NA UPENDO MOSHA – MOSHI
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Moshi (MUWSA), imekata maji katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi (CCP), kutokana na malimbikizo ya deni la maji la Sh milioni 523.
Meneja Biashara wa (MUWSA), John Ndetico, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa na kuongeza kuwa, mamlaka hiyo inadai zaidi ya Sh bilioni 2.2 kutoka katika taasisi hizo za Serikali na taasisi binafsi.
Alisema mamalaka hiyo imezikatia huduma taasisi hizo tatu za umma kutokana na kuwa wadaiwa sugu, kwani zimeshindwa kulipa deni la Sh 1,339,061,081 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa hivi karibuni juu ya taasisi za serikali zinazodaiwa bili za maji kusitishiwa huduma hizo mara moja hadi walipe madeni yao.
“Mpaka sasa zoezi la kuzikatia maji taasisi za Serikali ambazo ni wadaiwa sugu linaendelea na tumeshawakatia huduma , ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ambao wanadaiwa zaidi ya Sh milioni 785, Hospitali ya Mawenzi zaidi ya Sh milioni 65 na CCP zaidi ya Sh milioni 523,” alisema.
Alisema kabla ya kuzikatia huduma taasisi hizo mamlaka hiyo iliziandikia barua za kuwataka kulipa deni hilo kwa hiyari kabla ya Julai 24 mwaka huu, kwani taasisi za umma ndio zinazo ongoza kwa kuwa wadaiwa sugu kwa asimilia 77.
Raisi watawalipia. Msiwe na Wasiwasi.