira magumu, lakini aliweza kuipigania timu kwa michezo hiyo ambayo aliisimamia.
Kutokana na hali hiyo, hatukuweza kuvumilia kwa matokeo ambayo tulikuwa tunayapata, lakini tunaheshimu kwa jitihada zake, ameondoka Fulham huku akiwa bado ni rafiki yetu na tunaamini ataendelea kuwa mmoja kati ya watu wenye mafanikio,” alisema Khan.
Ranieri alikuwa mmoja kati ya makocha ambao wameweka historia katika Ligi ya England baada ya kuwapa ubingwa wa michuano hiyo klabu ya Leicester City msimu wa 2015/2016. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 67, alipewa jukumu la kuifundisha Fulham kuchukua nafasi ya Slavisa Jokanovic.