25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

CHUKI ZA KISIASA ZANZIBAR ZINAFANYA MUUNGANO UCHUKIWE

NA LUQMAN MALOTO


JAMHURI ya Muungano wa Tanzania kwa uhai wake na nyakati zilizopo, mwanafasihi, Shannon Alder, angezielezea vizuri zaidi kwa maneno: “The moment you realize that no one is your enemy, except yourself.”

Tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili: Nyakati za kuukiri ukweli kuwa hakuna adui yako, isipokuwa wewe mwenyewe.

Naam, suala la Muungano linapozidi kuleta shida na kuumiza vichwa, ni vema kukiri kuwa adui wa Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar ni Watanzania wenyewe.

Shida ni kukosekana dirisha la kusikilizana na kuelewana. Upo upande ambao unaona kama unaburuzwa. Muungano wa pande mbili, kukiwepo upande wenye kuona unaburuzwa maana yake uhalali wa Muungano haupo.

Katika somo la Sayansi ya Siasa (Political Science), ‘legitimacy’ ndiyo uhalali wa mamlaka. Mbobezi wa Political Science, Malcolm Gladwell, raia wa Canada, anaielezea legitimacy kuwa hudhihirishwa na mambo matatu.

Mosi, ni watu wenye kutakiwa kutii mamlaka, wao wenyewe wajione wanayo sauti, kwamba wakizungumza wanasikika. Pili ni sheria ziwe wazi na zitabirike kwenye vyombo vya utoaji haki. Tatu ni mamlaka kufanya mambo yake kwa usawa.

Wazanzibari kwa wingi wao wanaona sauti zao hazisikiki kuelekea kwenye Muungano wenye usawa. Hivyo mambo matatu ya Gladwell, mawili, kwa maana ya mosi na tatu, yanatia dosari legitimacy ya Muungano upande wa Zanzibar.

Chuki za siasa

Mwandishi wa Marekani mwenye asili ya Ukraine, Charles Michael Palahniuk maarufu kama Chuck Palahniuk, anasema: “When we don't know who to hate, we hate ourselves.”

Kiswahili: Tunapokuwa hatujui mtu wa kumchukia, huchukiana sisi wenyewe.

Ndani ya Zanzibar ipo chuki kwamba kuna watu ni vibaraka wa Bara ambao wanatetea ukandamizwaji dhidi yao, hivyo shida kubwa iliyopo Zanzibar ni chuki ya ‘sisi kwa sisi’ kisha kuhatarisha Muungano.

Pemba kila uchaguzi huubeba kama mchakato wa kudai uhuru wao. Wanajiona kama wanakaliwa kwa mabavu. Ni kwanini imekuwa hivyo?

Sasa jiulize, ni kwanini Pemba hupiga kura ya upendo kwa Cuf na chuki kwa CCM? Wapemba wana nini ndani ya mioyo yao?

Ni kwanini misimamo ya Wapemba ipo wazi kabisa kuwa bora kupigia kura jiwe kuliko mgombea bora wa CCM?

Ni kwa vipi siasa Pemba zinabebwa kama imani kutoka mbinguni? Kwamba kuwa Cuf ndiyo njia ya Mungu na CCM ni upagani?

Zanzibar isitazamwe kwa jicho la siasa peke yake. Acha mhemko, achana na siasa za CUF na CCM, kisha itazame kwa jicho dadisi, dodosa historia, mwisho utapata jibu kuwa hatari iliyopo ni zaidi ya inavyonenwa.

Watu hawajiulizi ni kwanini Uchaguzi Mkuu 2015 wimbo ulioimbwa sana ulihusu Zanzibar na Mamlaka Kamili? Nini kilichokuwa kinatafutwa? Mamlaka kamili kutoka wapi kama si Tanganyika?

Ni kwanini wapo Wazanzibari wanaishi nje na hawataki kurudi nyumbani kwa madai kuwa nchi yao imekaliwa kwa mabavu na Tanganyika?

Chuki hii dhidi ya Muungano nani aliianzisha? Na kwanini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda mrefu imepoteza umaarufu (popularity) Zanzibar, hususan Pemba?

Nani hajui? Wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya kuundwa kwa Katiba Mpya mwaka 2014, Zanzibar kulikuwa na harakati za kutaka sauti ya Wazanzibari isikike kuhusu uhai wa Muungano.

Walitakiwa kuchagua miongoni mwa mambo matatu. Mosi Muungano uendelee kama ulivyo. Pili Muungano uwepo wa mkataba. Tatu waachwe wapumue. Je, hili nalo ni la kupuuzwa? Wanawezaje kusema waachwe wapumue kama hawajioni wanaminywa mpaka wanashindwa kupumua?

Wala Zanzibar shida si maendeleo. Katika miaka 220 ya CCM kutokukubalika Pemba, kumekuwa na jitihada nyingi za kupeleka maendeleo yenye kuonekana kisiwani humo.

Taswira ya Zanzibar imulikwe katika macho yenye kuona mbali. Macho yenye tiba na suluhu ya uhakika. Maana Zanzibar hakuna mgogoro wa kisiasa, kuna chuki.

Hali ilivyo sasa ni kuwa unapoiondoa Tanganyika hutaikuta Zanzibar, bali vitakuwapo visiwa vya Unguja na Pemba. Kama watu hawathubutu kuwaza hili basi wanafanya kosa kubwa mno la kiufundi.

Unapoutazama ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unapata jawabu kuwa ipo kazi ya kufanya kuhakikisha kuwa Wazanzibari na Watanganyika kwa pamoja wanaufurahia Muungano wao.

Lipo jukumu la kutekeleza kuhusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna kazi ambayo haihitaji kupuuzwa. Hii inahusu maoni ya walio wengi lakini wachache pia wasikilizwe, nini kinachowauma?

Mbegu ipi imepandikizwa kwenye nyoyo zao? Wazanzibari kutoka Pemba wanaumizwa na nini? Mbona Rais Ali Mohamed Shein ni Mpemba lakini hiyo haijawafanya wakikumbatie Chama Cha Mapinduzi (CCM)?

Hapo unapata jawabu kuwa hoja si Upemba, sasa kuna nini kingine? Tuzame katikati ya kichaka! Tusikariri majibu wala hatutakiwi kuongozwa na dhana.

Tusipuuze ile hoja ya kuwa kuna ‘malodi’ Uarabuni wanaifuatilia Zanzibar mithili ya fisi anavyoumendea mkono wa binadamu kwa nyuma akiamini utaanguka ale kitoweo.

Kwamba malodi waliopo Uarabuni shida yao kubwa ni kuona Muungano unavunjika na Zanzibar inakuwa jamhuri kamili. Baada ya hapo ndipo waanze kufaidi rasilimali za Wazanzibari.

Inaelezwa kuwa sasa hivi wanashindwa kuzifikia mali za Wazanzibari kwa sababu visiwa hivyo vimeatamiwa na Tanganyika. Kila hoja itazamwe kwa upana wake. Na hapa ukweli uko wapi?

Je, ni kweli kuwa chuki za Wapemba kwa CCM nyuma yake kuna mkono wa malodi wa Uarabuni? Hawalitaki zimwi linalowajua, wanataka jipya.

Hoja ya ugaidi inazungumzwa pia, nayo ipewe nafasi. Eti Zanzibar ikiachwa peke yake, magaidi watavifanya visiwa hivyo kuwa ngome yao ya kujitanua, hivyo kutanua wigo wa magaidi katika Pwani ya Afrika Mashariki, Afrika na duniani kwa jumla.

Usifanye kosa kubwa kwa kusahau kuhusu uwepo wa hofu ya kutaabika baada ya matokeo (aftermath). Kwamba Waunguja wamekuwa wakifaidi zaidi keki ya Zanzibar kuliko Wapemba tangu Muingereza na Sultan wake walipotimuliwa.

Kwamba, Waunguja wameshawafanyia mambo mengi ya hovyo Wapemba, kuwa malodi (elites) wa Unguja, wameshafanya matukio ya kuwafunga jela, kuwadhalilisha Wapemba (hasa wana CUF), wapo waliopata ulemavu wa maisha na hata baadhi kufariki dunia, hofu ipo kuwa je, kisasi kitalipwa?

Uhai wa Muungano

Kila upande hautakiwi kuwa kipofu, moja ya tunu bora kama Watanzania ni uwepo wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Matatizo yashughulikiwe kinagaubaga.

Hata hivyo, hatutakiwi kusahau kuwa zipo dola zilizoungana, zilizokuwa na nguvu kubwa ya kijeshi, kirasilimali na kimamlaka lakini ziligawanyika vipande vipande. Uko wapi Muungano wa Umoja wa Nchi za Sovieti (USSR)?

USSR walifikia uwezo mpaka wa kumiliki nyuklia. Urusi haikuwa yenye kukamatika ulimwenguni. Ni USSR na Marekani pekee zilizotamba kiuchumi na kijeshi duniani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Urusi kama baba mwenye nyumba wa USSR, inabaki kulaumu kuwa iliangushwa kwa sababu ya vita ya Ubebari na Ujamaa. Marekani bepari mkuu na Urusi mjamaa.

Ukweli upewe heshima yake kuwa hata kama Marekani ilihusika kuiparaganyisha USSR, lakini sababu ni matunda ambayo Urusi iliyatengeneza yenyewe. Kwamba dola nyingi ziliona zinapunjwa, kwamba Urusi ilizitumia kujiimarisha.

Hii dhana ya Tanzania Bara kuonekana kama inaitumia Zanzibar kujiimarisha haipaswi kuachwa ikatawala kwenye vichwa vya watu. Ni tatizo kubwa.

Wanandoa wenye maelewano huwa hawafarakanishwi na maneno ya pembeni. Ila neno la uchonganishi hupata nguvu kwenye ndoa ya watu wenye migongano. Marekani walifanikiwa kuiua USSR kwa sababu wao wenyewe ndani kwa ndani walikuwa na migongano.

Ulikuwepo Muungano mzuri wa kijamaa wa Czechoslovakia, ulikwenda na maji kisha kuacha nchi mbili Jamhuri ya Czech na Slovakia, sababu ni kama zinazosemwa kuhusu Zanzibar na Tanganyika. Slovakia iliona Czech inanufaika kuliko yenyewe.

Rejea kwenye kifo cha Muungano wa Dola ya Yugoslavia kisha uone kuwa Tanganyika na Zanzibar inaweza kuifanya Tanzania isiwepo. Muhimu ni kutambua kuwa heshima ya Muungano lazima izingatie mahitaji na matakwa ya kila upande.

Naiona hofu kuu kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu zaidi katika kuifanya Zanzibar iwepo kama dola moja. Kinyume chake zitakuwepo dola mbili, ile ya Unguja na Pemba. Maana hawaaminiani kwa sababu hawapendani na wasiopendana huchukiana.

Mimi ni mjumbe tu, nafikisha, maana atangazaye mirimo si mwana wa ruwari (mjumbe hauawi). Mvumo wa Zanzibar na chuki za siasa kati ya CCM na CUF, zinafanya chuki ya Unguja na Pemba ishamiri, kisha Muungano kuingia shakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles