29.9 C
Dar es Salaam
Saturday, September 28, 2024

Contact us: [email protected]

Chuo cha Ustawi wa Jamii na mkakati wa kumaliza ukatili dhidi ya watoto

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Programu mpya ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto iliyoanza kutolewa na Chuo cha Ustawi wa Jamii itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, imeelezwa.

Programu hiyo inatolewa katika ngazi ya cheti cha msingi na stashahada katika Kampasi ya Kisangara iliyopo Mwanga mkoani Kilimanjaro ambayo ni maalumu kutoa mafunzo ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto.

Akizungumza Julai 8,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Mkuu wa chuo hicho,, Dk. Joyce Nyoni, amesema programu hiyo imeanza mwaka 2023 na mwitikio umekuwa mkubwa.

“Kozi hii inawaandaa wakufunzi wa kufundisha walezi wanaokwenda kulea watoto kwenye vituo vya ‘day care’, shule za watoto wadogo na wataalam wa malezi ya watoto, tunafundisha vitu vingi mfano; maendeleo ya michezo kwa sababu mtoto ni lazima acheze hivyo, tunafundisha mtoto acheze vipi kulingana na umri wake. Tunandisha kuhusu ulinzi wa mtoto kwa sababu ukatili umekuwa mwingi, mtoto analindwaje na vitu gani ni hatari zaidi kwa ukuaji wa mtoto,” amesema Nyoni.

Mkuu huyo wa chuo amesema miongoni mwa mambo yanayofundishwa ni uongozi katika vituo vya malezi na makuzi ya awali ya mtoto, maendeleo ya kimichezo ya mtoto, usalama na ulinzi wa mtoto, sanaa ya ubunifu katika malezi na makuzi ya awali ya mtoto, mbinu za malezi, utoaji wa huduma ya kwanza katika malezi na makuzi ya awali ya mtoto na saikolojia ya mtoto.

Aidha amesema wameweka mikakati ya kuitangaza zaidi programu hiyo ili iweze kufahamika na kutoa wito kwa jamii wakiwemo wamiliki wa vituo vya kulea watoto kujitokeza kusoma.

“Ukatili kwa watoto umeongezeka na watu wengi wanaolea watoto kwenye vituo hawana ujuzi, hawajui haki za watoto, michezo ya watoto hivyo, lazima wabadilike,” amesema.

Amesema katika maonesho hayo wanatoa elimu kwa umma kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo pamoja na kufanya udahili na kuwaasa Watanzania kutembelea banda la chuo hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles