Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital
CHUO cha Diplomasia Tanzania, kimetakiwa kuzingatia utoaji wa elimu bora yenye kukidhi mahiaji ya dunia kwa maslahi mapana ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo Desemba Mosi, jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola katika mahafari ya 24 ya chuo hicho.
Amesema utoaji wa mafunzo bora kwa wanadiplomasia kutasaidia Taifa kuimairisha mahusiano kimataifa na hatimaye kujenga uchumi imara.
Aidha amewataka wahitimu kutambua kuwa elimu ni ufunguo wa maisha hivyo wakaitumie kufungua mafanikio yao na taifa kwa ujumla.
“Mtumie lugha ya kiswahili kwa wadau wa ndani na nje ya nchi ilikuongeza utafiti na ushauri elekezi ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazolikumba Bara la Afrika ikiwamo ugaidi, mabadiliko ya tabia ya nchi, mapigano ya waasi na uharifu wa bahari,” amesema Balozi Agnes.
Balozi huyo amewapongeza wanafunzi walihitimu akiwataka iwe chachu ya kujiendeleza zaidi na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Balozi Abraham Kaniki, amesema chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kukosa maeneo ya kupeleka wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo.
Aidha amesema chuo hicho kinawakaribisha wahadhiri na taasisi mbalimbali kuandika makala zitakazochapishwa kwenye jarida linaloandaliwa na chuo.
“Katika kuimarisha maofisa wa serikali na sekta binafsi ili kuendana na mabadiliko yanayotokea duniani, chuo kimeendesha kozi fupi ambazo ni Diplomasia ya uchumi, Ofisa Uhusiano na Itifaki, Itifaki na uhusiano wa Serikali, usuluhishi wa amani migogoro na amani na zinginezo,amesema.
Amesema wamezalisha mabalozi 20, waliopangiwa katika mataifa mbalimbali na watumishi zaidi ya 102 wanaofanya kazi katika Wizara ya Mambo Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda waliopangiwa ofisi mbalimbali.