Na MOHAMED KASSARA
-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Azam FC umesema umemwachia kocha wao, Aristica Cioaba, kuamua hatima ya kiungo wao Ramadhani Singano ‘Messi’.
Singano amerejea nchini baada ya mpango wake wa kusajiliwa katika klabu ya Jadid kukwama kutokana na kile kilichodaiwa tamaa ya wakala wake.
Kwa mujibu wa kaka wa Singano, Hamis Abdalah, klabu aya Jadid ilisitisha mpango wa kumsajili kiungo huyo baada ya wakala wake kutaka malipo zaidi ya dola 50,000 tofauti ya dola 165,000 ambazo pande hizo mbili zilikubaliana awali.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffari Iddy, alisema wameliacha suala la mchezaji huyo kwa kocha wao ambaye ataamua kama waambatane naye katika safari ya Uganda au wamtose.
“Tunatarajia kupeleka kikosi chote, kuhusu suala la Singano kocha ndiye ataamua kama atamjumuisha au la, lakini bado ni mali ya Azam.
Kimsingi Morocco alienda kwa baraka zote kutoka kwetu, hivyo hata alivyorudi bado ataendelea kuwa mchezaji wetu, labda kocha aamue vinginevyo,” alisema.
Azam inatarajia kuondoka nchini kesho kwenda Uganda ambako itacheza mechi nne ya kirafiki dhidi ya timu za URA, SC villa, Vippers na KCCA.