29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

CHUZ ATOA SIRI RUSHWA YA NGONO KATIKA SANAA

Na KYALAA  SEHEYE


WASICHANA wengi wamekuwa wakikumbwa na tatizo la kuombwa rushwa ya ngono ili kupata nafasi kwenye sehemu wanazotaka kufanya kazi.

Mabosi wengi wamekuwa wakitumia njia hiyo ili kuwapatia ajira mabinti na imezoeleka kuwa ili kumpatia kazi au nafasi fulani kwenye jamii kwa mtoto wa kike basi ni sharti atoe rushwa ya ngono. Hata hivyo tabia hii inakemewa vikali na Serikali ambapo watu mbalimbali wamekuwa wakifikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kukomesha hali hii.

Katika tasnia ya filamu, tamthilia na maigizo hali ni mbaya kwani wasichana wanaotaka umaarufu wamekuwa wakitumia miili yao ili kupata nafasi za kufanya kazi hizo ili kuwa maarufu kwenye jamii.

Mmoja wa waongozaji wakongwe wa filamu nchini ambaye pia amewahi kukumbwa na kashfa hiyo, Tuesday Kihangala maarufu kwa jina la ‘Mr. Chuz’ ameliambia MTANZANIA kuwa waandaaji na waongozaji ndiyo wanaolaumiwa kwa jambo hilo wakati ukweli ni kwamba mabinti wenyewe ndiyo hulazimisha kufanyiwa hivyo wakiamini kuwa watatoka na kuwa maarufu nchini.

“Hali sasa hivi ni tofauti, mabinti wengi wanahitaji kuigia katika tasnia hivyo wamekuwa wakishindana kwa kutulazimisha waongozaji kufanya nao ngono na kuwapa nafasi hata kama hana vigezo.

“Ukiwaona wasichana hao ni warembo lakini hawawezi kazi,” anasema Chuz.

Anasema hali hiyo inawafanya wafanye kazi katika mazingira magumu kwani msichana anapoona hajapata nafasi aliyoitaka ili aweze kupata umaarufu ndiyo anaanza kutangaza kuwa aliombwa rushwa ya ngono akakataa ndiyo maana hukupata nafasi.

“Kwa mfano sasa hivi mimi nina skendo ya aina hiyo, kila mtu anaamini kuwa ndio tabia yangu wakati si kweli.

“Kashfa hii nimeipata baada ya kuwafukuza baadhi ya wasichana walioonesha utovu wa nidhamu wakati tuko kambini. “Walinishawishi kutembea nao ili niwape nafasi, wakaamini kuwa nitafanya hivyo lakini sivyo. Mimi huwa uwezo wamtu na si vinginevyo, walinishawishi nikashawishika lakini lilipokuja suala la kazi nikaangalia uwezo ambapo wao hawakuwa nao,” anasema Chuz.

Chuz anawashauri wasichana wanaotaka kuingia kwenye sanaa kuacha kutoa rushwa ya ngono ili waweze kufanikiwa, badala yake waongeze juhudi katika kazi ili wafanikiwe.

Anasema kuwa kama waliotangulia walitoa rushwa na kufanikiwa basi suala hilo kwa sasa halipo.

“Nawashauri wadogo zangu na watoto wangu wa kike wanaoingia katika hii tasnia waache kufikiria kutoa rushwa ya ngono kwa waongozaji na waandaaji ndiyo kutawatoa, kazi bora ndiyo itakayowafikisha wanapotaka kufika.

“Wasichana wengi walioingia kwa rushwa ya namna yoyote ile wameshindwa kudumu hadi leo hii na ndio waliochangia kuifikisha tasnia hapa ilipo,” anasema.

Anasema waandaaji na waongozaji wa filamu wamejipanga kukomesha tabia hiyo mbaya inayorudisha nyuma maendeleo ya kuboresha filamu nchini.

“Chama cha Waongozaji na Waandaaji wa kazi za sanaa tumepanga kukomesha tabia hii na mara moja hatua zitaanza kuchukuliwa, kwani sisi ndiyo tunaonekana chanzo cha tabia hii wakati si kweli,” anasema Chuz huku akitoa mfano kwamba asingekuwa na ushahidi wa kulazimishwa kufanya ngono na wadada wanaohitaji kutoka angezidi kuchafuliwa jina lake.

MWISHO.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles